Thursday, 27 April 2017
NYUMBA YA MAAJABU: 51
“Yuko wapi mumeo?”
“Hata sijui alipo bibi”
“Je, unahisi kuwa bado yupo kwenye nyumba yenu?”
“Sijui bibi, yani mimi na yeye tumeachana kwenye mazingira ya kutatanisha sana”
“Pole sana ila angalia nyuma kwanza”
Sophia akageuka nyuma na kumuona Ibra, kwakweli alishtuka sana.
Sophia akasema kwa sauti,
‘Si Ibra yule!”
Bibi naye akajibu,
“Ndio ni yeye, haya twendeni atatufata tu nyuma”
Wakaendelea kufatana na yule bibi hadi walipofika nyumbani kwake, kisha akawakaribisha
“Hapa ni nyumbani kwangu, karibuni sana. Hapa naishi peke yangu”
Walikaribia, ilikuwa ni nyumba ndogo tu ya vyumba viwili, Sophia aliamua kumuuliza huyu bibi kuwa kwanini anaishi peke yake kwani alimuona ni mzee sana kuishi mwenyewe ila huyu bibi hakujibu zaidi ya kucheka kisha akawaambia wamsubirie Ibra waliyemuona nyuma yao na muda kidogo tu Ibra aligonga mlango wa yule bibi ambapo alikaribishwa pia kwahiyo wote walikuwa kwenye sebule ya yule bibi ambapo kulikuwa na mikeka ya kutosha na kuwawezesha wote kukaa.
Huyu bibi akamuuliza swali Sophia kwanza,
“Kabla ya yote naomba uniambie sababu yaw ewe kunitafuta mimi”
“Kutokana na matatizo niliyoyapata na vile ambavyo ulinieleza mwanzoni kabisa nikaona kuwa wewe ndiye unaweza kunisaidia kwasasa”
Kisha huyu bibi akamuangalia Ibra na kumuuliza swali lile lile ambalo amemuuliza Sophia ila Ibra hakuweza kujibu na alikuwa kimya sana, huyu bibi akamwambia Ibra,
“Pole sana, katika maisha tunapitia mambo mengi na kujifunza vitu vingi sana. Najua uliyoyapitia ni zaidi ya adhabu katika maisha yako, pole sana”
Ibra hakujibu kitu ila ni machozi tu yalikuwa yakimtiririka, kisha huyu bibi aliwaangalia hawa ndugu wa Sophia pamoja na Siwema na kuwaambia,
“Jamani msimfikirie vibaya kijana huyu, kwasasa hana uwezo wa kuongea ndiomana mnamuona hivyo”
Kimya kikatawala huku wakionekana kumsikitikia Ibra ila ni Sophia tu ambaye hakuonekana na huruma yeyote dhidi ya Ibra kwani mpaka sasa alitambua kwamba matatizo yote yaliyomkabili ni sababu ya makosa ya Ibra, amekosa tena uwezo wa kuzaa sababu ya Ibra kwahiyo ndio kitu kilikuwa kikimuuma sana na kumfanya asiweze kumuonea huruma mume wake.
Bibi akainuka na kuchemsha maji ambayo aliweka dawa kama unga unga hivi kisha akaweka kwenye kikombe na kuwataka wote waliofika hapo wanywe ambapo alianza kunywa yeye mwenyewe kwanza na kuwapa wanywe wengine, wote walikunywa ile dawa kisha huyu bibi alikaa sasa na kumuangalia Sophia kisha akamuuliza,
“Unakumbuka kipindi ambacho ulikuwa ukiamka unakuta vyombo vyako vimeoshwa, mara nyingine umeshapikiwa chakula. Siku nyingine unakuta nguo zako zimefuliwa na kuanikwa kisha kuanuliwa na kupangwa kabatini unakumbuka?”
“Nakumbuka ndio, na nilikuwa nikishangaa sana”
“Je ulihisi ni nani aliyekuwa akifanya matukio hayo?”
“Mwanzoni nilikuwa nikihisi ni mume wangu”
“Ila je tabia za mume wako huzijui kwani? Hukujiuliza amewezaje kubadilika gafla vile?”
