Tuesday, 25 April 2017

NYUMBA YA MAAJABU: 48


Kisha Sophia akaanza kusonga mbele kurudi kwao, ni kweli akasikia sauti nyingi zikimuita kwa nguvu ila Sophia hakugeuka nyuma kabisa hadi alipofika nyumbani kwao.
Alishangaa pale kwao kukiwa kuna watu wengi sana, na sauti zilisikika wakilia na kuomboleza huku wakitaja jina lake.
Sophia alisita kusogea kwa muda huku akitafakari kuwa pale kwao kwanini watu walijaa na kwanini walikuwa wakilia huku wakitaja jina lake, akawa amesimama kwanza akisikilizia mara akasikia sauti ikimuita kwa nguvu sana ila akakumbuka maneno ya yule mtu kuwa asigeuke nyuma hadi atakapoingia ndani kwao kwahiyo akajipa ujasiri wa kutokugeuka. Wakati amesimama hapo, akahisi kuna mtu amemshika bega kanakwamba ageuke ili amtazame ila Sophia alijivika ujasiri wa hali ya juu na kuendelea kutembea mbele bila hata ya kugeuka, huyu mtu alisikika akimwambia Sophia,
“Jamani Sophia wewe, hata kugeuka kidogo jamani. Hivi unajua ni kitambo sana hatujaonana!”
Ile sauti ilikuwa ni sauti ya rafiki kipenzi wa Sophia ila bado alijipa ujasiri wa kutokugeuka kabisa.
Akafika mlangoni sasa na kuingia ndani huku akiwa amewapita watu wote pale nje bila ya kugeuka wala nini, alimuona mama yake akiwa amelala hini akilia, akamuona mdogo wake akionekana kuomboleza sana. Sophia akaita,
“Mama”
Sauti hii ilimshtua kila mtu aliyekuwepo eneo lile, na gafla watu wakaanza kupiga kelele huku wakikimbia hovyo hovyo ila Sophia alisimama eneo lile lile akiwaangalia tu.
Kisha akaamua kusogea alipo mama yake ambaye alikuwa akitetemeka tu, Sophia akamuita tena mama yake;
“Mama”
Mama aliinama kwa muda kisha akainua macho yake na kumuuliza mwanae,
“Ni wewe kweli mwanangu au naota? Siwezi kukimbia, sina nguvu mimi. Kama ni mwanangu kweli basi namshukuru Mungu kwa hilo”
“Ni mimi mama, mimi ni mwanao Sophia”
Mama Sophy akamgusa mwanae, kisha akamkumbatia huku machozi yakimtoka, huyu mama alilia sana na alilia kwa muda mrefu na kumfanya Sophia nae alie huku akimbembeleza mama yake.

Baada ya muda wakatulia sasa, mama Sophy alimshika tena mwanae na kumuuliza,
“Nini kimekupata mwanangu?”
“Ni historia ndefu sana mama, ila mbona watu wote hapa wamekimbia kwanini?”
Huyu mama akapumua kidogo na kuanza  kumueleza Sophia,
“Mwanangu, hapa tupo kwenye msiba wako na leo ilikuwa ni siku yako ya mazishi yani hapa. Ndiomana kila mtu amekimbia, hata mimi bado siamini kama ni wewe najihisi kamavile nipo ndotoni”
“Sasa mama, mnanizikaje bila maiti yangu?”
Huyu mama akashtuka sana, kisha akamuangalia tena mwanae
“Sophy mwanangu umekufa, na maiti yako ipo hospitali yani hivi ninavyoongea kuna nduguzo wameenda kuichukua ili tuje kuzika. Hapa watu wote walikuwa wakingoja maiti yako ili tukazike”
Sophia akapumua kidogo kwani alishindwa kuelewa moja kwa moja kuwa tayari hata kufa alishakufa, machozi yakamtoka na kumwambia mama yake
“Lakini mama, mimi ni mzima kabisa sijafa mimi”
“Mwanangu, mimi ni mama yako na ninaamini kuwa umerudi tena mwanangu na nimefurahi sana lakini najua kwa wengine itawachukua mud asana kuamini hilo”
Mama Sophy akamkumbatia tena mwanae.
Mara gafla wakasikia sauti kutoka nje,
“Kheee imekuwaje hapa, mbona watu wote hawapo?”
“Sijui jamani, maana nahisi kuchanganyikiwa kabisa. Jana nilihakikisha kwa macho yangu maiti ya Sophy kisha ikarudishwa tena monchwari eti leo haipo kwakweli haiwezekani jamani”
Sasa wakawa wanazungumza hivyo huku wakiingia ndani na kukutana macho kwa macho na Sophia, kwakweli hakuna aliyeweza kustahimili kwani wote walikimbia na hawakugeuka hata nyuma kwahiyo bado Sophia alibaki pale na mama yake huku Sophia akijaribu kumdadisi mama yake kuhusu hiko kifo chake kuwa ilisemekana aliumwa na kitu gani hadi kufa.
“Tuliambiwa ajali mwanangu, yani kwenye hiyo ajali umekutwa mwili wako tu. Inasemekana ulikuwa na mume wako ila nasikia alikimbia baada ya kuzinduka. Tena tumeambiwa wiki imepita na ulipelekwa hospitali wakitafutwa ndugu zako na tulipopatikana wakaenda dada zako kuhakikisha na kweli wanasema walikukuta ni wewe”
Sophia aliishia kushangaa sana kwani hakumbuki kama na mumewe walipata ajali ila anachokumbuka ni kuwa walikutwa pale chini kisha yeye kuchukuliwa na wale watu waliojifanya kuwa ni wasamalia wema wanataka kumsaidia.

