Showing posts with label MAHUSIANO. Show all posts
Showing posts with label MAHUSIANO. Show all posts

Tuesday, 14 February 2017

MAPENZI MUBASHARA: ZAWADI GANI YAFAA ZAIDI SIKU YA VALENTINE?JE,WAJUA HISTORIA YA SIKU YA WAPENDANAO (VALENTINE DAY)? JIFUNZE HAPA

Imeandaliwa na: Thobias Omega

KUNA HISTORIA TOFAUTI TOFAUTI KUHUSU CHIMBUKO NA MAANA HALISI YA SIKU YA WAPENDANAO, JIFUNZE ZAIDI KUPITIA HIZI ZIFUATAZO:

HISTORIA #01
Historia ya siku ya valentine imetokana na Mtakatifu, Mchungaji/Askofu wa Kanisa katoliki wa miaka ya 496 baada ya Kristo ambaye aliitwa Valentine. Wengine wanamtaja kama Askofu wa kiprotestanti wakati wengine wakimtaja kama a Mtakatifu Padre/Askofu wa Kikatoliki ambao kwa pamoja wana historia iliyofanana. Hata ndani ya Katoliki bado kulikuwa na kutofautiana kwa kumfananisha na kuhani wa huko Roma na askofu wa Temin na wa tatu ni Mchungaji wa Kiprotestanti ambaye taarifa zake hazijulikani ila inaaminika aliishia Afrika katika utumishi wake.
Katika kipindi hicho Papa Gelasius alidhamiria kumuenzi Valentine kwa kuweka siku ya 14 Februari kama siku ya wapendanao duniani.
Historia inaeleza kuwa Askofu Valentine alikuwa akifundisha na kufungisha ndoa za siri kwa vijana wadogo wapendanao ambao walipigwa marufuku kuoana katika sheria za kirumi wakati huo kwa sababu walikuwa bado ni wadogo.
Kwa sababu Valentine alikirimiwa na Mwenyezi Mungu karama za uponyaji, afisa mmoja wa magereza ambaye binti yake alikuwa ni kipofu aliposikia uwezo uliwekwa kwa Askofu Valentine ya uponyaji, alimwendea na kumuomba amponye binti yake apate kuona tena. Valentine alifanya hivyo kwa nguvu za Kimungu na binti huyo akapona na tangu hapo binti wa afisa wa magereza alimpenda Askofu Valentine na wakawa marafiki wa karibu.
Dola ya kirumi iligundua kuwa Valentine alikuwa akifundisha na kufungisha ndoa kwa vijana ambao bado ni wadogo kinyume na sheria za kirumi ambayo ilikataza vijana wadogo kuoa au kuolewa mpaka wakue wakubwa, dola ya kirumi ilimkamata na kumweka ndani mpaka hukumu yake itolewe.
Baadaye valentine mwingine alitokea akampenda binti wa afisa wa magereza lakini maelezo yake haikupewa umuhimu na wanahistoria. Kwa hiyo tarehe 14 Februari kila mwaka ikawa ni siku ya wapendanao duniani. Lakini siku hii ilikuja kuwekwa rasmi kuanzia karne ya 14.
Siku ya valentine ilikuwa kwa umaarufu na ukubwa na katika miaka ya hivi karibuni iligeuka na kuwa ya kibiashara zaidi kwa kuuza kadi nyingi za valentine.


__________
HISTORIA #02
________________
Siku ya wapendanao ni sikukuu ambayo huadhimishwa kila ifikapo tarehe 14 Februari ya kila mwaka (Valentine Day).
Historia yake imeanzia karne ya 3 huko Roma ambapo alikuwapo padri Valentinus ambaye akaja kuheshimiwa kama mtakatifu hasa tarehe hiyo.
Hadithi zilizosababisha sikukuu kuenea
Inasemekana kwamba Kaisari wakati huo alikuwa Claudius II: yeye aliona kuwa askari mkakamavu na bora zaidi ni yule asiyeoa wala kuwa na familia (kapera). Hivyo alipiga marufuku ndoa kwa askari.
Valentinus alipinga jambo hili hivyo kuendelea kufungisha ndoa kwa siri. Mfalme Claudius alipopata habari hizi aliamuru Valentinus akamatwe na kuuawa.
Kuna hadithi nyingine ya kuwa akiwa gerezani Valentinus aliandika barua ambayo ilikuwa na salamu za kwanza za Valentine kwa binti aliyekuja kumsalimia gerezani; mwisho wa barua alihitimisha kwa maneno haya: Kutoka kwa Valentinus wako.
Toka hapo Valentine anakumbukwa kama mtetezi wa wapendanao na sikukuu yake kuadhimishwa kote duniani.