“Kwakweli sikujua tena kuna kipindi hadi nilikuwa nikigombana nae kwani nikimwambia yeye ndio amefanya akawa anakataa, nikajaribu kuomba ushauri kwa dada hapa akasema itakuwa mume wangu kaamua kunionyesha upendo wa dhati”
“Pole sana, katika maisha huwa tunatakiwa kutafakari kila tunachokiona mbele yetu na kujua mantiki ya kitu hiko. Mungu ametuumba na akili kwa makusudi kabisa ili tuweze kuchambua mambo, unajua ulitakiwa uwe na mashaka pale tu mumeo anapokukatalia kuwa si yeye kuliko kujiwekea imani kuwa ni yeye wakati kashakuambia kuwa si yeye. Ngoja nikufundishe kitu”
Wote walitulia kimya kabisa wakimsikiliza huyu bibi, kwa muda huu aliweza kuwaeleza toka siku ya kwanza walipoingia kwenye ile nyumba mpaka yale mauzauza yaliyokuwa yakiwapata mwanzoni,
“Siku nilipokutana na wewe Sophia niliweza kuona maisha yenu kwenye ile nyumba na ndio maana nilikwambia kuwa nyumba unayoishi ni nyumba ya maajabu ila ulibaki kushangaa tu na kuitana na dada yako huku mkinihisi mimi ni mchawi. Lengo langu lilikuwa ni kuokoa maisha yako ila kwa muda huo hukuchagua kunisikiliza”
Sophia alitokwa na machozi kwani alikumbuka vizuri siku ya kwanza kukutana na huyo bibi na jinsi alivyomwambia kuwa nyumba anayoishi ni nyumba ya maajabu, Sophia aliongea kwa uchungu muda huu na huyu bibi
“Kwakweli bibi waswahili walisema usilolijua ni sawa na usiku wa giza, kipindi hiko sikuelewa maana ya methali hii ila sasa nimeelewa. Ni kweli uliniambia wazi kabisa kwamba nyumba ni ya maajabu ila hata sijui kwanini sikusikiliza maneno yako au hata kukutafuta na kuhitaji ufafanuzi zaidi. Sasa nimebakiwa na kovu zito lisilo na mwisho”
“Pole sana, ila nataka kukufundisha kitu. Huruma ni kitu chema sana katika maisha ila kinachotakiwa ni kupima huruma zetu, kuna watu walikaribisha watu ndani kwa huruma kumbe walikaribisha majambazi. Nchi yetu ina sheria zake pale upatapo mgeni usiyemtambua, kama nyie mlimkaribisha mtu ndani asiyekuwa mtu”
Sophia akadakia hapo na kumuuliza kuwa Neema ni nani, na kama ni mtu basi ni mtu wa aina gani.
Bibi alitulia kwanza kisha akawaeleza kwa kifupi kuhusu historia ya Neema,
“Kwanza kabisa napenda mfahamu kwamba Neema si mtu wa kawaida kama mnavyofikiria”
Wote wakashtuka na kusikiliza kwa makini,
“Neema alishakufa miaka ya nyuma huko, hata kaburi lake ukienda kufukua utakutana na mifupa tu. Ila jambo linaloendelea kwa Neema ni kisasi alichojiwekea kabla ya kifo chake.”
Sophia akakatisha mazungumzo kwanza na kuuliza,
“Kwahiyo Neema ni marehemu? Yani sisi tulikuwa tukiishi na marehemu ndani?”
“Neema alikufa siku nyingi, na pale alipo ni jini. Ngoja nikupe tabia za majini, kama umekuwa makini basi ushawahi kusikia kuwa kuna majini wazuri na majini wabaya. Na hawa majini huwa ni kutokana na ulivyokuwa tangu hapa duniani. Majini wabaya wao wamekaa makini sana kuingilia watu wenye tabia mbaya, ndiomana unaweza kukuta mtu ana tabia za ajabu na gafla zimezidi kupita za mwanzo ujue jinni mbaya ameshamuingia na yote hiyo ni sababu ya tabia aliyokuwa nayo toka mwanzo”
Huyu bibi alinyamaza kwanza kisha akaenda kuchukua majivu na kuwapaka kila mmoja mule ndani na kuwaambia sababu ya kuwapaka bile,
“Nimewapaka kwa tahadhari tu maana tunaongelea vitu hatarishi na watu ambao walishakufa siku nyingi sana. Mkaa ni dawa sana, ndiomana hata kama unahisi kuna watu wanafanya chuma ulete kwenye biashara yako ukaamua kuweka mkaa kwenye pesa zako basi hawatachukua hizo pesa tena. Mambo mengine sio lazima uende kwa mganga wa kienyeji ila ni maarifa tu, kama mkaa ni dawa basi majivu nayo ni dawa pia”
Humu ndani wakaishia kutazamana tu kwani hawakuwahi kufikiria kuhusu hiki kitu, kisha huyu bibi akaendelea kuwaeleza,
“Maisha ya Neema yalikuwa ni maisha ya visasi sana yani yeye akifanyiwa ktu lazima alipize na ndiomana imekuwa rahisi kwa majini wabaya kumtumia vilivyo ingawa amekufa na hiyo inapelekea hata marehemu kutokupumzika kwa amani sababu duniani unatumiwa vibaya. Unakumbuka mtu aliyekusaidia hadi ukarudi nyumbani kwenu?”