Kimya kikatanda kisha mtu mmoja mmoja akaanza kurejea pale nyumbani kwakina Sophia huku wakiogopa kumsogelea Sophia mpaka pale mama Sophy alipokuwa akiwahakikishia kuwa yule ni Sophia tena ni mzima kabisa, walifurahi kusikia vile kuwa Sophy ni mzima kabisa ila bado walishikwa na uoga juu ya uzima wa Sophia.
Mwishowe karibia familia nzima iliwasili pale nyumbani huku wakijaribu kuzungumza mawili matatu na Sophy waweze kuhakikisha kuwa ni yeye ila mama Sophy alimuhurumia mwanae kwani alionekana kuchoka sana hivyo akamtaka mwanae apumzike, Sophia aliamua kwenda kuoga kwanza kisha wakampa chakula na kwenda kupumzika ambapo mama yake alienda na kulala pembeni ya mtoto wake.
Familia ya Sophy bado hawakuelewa kuwa ni nini kilichotokea mpaka imekuwa hivyo ukizingatia kuna ndugu zake kabisa waliohakikisha maiti ya Sophy na kugundua kuwa ni kweli amekufa. Kitendo cha wao kwenda na kuikosa kiliwashangaza sana na kuhisi kama wanafanyiwa mchezo hospitali ila kitendo cha kumkuta Sophia nyumbani ndio kilichowashangaza zaidi.
Kwa upande wa Sophia hakuweza kulala wala nini kwani picha ya matukio katika maisha yake ilikuwa ikimjia kichwani mara kwa mara haswaaa tukio lake la kutolewa kizazi, yani lilikuwa likijirudia kama sinema vile ila ndio jambo halisi lililomtokea katika maisha yake ingawa kila alipolifikiria mwili wake wote ulisisimka na ndipo alipowaza pia kuhusu Ibra ila hakupata jibu kuwa mumewe huyo yupo mahali gani. Kwakweli Sophia hakuweza kulala kabisa, kwani alikuwa akilala kidogo na kushtuka, bado alikuwa na uoga na nyumba aliyokuwa akiishi.
Kuna muda usingizi ukampitia na akaona kitu kwenye ndoto, alimuona yule mtu aliyemsaidia akimwambia,
“Kuna umuhimu wa wewe kwenda kukutana tena na yule bibi aliyekupa dawa za kurudisha akili yenu, nenda ukaonane nae na kwa hakika utatambua mengi sana na pia atakusaidia kwani hapa sio mweisho wa wewe kufatiliwa. Ilimradi uliingia kwenye ile nyumba basi utafatiliwa siku zote, kwahiyo kwa ushauri wangu jitahidi ukaonane na yule bibi kwanza kabla mambo hayajawavurugikia hapo kwenu pia”
Sophia alionyesha kuelewa vizuri sana na alipoamka sasa hivi kulikuwa kumekucha kabisa.
Sophia akamuamsha mama yake, ambaye alimka na kutoka nae nje ambapo bado kulikuwa na hali kama ya matanga vile kwa uoga ambao walikuwa nao.

