Mtunzi:Jimmy Luoga
Simu +255 755 714 395
EPISODE:1
Daniel ndio jina nililopewa na wazazi wangu na kubatizwa katika kanisa la Roman Cathoric lililopo katika kijiji cha Kiuma wilayani Tunduru, Baba na Mama yangu walibahatika kuwa na familia ya watoto wawili yani mimi ambaye nilikuwa mtoto wa kwanza na dada yangu Lilian ambaye alinifuata mgongini kwangu.Kwa kifupi hatukuwa na maisha mazuri kutokana na wazazi wangu kutegemea zaidi kilimo cha mpunga ambacho kilituwezesha kusogeza maisha yetu mbele, nyumba yetu iliezekwa kwa nyasi na ilikuwa mkabala kabisa na chuo cha uuguzi Kiuma.Siku zote tabia ya Mzee Ford hazikufurahiwa na Mama yangu, kwani mara nyingi alirudi usiku wa manane na kumpiga Mama tena bila hata sababu za msingi.Nakumbuka siku moja majira kama ya saa sita usiku nikiwa usingizini niliamshwa na sauti ya mtu aliyekuwa akiimba kilevilevi, haraka niliweza kugundua sauti hiyo ilikuwa ni ya nani, ilikuwa sauti ya Mzee Ford Baba yangu akiwa anatokea kilabuni.Alipoufikia mlango alianza kupiga mateke na kutukana matusi makubwa hali iliyopelekea Mama kuamka upesi na kwenda kumfungulia, lakini mara baada ya kumfungulia mlango niliweza kumsikia Baba akimtukana Mama pia akimkalipia kwanini alichelewa kumfungulia mlango, baada ya dakika kadhaa nilisikia vishindo na sauti za vyombo vikianguka hovyo pale sebuleni pia sauti ya Lilian akilia ambaye kwa wakati huo alikuwa na umri wa miaka sita na mimi kumi ilinifanya niamke niende kutazama kulikoni.La hasha! nilimkuta Baba kamkaba koo Mama huku akiwa kamkandamizia ukutani, Mama alitoa macho mithili ya mtu aliyekuwa anataka kukata roho, japo nilikuwa na umri mdogo nilijaribu kwenda kuuvuta mguu wa Baba lakini bila hata ya huruma alinipiga teke la tumboni na kunifanya nianguke chini.Hasira zilinipanda kama upepo nilichomoka mlangoni moja kwa moja mpaka kilipokuwa kinu cha kutwangia nafaka kisha nikauchukua mwichi tayari kwa lolote ili mradi niokoe maisha ya Mama yangu.Niliporudi ndani nilimkuta Baba bado kamkandamiza Mama kwa mikono yake miwili bila hata ya kumuonea huruma, niliinua ule mtwangio juu na kuuachia kichwani kwa Mzee Ford ambaye alianguka chini na kuanza kutupa miguu na mikono, sikujali hilo bali nilimtazama Mama ambaye aliakuwa anahema kwa shida huku Lilian naye akiendelea kulia, sauti ya Mama aliyoitoa kwa shida ilinisisitiza kuwa nikimbie toka eneo hilo haraka kabla watu hawafika, nilijiuliza kwanini Mama alitamka maneno hayo lakini nilipata jibu mara baada ya kugeuka na kuona Baba akiwa ametulia kimya huku damu zikiwa zimetapakaa pale chini alipolala.Ghafla nilihisi kuchanganyikiwa kwani hata nilipojaribu kumuita Baba mara kadhaa hakuitika, nilipomtazama Mama alinionyeshea ishara ya kuondoka eneo hilo haraka, kwa mbali niliweza kusikia sauti za watu waliokuwa wanakuja upande uliokuwa nyumba yetu, nilijikuta nikigeuka kumtazama kwa mara ya mwisho Mama aliyekuwa taabani kichwa chake kakiegemeza kwenye miguu ya Lilian aliyekuwa akilia, nilianza kukimbia bila ya kujua mwisho wa mbio zangu ungekuwa wapi.Niliendelea kukimbia nikiwa nafuata barabara kubwa iendayo Tunduru mjini, japo kipindi hicho wilaya ya Tunduru ilisifika kuwa na simba wala watu lakini sikuogopa hata kidogo, nikiwa nakimbia kwa mbele yangu niliweza kuona taa nyekundu ambazo kwa akili yangu ya haraka niliweza kugundua kuwa hilo lilikuwa ni gari ambalo lilisimama, niliongeza kasi mpaka lilipokuwa limesimama gari lile lakini nilipokaribia kama hatua mbili kulikuta lilianza kuondoka.Sikukata tamaa nililifukuzia kwa nyuma kisha nikadandia, lilikuwa ni scania ambalo lilikuwa limebeba mbao ambazo sikujua zilipelekwa wapi, bahati nzuri mlango wa gari hilo haukufungwa na kufuli jambo lililopelekea mimi niweze kuingia na