Yani siwema alikimbia kama chizi na hakuangalia nyuma tena.
Ibra nae akajaribu kuinuka na kumkongoja mkewe ili waweze kutoka ila walishtukia kama mtu akiwasukuma na kuwakalisha chini.
Kisha akaona Sophia akisukumwa zaidi na kulazwa kwenye kochi ila aliyekuwa akifanya hivyo hakuonekana kabisa, Sophia akaonekana akijinyonga nyonga tumbo huku pale chini damu zikitapakaa.
Ibra alimuhurumia sana mkewe ila hakuwa na la kufanya kwani hata ule uwezo wa kuinuka eneo lile hakuweza, Sophia alizidi kuugulia pale chini na baada ya muda alikuwa kimya kabisa hata kuendelea kuugulia hakuweza na ilionyesha wazi kuwa amezimia. Ibra nae akajaribu tena kuinuka na kujikuta akiweza kuinuka, kisha akasogea alipo mkewe na kumbeba kwa lengo la kumpeleka hospitali huku akijiuliza kuwa atampeleka kwa usafiri gani ila akajipa moyo kuwa ataomba msaada kwa watu nje ili wamsaidie na akaamini kuwa ni lazima atapata msaada.
Wakati anatoka nje na mke wake, akashangaa kuona gari yao ikiwa pale nje hivyo Ibra hakutaka kufikiria mara mbili kwani alifungua ile gari na kumuingiza mkewe hata hakujiuliza kuwa ile gari ililetwa na nani pale nyumbani na kwanini funguo zake zilikuwa zikining’inia muda wote kwenye mlango. Akaanza kuendesha huku akimuwaisha mkewe hospitali.
Kwa bahati akaona jingo la hospitali, ingawa ile hospitali ilikuwa ngeni kabisa machoni pake ila aliingia na gari yake kwani nia yake ni kumuwaisha mkewe kwa lengo la kupata huduma ya haraka.
Alisimamisha gari na kumshusha mke wake ambapo kuna nesi alimpokea na kumpeleka Sophia moja kwa moja kwa daktari kisha Ibra akaachwa nje na kuambiwa kuwa asubiri, Ibra akamuuliza huyu nesi
“Kwani sitakiwi kwenda kutoa maelezo ya chanzo cha ugonjwa maana mimi ni mume wa mgonjwa na mgonjwa huyu hawezi kuzungumza”
“Hata usijali juu ya hilo, kama daktari angehitaji maelezo yako basi angekuita ila kwavile hajakuita jua kwamba maelezo yako hayana umuhimu kwake”
“Samahani dada, hivi hii hospitali ni mpya eeeh maana sikuwahi kuiona hapo kabla”
“Hii hospitali ni mpya ndio na imefunguliwa mahususi kwa matatizo ya mkeo”
Kisha huyu nesi akaondoka na kumuacha Ibra akiwa na mawazo kuwa hospitali imefunguliwa mahususi kwa matatizo ya mkewe kivipi ila hakupata jibu, na pia alitamani sana kujua hali ya mkewe huko kwa daktari ila hakuwa na namna yoyote zaidi ya kusubiri majibu atakayoletewa na huyo daktari.
Ibra alikaa pale mapokezi na kujikuta akipitiwa na usingizi wa hali ya juu hata hakuweza kushtuka kwa muda huo, usingizi huo ulimpeleka mbali sana na akajikuta akiyaona maisha ya zamani aliyokuwa akiishi na mkewe na jinsi yalivyokuwa na amani yani ni tofauti kabisa na maisha waliyokuwa wakiishi kwasasa.
Sophia alipokuwa kule kwa daktari, muda huu akazinduka na kushtuka sana kwa sura ya daktari aliyoonana nayo. Daktari huyu alikuwa ni Neema na alikuwa akitabasamu tu, Sophia alianza kulia huku akimuomba Neema kuwa amuhurumie,
“Nihurumie Neema, naomba nihurumie usinitende vibaya. Kwanini uniumize hivi ilihali sijawahi kukufanyia jambo lolote baya jamani!”
Neema alikazana kucheka tu kisha akamwambia,
“Hiyo nihurumie yako haitasaidia chochote kwani nishakufanyia kitu kibaya sana”
“Kitu gani?”
“Nimekutoa kizazi”
Kwakweli Sophia alihisi kama kuchanganyikiwa aliposikia ile kauli kuwa ametolewa kizazi na kujikuta akilia zaidi,
“Jamani Neema jamani, mmekula watoto wangu ila ukaona hiyo haitoshi hadi kunitoa kizazi jamani. Kwani nimekukosea nini mimi? Niambie Neema, ni kitu gani nimekosea jamani, mbona nahukumiwa bila kosa?”
“Kumbe kosa lako hulijui?”