“Nakumbuka ndio, je nay eye alikuwa ni mtu kama sisi?”
“Hakuwa mtu pia ila ni jinni, yupo kwenye mwili wa mtu aliyekufa siku nyingi sana ila mtu huyu hakuwa na kisasi chochote juu ya mtu yeyote ingawa aliishi maisha ya shida sana ila hakuwa mtu mbaya. Na kilichomuua ni kitendo cha kulala na kaka yake ingawa hakujua kama ni kaka yake mwanzoni, hiko ndicho kilichopelekea kifo chake ila bado hakufa kwa kinyongo. Kuna baadhi ya vifo watu wanapokufa hutumiwa na majini, hapo ndio inategemea na tabia yako ilivyokuwa na ndiomana yule alikusaidia wewe kwani hakupenda kuona unakufa bila sababu ya msingi. Na je unajua kilichompata baada ya kukusaidia wewe?”
“Nini kimempata?”
“Ni mateso, ila mateso haya yataisha baada ya sisi kumaliza tatizo kuu la mtu mmoja wa visasi aitwaye Neema ambaye si Neema halisi bali ameshavaliwa ndani ya jinni mbaya”
Wote walikuwa kimya kabisa kwani hakuna aliyeweza kumuelewa moja kwa moja huyu bibi.
Bibi aliendelea kuelezea sasa na alimpa Sophia maelezo yale yale ya Ibra kukataa mimba ya mdogo wake Neema,
“Ila jiulize kwanini mtu ambaye anafanyia mabaya sio huyo Nancy? Ni kwasababu alikufa na kuyaacha yote duniani, hakutaka kuondoka na kinyongo na alijiona kuwa anastahili kufa. Tofauti na upande wa Neema, kwanza kabisa alikuwa na hasira na Ibra kwa kusababisha kifo cha mdogo wake na pia alipatwa na matatizo yaliyomfanya sfe kwa kinyongo sana, mwisho wa siku ameweza kutumiwa kwa visasi. Cha kujifunza ni kuwa si kila unayemtendea baya anaweza kukulipizia, ila je ile jamii iliyomzunguka imeridhika na lile baya ulilolifanya? Cha muhimu ni kujitahidi kutenda mambo katika mlolongo mzuri kwani tunaweza kukosea leo ila baada ya miaka kadhaa tukawatesa tunaowapenda kama ambavyo makosa ya Ibra yalivyomtesa Sophia”
Familia ya Sophia ilishangaa sana kwani hawakuweza kufikiria kama kuna kitu kama hiko kuwa Ibra amewahi kukataa mimba kwani Ibra alionekana ni kijana mstaarabu, mkweli na muwazi sasa iliwashangaza sana hii habari na kujiuliza kuwa Ibra aliwezaje kuyaficha yote hayo kwa mke wake, mama Sophia alimuangalia Ibra na kusikitika sana kisha akamwambia,
“Ibra unakumbuka wakati umekuja kumchumbia binti yangu? Nilikuuliza kabisa, je umewahi kuwa na mke? Ukakataa, nikakuuliza, umewahi kumpa mwanamke mimba au una mtoto? Napo ukakataa kumbe kuna mambo nyuma ya pazia mmh!”