kwenda kujificha ndani, Nilipata sehemu ya kujibanza na taratibu usingizi ulianza kunichukua na mwisho nikawa sijitambui.Kwa mbali niliweza kusikia sauti ya mtu aliyekuwa akimuongoza dereva "rudi nyuma, rudi nyuma" nilishtuka kwani nilijua hapo ningekamatwa wangenipeleka kituo cha Polis, nilitulia mule ndani huku nikitafuta njia ya kutokea, baada ya dakika kadhaa nilisikia sauti ya mtu ambaye upesi nilitambua huyo ndiye dereva wa gari hilo, alisema kuwa wasiteremshe mzigo mpaka wao watoke kula chakula.Mpaka wakati huo sikuweza kutambua mahali hapo ni wapi na ni muda gani, nilipoona kimya kimetawala pale nje ya gari nilijivuta mpaka mlangoni na kuchungulia ambapo sikuona mtu, hivyo kwa kasi kama ya umeme niliteremka garini nikiwa nimeoga vumbi mwili mzima.Kitendawili kuwa nilikuwa wapi kiliteguliwa mara baada ya kusoma bango lililokuwa kwenye jengo zuri "MTWARA HOTEL" nilishtuka kwani niliona kama sijafika mbali kiasi hicho kwa usingizi niliolalala hivyo nikahisi kama vile bado nilikuwa naota, lakini ukweli ni kwamba nilikuwa nimeingia Mkoa Wa Mtwara.Watu waliopishana nami walinitazama toka walipotokea mpaka walipoishia, sasa njaa ilianza kunikong'ota na mfukoni sikuwa hata na shilingi, nilitembea mpaka kwenye mgahawa mmoja ambao nje alikuwa mzee mmoja aliyevalia kanzu yake nadhifu huku akiwa na birika kubwa la kahawa na kashata mezani ambapo nilijua kuwa yeye ndiye muuzaji, nilimsogelea yule mzee kisha nikamsalimia lakini mzee huyo aliitikia bila hata ya kunitazama, nikarudia tena yule mzee akanijibu kwa ghadhabu tena lafudhi ya kimakonde "we ntoto unataka kuniibia nini? mbona nneitikia".Nikiwa nataka kumjibu yule mzee alitokea mpemba mmoja ndani ya ile hotel "dogo una matatizo gani mbona umechafuka hivyo?" swali la huyo mpemba lilinipa fursa ya kujieleza shida yangu, akaniita ndani kisha akaamuru nipelekewe chakula ambacho mimi ningehitaji, alipikuja mhudumu niliomba aniletee ugali samaki ambao haukuchukua muda ukaletwa mezani.Haikuchukua dakika kumi niliuporomosha ule ugali wote na kuwaacha hoi wateja na wahudumu wote, "muongezee sahani nyingine" yule mpemba aliamuru tena, nilijikuta nikichekea moyoni kwani ni kweli ule ugali niliona kama vile uliishia kooni tu kutokana na njaa niliyokuwa nayo, chakula cha awamu ya pili nilikula taratibu mpaka nikakimaliza.Baada ya kumaliza yule mpemba alikuja mpaka pale nilipokuwa nimeketi kisha akaja kukaa kiti cha pembeni yangu "unaitwa nani vile?" swali la mpemba huyo lilinifanya nibadilishe jina kwani niliogopa kutafutwa kupitia vyombo vya habari, hivyo nikabadili jina toka Daniel na kumtajia jina la Erick, yule mpemba alijaribu kuniuliza maswali mengi lakini nilimjibu kuwa sikuwa na wazazi wala ndugu.Baada ya maongezi ya hapa na pale akahaidi kunipa kazi ya kumuuzia Ice Cream mtaani pia akanihakikishia kunipa makazi nyumbani kwake jambo ambalo sikulipinga na pia niliona ni heri kwangu.Toka siku hiyo nilianza kuishi nyumbani kwa yule mpemba na kufanya biashara ya kuuza Ice Cream mtaani, siku zilisonga mpaka nikamaliza mwaka mzima namfanyia biashara yule mpemba.Sitoisahau siku ambayo mke wa mpemba huyo alisafiri na watoto wake wote kwenda kusherehekea sikukuu ya idi huko kwao Pemba, majira ya saa nne usiku nikiwa nimelala aliingia yule mpemba chumbani kwangu kisha akataka kuniingilia kinyume na maumbile, nilimpiga teke moja kwenye nyeti zake kisha nikatoka mbio nikimwacha kaanguka chini akiwa analia kama mtoto.Moja kwa moja nilikwenda mpaka bandarini ambapo niliamini asubuhi ya siku hiyo lazima ningezamia Meli iendayo Dar es salaam japo mfukoni sikuwa na hata shilingi moja......
Je nini hatma ya mtoto Daniel ambaye amebadili jina lake na kujiita Erick? Ungana nami Jumamos ili kupata uhondo huu.