“Sijui kosa langu, niambie Neema”
“Kosa lako ni kukubali kuishi kwenye ile nyumba, na pia kosa la mumeo ni kununua ile nyumba”
“Kwanini jamani mnifanyie hivi, nyumba imenunuliwa mimi nakataaje kuishi? Kwani ile nyumba ina uhusiano gani na wewe? Umenitoa kizazi Neema, furaha yangu yote ya kuwa na watoto umeipoteza”
Sophia alikuwa akiongea huku akilia kwa uchungu sana kwani uonevu huu aliofanyiwa hakuwahi kuufikiria katika maisha yake ila Neema alikuwa akicheka tu na kufanya Sophia aulize tena,
“Ni nani kanileta huku mimi?”
“Ni mumeo ndio kakuleta ili nikusafishe sehemu nilipokutoa kizazi”
“Jamani, kwanini Ibra ananifanyia hivi? Je mnajuana na Ibra? Kwani mimi kosa langu kubwa ni nini jamani?”
“Ibra najuana nae sana tu ila hajui kama najuana nae, Ibra usimuone vile aliwahi kumfanyia vibaya sana mdogo wangu na ndiomana nilifurahi sana kumuona ananunua nyumba ambayo ni himaya yangu ila wewe kiherehere chako cha kuhamia pale ndio kimekuponza”
“Ibra alifanya unyama gani sasa?”
Sophia alikuwa akilia huku akimsikiliza huyu Neema kwani kwasasa uoga wote ulimuisha na hatakama angeendelea kuwa na uoga basi Isingesaidia chochote kwani Neema alishatawala nusu ya mawazo yake.
Neema akamuangalia Sophia kisha akamwambia,
“Sitakuelezea kwa maneno ila ngoja nikuonyeshe ili usifikirie namsingizia mume wako, na kama mkipata muda wa kuongea muulize atakujibu kuhusu hizi tuhuma zangu”
Sophia alitulia tu, kisha Neema akanyoosha mkono wake ambapo ilikuwa kamavile Sophia anaangalia sinema.
Alimuona Ibra akiwa amekaa mahali na binti mmoja, yule binti alisikika akimwambia Ibra
“Ibra jamani, tulikuwa wote halafu leo hii unaikana hii mimba yangu?”
“Hivi Nancy kwa haraka haraka unataka nikwambie nini? Maisha yangu unayajua, kula kwa shida kulala kwa shida, hiyo mimba siitambui na siko tayari kuitwa baba kwasasa”
“Najua kwanini unanikataa, ni kwasababu ya yule mwanamke uliyemposa”
“Yule mwanamke nampenda na hata familia yangu inampenda pia na amekubali kuishi na mimi kwa hali yoyote ile halafu gafla aibuke mtu ana mimba unafikiri atakubali? Hiyo mimba siitambui”
“Inamaana mimi ulikuwa hunipendi eeeh!”
“Sikia Nancy nilikuwa nakupenda vizuri ila unajua wazi ni kwanini mimi na wewe hatuwezi kuishi pamoja wala kuoana. Kwahiyo sahau kuhusu mimi. Kwanza familia yenu kwa maelezo yako tu inaonyesha wazi nyie ni Malaya, dada zako wote hawajaolewa na hakuna mwanaume anayeweza kuwaoa nyie, yani sahau kuhusu mimi kabisa”
“Na hii mimba je?”
“Nimekwambia siitambui, hivi kwanini hutaki kunielewa? Kwanza haiwezekani ikawa mimba yangu, na wala haitakuwa ajabu wewe kuzalia nyumbani maana kwenu wote wamezalia nyumbani na ambao hawajazaa nadhani hawana vizazi hivyo achana na mimi kabisa, niache na maisha yangu, niache niishi kwa amani na mwanamke wa maisha yangu, mwanamke ninayempenda na anayependwa na familia yangu, mwanamke ambaye naendana nae na ninaweza kuishi nae na kufunga nae ndoa”
Huyu binti alionekana akiinama na kuanza kulia, Ibra akainuka ili kuondoka na kutaka kumuacha yule binti kwenye lile eneo, ambapo huyu binti aliinuka na kumfata Ibra kwa nyuma ila Ibra alipogundua anafatwa akageuka na kumsukuma yule binti ambapo alimuacha akiwa ameanguka chini na kuondoka. Ila huyu binti alisikika akisema neno moja tu,
“Ibra asante”
Ile picha ikapotea kisha Neema akamuangalia Sophia na kumwambia,
“Mdogo wangu alirudi nyumbani akiwa analia sana na kwakweli nilimuonea huruma iliyopitiliza, kumbe mdogo wangu akapanga kutoa ile mimba na kwenda kunywa vidonge vilivyopelekea kupatwa na umauti. Niliapa kulipa kisasi kwa Ibra ila kwa bahati mbaya na mimi nikaja kupatwa na majanga yaliyopelekea niwe nilivyokuwa sasa”
“Majanga gani?”