Mama Sophia aliinama huku akisikitika ila huyu bibi akamwambia,
“Usisikitike sana, cha muhimu ni kushukuru uzima tu”
Kisha akaendelea kuzungumza nao,
“Kuna mambo ya mihimu sana kuyafanya ili muweze kuishi kwa amani sasa”
Ila kabla bibi hajaongelea hayo mambo, Sophia aliamua kumuuliza kuwa ilikuwaje hadi mumewe kuangukia kuinunua hiyo nyumba wakati kuna matatizo hayo,
“Kwanza kabisa mnatakiwa mjifunze kitu, ukiona kitu kinauzwa tofauti na thamani yake unatakiwa kukiwekea mashaka, angalia ile nyumba na pesa ambayo Ibra alinunulia yani haifikii hata robo ya thamani ya ile nyumba. Swali la kwanza ni kujiuliza kuwa imekuwaje mwenye mali akaiuza kwa bei ya hasara kiasi hiko? Kitu pekee kilichopelekea yule mwenye nyumba kuuza kwa bei hiyo ya hasara ni kutokana na mauzauza yaliyompata kwenye nyumba ile. Akashindwa kuvumilia na kuamua kuiuza huku akiamini kwamba huenda atakayenunua atakuwa salama kwani vile vitu vibaya vya kwenye ile nyumba havifahamu. Sema kwa bahati mbaya sasa, aliyeweza kuingia mkenge na kununua ile nyumba alikuwa ni mbaya wao, ila mwenye ile nyumba alijitahidi kwa kila hali kuhakikisha kwamba ile nyumba inakuwa salama kwa mnunuzi wake.”
“Sasa kwetu haikuwa salama kutokana na makosa ya Ibra au?”
“Ni kweli Ibra ndio chanzo ila wote mmechangia, na ubaya mkubwa mlioufanya ni kuweza kumkaribisha yule kiumbe ndani kwenu. Majini yanapenda sana kukaribishwa, na unapoyakaribisha yanakuwa huru zaidi na kufanya chochote wanachohitaji kufanya tofauti na usipomkaribisha. Kwahiyo kitendo chenu cha kumkaribisha kilimpa mwanya zaidi wa kuwasumbua na kuwafanya anavyotaka. Mfano kule kwenu pia wakati anagonga mngejaribu kumkaribisha tu basi kwa hakika hata msingeweza kuonana na mimi kwasasa kwani ameshakuwa na hasira zaidi na nyie na angemaliza wote mule ndani kwenu tena ingekuwa rahisi zaidi kwavile mmemkaribisha. Katika maisha tunatakiwa kuwa makini katika maamuzi yote tunayoyafanya na tuangalie je yanaweza kutudhuru kwa kiasi gani.”
Walikuwa kimya kabisa, kisha Sophia akauliza tena,
“Wakati tunakuja huku niling’atwa na nyoka je ilikuwa ni maana gani?”
“Hakuhitaji muonane na mimi, alikuwa anafanya kila njia kuwazuia na yule wala hakuwa nyoka bali ulikuwa ni upepo wa kuwashtua tu. Ila lile gari lililokuja kuwachukua ili muende nalo hospitali ndio lingewapeleka na maji”
Wakabaki wanashangaa kwani karibia wote hawakuwa na ufahamu wa kutosha juu ya mambo haya, yalikuwa ni mageni kabisa kwenye masikio yao na mawazo yao.
Sasa bibi akaanza kuwaeleza mambo muhimu ya kufanya kwa wakati huo kwaajili ya kuwasaidia kutokana na jambo hilo,
“Tatizo kubwa ni moja tu, yule kiumbe ana nguvu na ni kiumbe wa visasi yani hapa tunatakiwa kuwa makini sana kuhakikisha tunamshinda kabisa na ikiwezekana apotee kabisa mbele yetu.”
“Sawa bibi, sisi tunakusikiliza ili utuambie cha kufanya”
“Kwanza kabisa Sophia, nakuomba uchukue viatu vyako ulivyoviacha hapo nje ndio tuendelee na mambo mengine”
Sophia akainuka na kutoka nje, akainama na kuchukua viatu vyake ila wakati anataka kuinua kichwa sasa ili aingie ndani akaona miguu ya mtu amesimama mbele yake, na alipomtazama alikuwa ni Neema, kwakweli Sophia alipiga kelele sana.
Itaendelea kama kawaida…….!!!!!
Toa maoni yako mdau.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment