Serikali ya John Pombe Magufuli chini ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imepaisha mishahara ya wafanyakazi (watumishi wa umma) nchini kama utekelezaji wa ahadi ya Rais Magufuli kwamba atawashusha malaika (wenye mishahara mikubwa) kuwa mashetani (mishahara ya kati) na kuwashusha mashetani kuishi Kama mapepo.
Mwezi Oktoba Rais Magufuli Pamoja na msemaji wa serikali waliahidi watumishi wa umma, watanzania na dunia nzima kwa ujumla kwamba baada ya uhakiki wa miaka miwili mwezi Novemba 2017 watumishi watapandishiwa madaraja, kupandishiwa mishahara na kulipwa madeni. Rais Magufuli aliwahakikishia watumishi kwamba wawe tayari kupokea neema mwezi Novemba.
Mshahara wa mwezi Novemba umetoka tarehe 24/11/2017 na watumishi wa umma wamelamba mshahara mnono kwa kupandishiwa shilingi elfu Saba, wengine elfu nane, elfu tisa na elfu kumi na tano. Mathalani, mwalimu mwenye elimu ya shahada (degree) mwenye kianzio cha mshahara (basic salary) TGTS D1 shilingi 716,000 ameongezewa shilingi 8000(elfu nane tu) sawa na alimia moja nukta moja (1.117) huku mwenye daraja TGTS E mwenye mshahara kianzio shilingi 940,000 ameongezewa kiasi cha shilingi 9000(elfu tisa tu) chini ya asilimia moja.
Ikumbukwe kwamba, mikataba ya wafanyakazi inaonesha kwamba ongezeko la Kila mwaka (annual increment) ni asilimia kumi (10 percent) na haki hiyo imefafanuliwa katika Kanuni za kudumu Utumishi wa Umma (Public Service standing orders) za mwaka 2009 Kanuni namba E.
Hata hivyo, serikali haijaongeza mshahara kwa miaka miwili yaani Julai Mosi, 2016 mpaka Juni 30,2017 na Julai Mosi 2017 kinyume cha Sheria ya Ajira na Mahusiano kazini namba 6 ya mwaka 2004 na Katiba Pamoja Kuvunja mikataba ya ajira .Kwa tafsiri nyepesi, serikali ya Rais Magufuli imepandisha mishahara ya watumishi kwa asilimia sifuri nukta tano kwa mwaka 2016/2017 na 2007/2018 yaani mwalimu mwenye ongezeko la shilingi 8000 ni sawa na kwamba ameongezewa shilingi 4000 kwa mwaka 2016/2017 na shilingi 4000 kwa mwaka 2017/2018.
Ikumbukwe Kwamba Rais Jakaya Kikwete aliongeza mishahara kwa zaidi ya asilimia kumi.Mathalani, mtumishi aliyekuwa na mshahara kianzio (basic salary) 630,000 kuanzia Julai Mosi 2014 mpaka Juni 30,2015 alipandishwa kutoka shilingi 630,000 mpaka shilingi 716,000(kianzio) huku fedha iliyobaki kutoka kwenye makato ni zaidi ya shilingi 70000/=.
Serikali ya Rais Kikwete ilihusishwa na kukithiri kwa Ufisadi, kukwepa kodi, matumizi mabaya ya fedha na madaraka na mambo mengine lakini hali ya wafanyakazi iliboreshwa na kuwapa angalu heshima inayofaa. Serikali ya Rais Magufuli imeondoa watumishi hewa, imeondoa watumishi wenye elimu ya darasa la saba, imeongeza mapato zaidi ya bilioni 500.imezuia safari za nje ya nchi, imezuia posho zisizo na maana, imepunguza ukubwa wa serikali, imekopa nje ya nchi na mambo mengine mengi lakini imeongeza mshahara shilingi 8000 kwa miaka miwili yaani 4000 kwa mwaka mmoja.
Ama kweli hongera sana Rais Magufuli kwa mishahara mnono kwa watumishi wa umma. Malaika sasa wanaishi kama mashetani na mashetani sasa wanaishi Kama mapepo. Hapa kazi tu.
Daniel Ezekiel Daniel (DED).
No comments:
Post a Comment