HISTORIA #03

Siku ya Valentines Day asili yake ni kutoka Dola ya Warumi. Ni siku ya kumbukumbu (memoria day) na sehemu nyingine ni (festum) maana yake siku kuu ya daraja la kwanza kwa kumkumbuka Padre Valentine aliyeuawa na utawala wa kirumi sababu ya kutetea waumini wake kufunga ndoa badala ya kuishi na vimada tu. Lakini sikukuu hiyo imeenea sana katika nchi za magharibi na baadaye karibu sehemu kubwa ya ulimwengu kuisherehekea kama siku yamapenzi kinyume cha dhamira ya Mt. Valentine.
Watawala wa dola ya kirumi walikuwa na fikra za kueneza dola ya kirumi duniani kote na hivyo vijana hawakutakiwa kuoa, ili wawe huru muda wote kwenda vitani kupigania nchi. Wakioa hawangekuwa na uhuru wa kwenda vitani bali kuwa na famiia zao. Vijana wengi wakawa na mtindo wa kuwa na vimada tu kitu ambacho kanisa lilikukwa linapinga.
Padre Valentine ambaye alikuwa Roma akawa anawahimiza vijana kufunga ndoa badala ya kufanya ngono bila ndoa kwani ni dhambi na kitu kisichokubalika mbele ya Mungu. Akawa anafungisha ndoa kwa siri kwenye makatakombe (mahandaki chini ya kanisa ambako kuna sehemu za ibada kwa watu wachache), alifanya hivyo kwa vile kufunga ndoa hadharani ilikuwa ni kukiuka amri ya wakuu wa dola ya kirumi.
Baadhi ya watu walifichua siri hiyo, hivyo Padre Valentin alishikwa na dola ya Warumi na kuuawa kama shahidi mfia dini kwa ajili ya kutetea waamini wake wafunge ndoa badala ya maisha ya ngono zembe bila ndoa.
Wakristo wakawa siku ya kumkumbuka Padre Valentin kama mfia dini sababu ya kutetea maisha ya wanakanisa kuwa wanandoa. Ikaenea katika kanisa nchi za magharibi na hata duniani ambako wanakanisa wanamkumbuka Mt. Padre Valentin. Baadaye ikapokeleka na watu hata wasio na imani ya kikristo kama ni siku ya kufanya kumbukumbu kwa Mt. Valentin kama mteteze wa Ndoa.
Maudhui ya siku hiyo kwa wasiowanakanisa imechukua maana nyingine ya kwamba ni siku ya wapendanao hata kwa wasio wanandoa bali mradi wanapendana, kitu ambacho ni kinyume cha malengo ya mfia dini Mt. Padre Valentin aliyetaka vijana wafunge ndoa badala ya kuwa na hawara tu (vimada).