Muda huu wa asubuhi walikuja wazee wa eneo lile na kuwataka wafanye tambiko juu ya Sophia kwani ni jambo la ajabu sana lililotokea,
“Ilitakiwa tambiko hili lifanyike jana ila kwavile kila mtu alishikwa na mshtuko basi hatunabudi kulifanya leo. Tulijua Sophia amekufa na tukachimba kaburi kwaajili ya kumzika ila kwavile imetokea yupo hai basi hatunabudi kufanya tambiko na kwenda kufukia lile kaburi ili tuondoe huu uchuro.”
“Sawa, sisi kama familia tumeafikiana na hilo. Kwahiyo tutafanya tambiko gani?”
“Tutachinja mbuzi, kisha mbuzi huyo tutaenda kumzika kwenye lile kaburi kwa niaba ya Sophia”
Wakakubaliana juu ya hilo kisha ndugu wa Sophia wakajitoa kwenda kutafuta huyo mbuzi wa kumfanyia kafara na walipompata walikuja nae ambapo yalifanyika matambiko kisha yule mbuzi akachinjwa halafu wote kwa pamoja wakaanza safari ya kuelekea makaburini kwa lengo la kumzika mbuzi huyo katika kaburi ambalo lilichimbwa mahususi kwa lengo la kumzika Sophia. Nyumbani walimuacha Sophia, mama yake na baadhi ya ndugu zake ila wengine wote walielekea makaburini kwa lengo la kumalizia hiyo kafara.
Cha kushangaza walipofika pale makaburini walikuta lile kaburi walilolichimba kwa lengo la kumzika Sophia likiwa tayari limeshafukiwa kanakwamba kuna mtu mwingine amezikw hapo,
“Imekuwaje jamani? Au sio hapa?”
“Ndio hapa hapa, na tuliochimba ni sisi wenyewe”
“Au pengine kuna watu walijiongeza na kuja kufukia?”
“Inawezekana ikawa hivyo”
“Sasa tutafanyaje na huyu mbuzi?”
Mmoja akatoa wazo kuwa wachimbe pembeni yake na wazike huyo mbuzi kwani lengo lao ilikuwa ni kumzika na si vinginevyo, hivyobasi wakaamua wafanye hivyo na kuchumba pembeni kidogo ya lile kaburi na kumzika yule mbuzi kisha wakaondoka na kurudi nyumbani.
Walirudi moja kwa moja na kuwataarifu yaliyotukia huko makaburini kisha wakaondoka zao na kuwaacha ndugu tu pale.

Sasa  waliamua kuweka kikao cha familia ambapo walielezana kwa urefu kuhusu kule makaburini,
“Nadhani vijana wa hapa waliamua kujiongeza baada ya kuona mambo yale wakaamua kwenda kufukia lile shimo”
Sophia alikuwa kimya tu kwani mashaka yake ilikuwa ni huenda Neema ndiye amefanya yote hayo na wala sio vijana wa mtaa huo, wakati wanafamilia wanajadili Sophia hakuchangia mada yoyote ile ikabidi wamuulize kutokana na ule ukimya wake,
“Sophia”
Kwanza akashtuka kwa kuitwa na kusikilizia wamemuitia nini,
“Wewe unashauri kitu gani kuhusu hili?”
“Nashauri mnipeleke huko makaburini nikaone hilo kaburi mlilonichimbia”
Wote wakamuangalia kwa makini kisha wakamuuliza tena,
“Hivi unajua tunazungumzia kitu gani?”
“Kwani mnazungumzia nini?”
Ni wazi kuwa Sophia hakuwa eneo hilo kimawazo kabisa ndiomana alijikuta akiongelea kitu cha mwanzo kabisa ambacho alisikia wakiongea,
“Pole sana, inaonyesha mawazo yako hayapo hapa kabisa, usijali huko makaburini tutakupeleka kesho nawe pia utaenda kuona. Ila hapa tulikuwa tukijadili jambo la kifamilia haswaa kuhusu mumeo, tulihitaji kujua ni wapi pa kuanza kumtafuta ndio tukakuuliza maoni yako”
“Sawa nimewaelewa, kwakweli akili yangu haipo sawa kabisa. Chochote mtakachoamua ni sawa tu kwangu”
Ikabidi wamuache kwanza kwani ni wazi akili ya Sophia haikuwa sawa na wala alikuwa hawaelewi kwa chochote ambacho walikuwa wakizungumzia.
Kuna muda alikaa mwenyewe na kutafakari akaona kuna umuhimu mkubwa sana way eye kwenda kwa yule bibi tena akahisi kuwa inawezekana itakuwa rahisi kumpata hata huyo mumewe ingawa moyo wake haukuwa na imani na Ibra tena kutokana na yote yaliyompata. Akajipa moyo tu kuwa atapatikana lakini hakuwa na imani ya kuendelea kuishi nae kwa maisha yake yatakayokuwa baada ya mambo yote haya. Mama Sophia alimfata mwanae na kujaribu kuzungumza nae ili kujua ni kipi haswaaa kilichompata mtoto wake,
“Mama weee acha tu, yani hapa nilipo mwanao sina kizazi tena”
“Huna kizazi kivipi Sophy?”
Sophia aliinama na kuanza kulia kisha akamwambia mama yake,
“Kizazi change kimetolewa mama”
Mama Sophy alimsogelea mwanae na kumkumbatia ingawa hakuelewa kisa na mkasa hadi mwanae kufikia hatua ya kutolewa kizazi.
“Jamani mwanangu imekuwaje tena? Kwanini utolewe kizazi?”
“Sijui mama yani sijui kabisa lakini ndio hivyo nimetolewa kizazi mama. Sitaweza kuzaa mimi, sitaweza kuwa na mtoto kamwe, hakuna mwanangu atakayekuita bibi mama yangu sina kizazi mimi”
Kwakweli mama Sophia alishikwa na uchungu wa hali ya juu kwa kauli hizi za mwanae hata yeye alijikuta akilia kwa uchungu huku akimbembeleza mwanae.
“Nyamaza mwanangu, kutokuwa na kizazi sio mwisho wa maisha. Tunachomshukuru Mungu kwasasa ni kukuona wewe ukiwa mzima mwanangu. Usilie Sophy wangu”
“Inaniuma sana mama, nilitamani watoto mimi. Nilitamani apatikane mtu wa kuniita mama, kunitania, kunichekea, kulia nimbembeleze lakini hayupo mtu huyo na hatokuwepo kamwe. Nimeishia kuwaona wanangu kwenye ndoto tu wakinipungia mkono na kuniaga kwa sura za simanzi. Oooh wanangu mimi, hawataweza tena kukaa kwenye tumbo langu maana sina kizazi”
Mama Sophy alipata kazi kubwa sana ya kumbembeleza mwanae na kuhakikisha kuwa anarudi kwenye hali yake ya kawaida, hadi pale alipokuwa sawa akamuomba mwanae kuwa waende kupumzika ili kuyaacha yale mawazo mabaya yawapitie mbali.

Kesho yake kama ambavyo Sophia alivyowaomba ndugu zake kuwa wampeleke mahali ambako walichimba kaburi lake wakaamua kufanya hivyo ambapo walijiandaa pamoja nae kisha kwenda nae huko makaburini, Cha kushangaza walipofika pale waliona yule mbuzi amefukuliwa na kuwekwa juu ya kaburi ambalo walipanga kumzika Sophia halafu mbele ya lile kaburi kulikuwa na kibao kilichoandikwa kwa herufi kubwa ‘MAREHEMU NEEMA’ kwakweli walistaajabu sana ila Sophia hakuweza hata kutafakari mara mbili na kuanza kukimbia ikabidi ndugu zake wamkimbilie na kumshika kisha kuanza kurudi nae nyumbani.
Walifika wakiwa wanahema sana, hata watu ambao hawakwenda eneo hilo walishangaa na kuwauliza kuwa ni kitu gani kimetokea huko ikabidi wawasimulie kitu walichokikuta.
“Mbona ni maajabu hayo?”
“Tena maajabu makubwa, hata sikuyafikiria mambo haya jamani. Hivi ile inamaanisha nini?”
“Inabidi twende tukawaeleze wazee tu”
Kwavile ilikuwa ni jioni na giza nalo lilikalibia kuingia, Sophia akawakataza kwenda kuwatafuta hao wazee kwa muda huo na kwenda kuwaambia.
“Tafadhalini sana ndugu zangu, wale wazee nendeni mkawaeleze kesho mapema na sio sasa”
“Kwanini Sophia wakati huu ndio muda mzuri ili wajue kabisa”
“Hata kama huu ni muda mzuri, watahitaji kwenda kushuhudia na sidhani kama ni muda mzuri wa kwenda huko makaburini”
Hawa ndugu waliamua tu kukubaliana na Sophia kisha kuendelea na mambo mengine ya hapa na pale.
Siku hiyo hiyo kwenye mida ya usiku saa sita wakasikia mtu nje ya nyumba yao akisugua masufuria na kufanya washtuke sana na kuamshana,
“Jamani mmesikia huko nje kuna mtu anasugua masufuria?”
“Hata mimi nimesikia”
“Je huenda ni nani?”
“Nadhani tujipange tutoke nje tukamshuhudie ni nani”
Sophia uoga ukamshika na kufanya awazuie ndugu zake kutoka nje,
“Tafadhali msitoke nawaomba sana”
“Kwani unajua ni nani?”
“Sijui, ila nawaomba msitoke nje”
Mdogo wa Sophia aitwaye Tausi akaamua kufunua pazia la dirishani ili achungulie ni nani, ila alipofunua tu alipiga kelele za uoga na kuanguka chini.

Itaendelea kama kawaida……!!!!!
Toa maoni yako mdau.

No comments:

Post a Comment