HISTORIA #04
Asili yake ni sherehe ya kipagani iliyoanzia mjini Rome Italy.Ikaingia kuwa ya kidini na sasa imekuwa ikitumika kama ni msimu wa kufanya biashara huria ambapo biashara za vyakula na mapambo ya maua, dhahabu na vyakula kama chakleti huchangamka sana.
Warumi wa kale walisherehekea siku za tarehe 13,14 na 15 kwa matambiko mbali mbali yenye lengo la kutafuta uzazi kwa jina la siku ya Lupercalia.Wanyama wa kila aina walichinjwa ambapo vijana wa kiume walijitapakaza damu zao na kubeba mikia ya wanyama hao huku wakiwa uchi na kufukuzana na wasichana huku wakiwapiga migongoni kwa lengo na kukuza urutuba wa uzazi.Warumi hao waliamini kuwa muasisi wa mji wa Rome anayeitwa Romulus siku moja alinyonyeshwa na mbwa mwitu na ndipo akawa mwenye hekima na shujaa.
Ukristo ulipoingia Rome pole pole sherehe hizi ziliingia ndani ya mafundisho ya dini.Kwa mfano yapo masimulizi kwamba Valentine alikuwa ni kasisi (bishop) mnamo mwaka 197 A.D wa mji wa Interamna ujulikanao sasa kama Terni.Kasisi huyo aliuliwa na viongozi wa kijamii baada muda mfupi kutokana na imani yake ya kikristo.Inaaminika alikufa siku ya Februari 14.
Kisa kingine kinamtaja kasisi mwengine wa mji wa Rome kwa jina la Valentine ambaye naye inaaminika aliuwawa Februari 14.Kosa lake la mwanzo linatajwa kwamba akiwa jela aliweza kumponya upofu motto wa afisa gereza ambaye baadaye akafanya mahusiano naye ya kimapenzi.Alikuwa akiandikiana barua naye kwa kutumia damu yake kama wino.Hiyo barua ikiweka saini yake kama “From your Valentine”.Kisa kingine cha kufungwa kwake inasemekana mtawala wa Rome wa wakati huo Claudius alikuwa amekataza wavulana kuoa ili awe na askari wazuri.Kasisi Valentine aligundulika kufungisha ndoa kwa siri ikabidi akamatwe.
Mnamo mwaka 496 A.D papa wa wakati huo Gelasius kwa kuvutiwa na wimbi la sherehe za siku ya Valentine akaamua kwamba kila Februari 14 iwe ni siku ya sherehe ya kikristo kwa ajili ya kumuadhimisha St.Valentine.
Kuifanya Februari 14 kama siku ya wapendanao kulipata nguvu zaidi mwaka 1382 wakati Richard П wa London alipotangaza uchumba na Anne wa Bohemia.Richard aliandika “For this was on St. Valentine's Day/ When every fowl cometh there to choose his mate.”.
Mwaka 1400 A.D mahakama maalum ilifunguliwa siku ya Valentine kushughulika na kesi mbali za mambo ya mapenzi kuhusiana na wachumba kupigana,kuachana na mateso mengine ya kimapenzi.
Kufikia mwaka 1601 sherehe za Valentine zilikuwa zimezoeleka sana katika maisha ya kawaida kiasi kwamba William Shakespeare aliandika katika shairi lake
“To-morrow is Saint Valentine's day,/All in the morning betime,/And I a maid at your window,/To be your Valentine.”.
Utaratibu wa kutumiana kadi za mapenzi ulianza rasmi mwaka 1847 jijini London wakati shughuli za uchapishaji ziliporahisika.Mwaka 1929 kwa mara nyengine sherehe za Valentine zilileta janga kubwa pale magenge matano jijini Chicago,Marekani yalipopigana na kuuana kwa risasi kuhusiana na mambo ya mapenzi.
Katikati ya ya miaka ya 1980 makampuni ya madini na biashara nyenginezo yalianza kuziteka nyara sherehe za Valentine kwa kuhamasisha watu kununua bidhaa zao.
Ukweli Kuhusu Siku Valentine, Tarehe 14 Februari
1. Zaidi ya kadi milioni 1 sawa na 25% ya kadi zote huuzwa nchini Marekani tu.
2. Siku ya valentine ni ya pili kwa ukubwa na umaarufu baada y a Krismasi
3. Siku ya valentine huazimishwa kila mwaka tarehe 14, Februari
4. Inakadiriwa kuwa zaidi ya kadi za valentine milioni 50 huuzwa duniani kote
5. Kadi za valentine kwa umuhimu : huuzwa zaidi kwa waalimu, watoto, wamama, wake, na wapendanao

Alama Mbalimbali za Kadi ya Valentine na Maana Zake

Moyo — Ni alama ya upendo, inamaanisha kutoa moyo wako kwa umpendae, moyo kuchomwa na malaika mdogo ni ishara kwamba ukimpa moyo wako umpendae tegemea hatari ya kukataliwa.

Malaika mdogo — huyu malaika mdogo kwa kingereza anaitwa Cupid ambaye ina asili and utamaduni katika dola ya rumi na ikiwa na maana ya mungu wa upendo. Inaaminika kuwa, yeyote aliyechomwa na huyu malaika (mungu wa upendo) hatakufa bali ataangukia katika mapenzi

Ua waridi — Waridi ni ua maarufu duniani kwa kupeana nyakati za sikukuu na yenye alama ya uzuri.
Ua waridi huja na rangi mbalimbali na zote zikiwa na maana tofauti.
Nyekundu: ni upendo au mapenzi,

Manjano: kwa ajili ya urafiki na uwazi,

Nyeupe : ikiwa na maana ya pendo la kweli na uwazi,

Pinki: ni rangi ya urafiki na wapendanao,

Nyeusi: inamaanisha kuagana kwa wapendanao

Zawadi Zinazotolewa pamoja na Kadi ya Valentine

Mara nyingi, kadi ya valentine inatumwa na zawadi. Ni vigumu kuandika hapa ni zawadi gani utatuma na kadi hii kwani inategemea sana mguso wa mtu binafsi , jinsia, sababu, majira nk.
Angalia hapa chini baadhi ya zawadi zinazotumwa pamoja na kadi ya valentine
Pochi, Saa, Simu, Pipi, chocolate, mikufu, pete, shati, vitu vya urembo vya kuvaa vilivyonakishiwa kwa vito vya dhamani na dhahabu, begi, ua waridi ambalo halijanyauka, Mengine unajua mwenyewe au utaongozwa na mazingira na hali halisi.

Thursday, 12 January 2017

Sababu Kuu 10 za Ugomvi kati ya Mke na Mme Katika Mahusiano



Wawili hao wanapoaanza kujenga mahusiano na kukaa pamoja kama familia,kuna vitu kadhaa ambavyo kila mmoja wao huvitazama tofauti na hivyo kuleta migongano. Migongano ambayo inaweza ikarekebishika kama wenza hao watamua kuifanyia kazi na kuelewana.
Kuna vitu vingi ambavyo husababisha ugomvi na migongano ndani ya mahusiano ya mke na mme na hapa tunaeleza sababu kuu ambazo kwa kawaida hutokea karibu katika kila mahususiano

1. Wivu na Kukosa Kujiamini

Wivu unatokana na jinsi ambavyo mpenzi mmoja anavyohusiana na watu wengine wa jinsia tofauti. Inaweza ikawa marafiki,wafanyakazi wenza au wapenzi wa zamani. Vyovyote vile itakavyokuwa ni kwamba wivu unasababisha ugomvi katika mahusiano mengi.
Kunatakiwa kuweka mipaka ya kutosha na iliyo wazi ili kujenga uaminifu kwa mpenzi wako na kumpa kujiamini. Mpenzi ambaye hajiamini ni tatizo kubwa kwani uwezekano wa kuanzisha ugomvi ni mkubwa.Hivyo ni vizuri ukamjengea mweza wako katika mapenzi kujiamini kwa kuwa mwaminifu.
Uaminifu ni kitu kimoja kikubwa sana katika mapenzi. Kama mwenza wako akikuamini hakutakuwa na wivu wa kupita kiasi na pia atakuwa anajiamini kuwa yeye peke yake ndio chaguo lako na hakuna mwingine.

2. Mawasiliano Finyu

Mawasiliano yanapovunjika katika mahusiano ugomvi ni kitu cha kawaida kutokea.
Mawasiliano ya kawaida kati ya wapenzi husaidia sana kutoa wasiwasi wa nyendo za mwenza wako. Huleta amani na kujenga uaminifu kwa mpenzi kwako.
Kuzungumza juu ya mipango yako ya mendeleo kama ujenzi au biashara ni vitu ambavyo ni muhimu sana kuvifanya vinginevyo utajenga wasiwasi kwa mweza wako na itasababisha ugomvi wa mara kwa mara.
Kuwa muwazi kwa mipango ya maendeleo binafsi,ya familia yako na ndugu.
Utafiti unaonyesha kuwa wapenzi wanaoongea na kusikilizana mara kwa mara hawagombani mara nyingi kama wale wasio na mawasiliano ya kutosha.

3. Masuala ya Fedha

Japokuwa fedha si msingi wa mapenzi,lakini ni kitu ambacho kinahitajika sana katika maisha ya kila siku ya kila mtu na ya familia. Na kimekuwa ni mojawapo ya vitu ambavyo wapenzi katika mahusiano au ndoa hugombana sana juu yake.
Mwenza mmoja anapokuwa mtumiaji mbaya wa fedha na mwingine siyo,huibua malalamiko na ugomvi. Baadhi ya wapenzi hasa wanawake hawataki kuchangia kwa kiasi kikubwa katika mahitaji ya msingi ya nyumbani na badala yake kuwaachia mzigo mkubwa wanaume.
Hili linaibua malalamiko mengi kwa baadhi ya wanaume,na wakati ungine toka kwa wanawake. Matumizi makubwa ya fedha kwaajili ya pombe na sharehe nyingine kwa wanaume na baadhi ya wanawake kumekuwa mojawapo ya sababu za ugomvi juu ya fedha katika mahusiano.
Ni muhimu kwa wenza wawili kupanga jinsi ambavyo fedha zao zitapatikana na kutumika. Vipaumbele vya kufanyika kwanza na kiasi cha kutumika kwajili ya starehe na urembo kwa wanawake kwa mfano.

4. Masuala ya Familia

Familia ya nani ianze kwanza na ipi ifuate ni tatizo kubwa katika mahusiano. Upendeleo wa upande mmoja ambao kwa asili huwa unatokea tu ni chanzo cha ugomvi ndani ya nyumba.
Mitazamo tofauti kati ya mmojawapo katika wapenzi na familia ya mwenza wake husababisha kutoelewana kwa wapenzi hao ndani ya nyumba.
Mbaya sana inakuja pale wanandugu wanapoingilia mambo ya ndani ya nyumba yenu. Wazazi wa kike na mawifi mfano, wamejulikana kusababisha matatizo mengi kwenye familia za watoto na kaka zao.
Kuepukana na hili ni muhimu kwa wapenzi ndani ya nyumba kuweka mipaka kwa ndugu ambayo haitaathiri uhusiano nao kama ndugu.
Pia ni muhimu kwa wenza hao kuweka mikakati ya pamoja juu ya kuhusiana nakusaidia ndugu toka katika familia zao mbili.

5. Suala la Unyumba

Japo kuwa suala kufanya mapenzi si kila kitu kwa wapenzi ndani ya nyumba lakini linachangia sana katika kuleta ugomvi aina yao. Kufanya mapenzi kupita kiasi au mara chache kunaleta matatizo kwa wapenzi hasa ambao wana uhitaji tofauti.
Wengine wanaona kama mpenzi ambaye hahitaji kufanya mapenzi mara nyingi na mwenzake labda anauhusiano na mtu mwingine zaidi yake. Au hamvutii tena kama zamani na huenda akaanza kuangalia nje.
Hii inajenga kutojiamini na kupoteza uaminifu,ambalo ni tatizo jingine kubwa katika mahusiano kama tulivyoonesha mwanzoni.

6. Vipaumbele katika Maisha

Wapenzi wawili wanapokuwa na mipango na malengo tofauti ni tatizo kubwa. Watu wanapokuwa katika uhusiano ambao ni wa kuishi daima,malengo na vipaumbele vyao ni lazima vioanishwe na juhudi za kila mmoja zilenge katika kufanikisha mipango hiyo ya pamoja.
Kunapotokea kuwa kila mmoja ana malengo tofauti basi hata vipaumbele vitakuwa tofauti na hapo ndipo shida zinapoanzia.

7. Uaminifu

Uaminifu katika mahusiaono ni jambo la muhimu sana. Bila uaminifu ni ngumu sana kwa mahusiano yoyote kudumu.
Uaminifu ni kitu ambacho hujengwa kwa muda mrefu na kikipotea ni ngumu sana kukirudisha. Japo inawezekana kujenga upya uaminifu lakini huchukua muda mrefu sana.

8. Wapenzi,Marafiki na Maisha ya Zamani

Mojawapo ya vyanzo vya ugomvi kati ya wapenzi ni wapenzi wa zamani. Mawasiliano ya aina yoyote na wapenzi wa zamani huleta wasiwasi mkubwa kwa mpenzi wa sasa. Ni kitu ambacho wapenzi wawili wanahitaji kuongea na kupanga jinsi ya kuepukana na matatizo ambayo yanaweza kusababishwa na historia zao za maisha.
Kuepukana na hii ni vyema kuvunya uhusiano wa aina yoyote na wapenzi wa zamani labda tu kama wapenzi hao ni wazazi wenza au mnafanya kazi pamoja na ni ngumu kutokuonana au kuwasiliana.
Suala linalofanana na hili ni uhusiano na baadhi ya marafiki wa jinsia moja ambao wanachukuliwa kuwa mfano mbaya na mpenzi wako. Kama haiwezekani kutowasiliana na kuonana na wapenzi wa zamani au marafiki, basi ni vyema wakawa marafiki wa familia nzima na mawasiliano yoyote kati yenu nao yawe wazi pasipo kificho.

9. Watoto

Suala la uleaji na ukuzaji wa watoto linasababisha ugomvi mara nyingi kati ya wazazi. Jinsi gani mtoto avae au shule ipi aende linapelekea wazazi wengi kugombana.
Ni jambo la muhimu sana kukubaliana juu ya mambo ya msingi juu ya malezi ya watoto. Tofauti za wazazi ziangaliwe kwanza vinginevyo zitaingilia malezi ya watoto na kusababisha ugomvi juu yao.

10. Kazi za Nyumbani

Imekuwa kama utamaduni kwa waafrika kuacha kazi nyingi kama si zote za nyumbani kwa mke. Kwa Wanawake ambao wanafanya kazi pia inakuwa ngumu sana. Hili linasababisha pia ugomvi kwa wapenzi nyumbani. Kama nguo ambazo mume anazivaa na kuzichafua tu bila ya kujali kuwa mweza wake ataumia wakati wa usafi na ikiwa yeye mwenyewe hajishughulishi na kufanya baadhi ya kazi za nyumbani ni wazi itasababisha ugomvi.
Ni vyema wanaume kuchukua baadhi ya majukumu nyumbani hata kama kutengeneza bustani au kulisha chakula mifugo.

Faida ya Ugomvi kati ya Mke na Mme Katika Mahusiano

Japokuwa ugomvi ni kitu cha kuepuka,lakini kina uzuri wake katika mahusiaono kama kikichukuliwa vizuri na kutumika kama kioo.
Kama mtu anagombana na mpenzi wake kwa madhumuni ya kuboresha ni kitu kizuri. Hii inaonesha kuwa anahitaji kuwa na wewe na anahitaji amani.
Ugomvi na mifarakano pia inatoa nafasi kwako kujiangalia vizuri na kama kinacholalamikiwa na mwenzio kina ukweli basi ni nafasi ya kujirekebisha.
Ni mategemeo kuwa kuna kipindi ambapo ugomvi utakuwa mkubwa na baadae wapenzi hao wataelewana na kurekebisha mambo yao.
i.  Ugomvi Unatoa Nafasi ya Kuongea Mambo Magumu
Wakati mwingine mazungumzo ya kawaida hayatoi nafasi ya wapenzi wawili kusema yale ya ndani na yanayozizonga nafsi zao. Ugomvi hufungua milango ya hisia za ndani na huenda vyanzo vya matatizo vikawekwa wazi na hivyo kufanyiwa kazi.
ii. Ugomvi unaonyesha Kuwa Mnajali na Mnataka Maboresho
Katika uhusiano ambao wenza hawajali,au hawana malengo ya muda mrefu huwa hawatoi duku zao juu ya utofauti na wapenzi wao.Hivyo wapenzi wanaogombana wanaonesha kuwa wana nia ya dhati na mwenzao na sio tu kupitisha muda.
iii. Ugomvi Unaboresha Uhusiano
Kwa muwa ugomvi unaibua hisia zilizojificha toka kwa wapenzi,ni wakati mzuri kuona matatizo ya kila mmoja. Na kama wapenzi hao wana nia ya dhati ya kuwa pamoja basi watafanyia kazi tofauti na mataizo waliyonayo. Hivyo kuboresha mahusiano yao