“Hiyo sio kazi yako kujua, ila tambua kwamba kitendo change cha kukutoa kizazi wala sijakuonea yani ni saizi yako kabisa”
Sophia alikuwa kimya akilia muda huu kwani bado hakuona kama alistahili kubeba lawama za mume wake, yani makosa yaliyofanywa na mumewe kipindi cha nyuma huko haikupaswa alipiziwe yeye, alilia sana huku akimuomba Neema aweze kumuachia sasa aondoke.
“Nakuruhusu ondoka ila nenda kauamshe mzoga wako pale nje maana ule mzoga wako hautumii akili hata kidogo nab ado nitawaendesha sana hadi pale akili zenu zitakapowakaa sawa”
Sophia akajitahidi kujaribu kusimama na akaweza kisha akaanza kujikongoja ili aweze kutoka pale nje, alishangaa kuona ile hospitali haikuwa na mtu mwingine yeyote zaidi ya Neema na kujiuliza kuwa kwanini Ibra aliamua kumleta hapo.
Alimkuta Ibra akiwa kalala hajitambui kabisa, akajaribu kumuamsha naye Ibra akaamka na kumuangalia mkewe,
“Sophia! Umepona, unaendeleaje mke wangu?”
“Naomba tuondoke mahali hapa Ibra”
“Unaendeleaje? Je tushalipia bili?”
“Naomba tuondoke Ibra”
Basi Ibra akaamua amsikilize mkewe na kuanza kumkongoja hadi kwenye gari lao ili wapande,
“Hivi wewe Ibra hiyo akili yako itarudi lini? Nilikwambiaje kuhusu hili gari, kwanini bado waling’ang’ania kila leo kuwa tuwe tunalipanda? Na nani aliyekutuma kunileta hapa? Hiyo gari sipandi, haya tuondoke”
“Sasa tutaondoka na usafiri gani Sophia?”
“Wowote ila hilo gari sipandi”
“Kwahiyo niliache hapa?”
“Unataka ulipeleke wapi sasa ikiwa gari lenyewe huwa linakufata ulipo”
Sophia alikuwa akiongea hayo huku akijikongoja mwenyewe ili atoke kwenye eneo lile ikambidi Ibra afatane tu na mke wake na kukongojana hadi kutoka, walipofika nje kabisa ya eneo lile
“Haya sasa tunaendaje nyumbani?”
“Tutafute usafiri wowote tu, na tena sitaki unirudishe kule nyumbani. Nataka unipeleke nyumbani kwetu”
“Sophia, Sophia jamani unajua fika kwenu kulivyo mbali halafu twende bila usafiri hivi tutafikaje ilihali gari tumeliacha ndani ya hospitali? Ngoja nikalichukue bhana”
Ibra akageuka nyuma ili akachukue gari yao ila alishtuka sana kwa alichokiona kwanoi hakuona tena lile jingo kubwa la hospitali na badala yake akaona makaburi na kumfanya amkumbatie mkewe kwa nguvu sana,
“Angalia Sophia”
“Nini tena?”
“Weee angalia”
Sophia nae akageuka kuangalia akashangaa pia kuona makaburi kisha akasema,
“Nilijua tu, Neema si mtu mzuri. Upumbavu wako Ibra ndio unaonitesa sasa”
Ibra hakutaka kuulizana chochote hapo na mke wake hivyo akaamua kumkongoja na kuanza kutoka kwenye eneo lile, alikongojana nae hadi barabarani na walipofika walikaa chini kwa muda ila Sophia bado alikuwa na kinyongo sana na aliendelea na msimamo wake ule ule kuwa usafiri ukipatikana basi apelekwe moja kwa moja nyumbani kwao
“Kwanini tusirudi nyumbani kwetu tu Sophia?”
“Ibra tafadhali, yaliyonipata yananitosha sana tu tena hayakustahili kunipata, sitaki makubwa zaidi naomba nirudishe kwetu”
“Kwani ni mambo gani yamekupata?”
“Hivi unajua kuwa mimi sina kizazi tena!”
Huna kizazi! Kivipi?
“Neema amenitoa kizazi na yote ni kwasababu yako”
“Kwasababu yangu! Kivipi?”
“Unamfahamu Nancy?”
“Nancy? Ndio nani huyo?”
“Mwanamke uliyekuwa nae kabla ya kuniposa mimi”
“Kheee yule Malaya, nani kakudanganya kuwa nilikuwa nae?”
“Basi kwa taarifa yako, yule Neema ni dada yake na huyo Nancy”
Ibra akashangaa na kumuuliza mkewe,
“Sasa undugu wa Neema na Nancy unahusiana vipi katika maisha yetu?”
“Wewe si ulikataa mimba ya Nancy?”
“Haikuwa mimba yangu ile”
“Ila si ulitembea nae?”
“Sophy tafadhali tuachane na hizo habari, hayo mambo yalishapita kitambo sana”
“Yalipita wakati ndio umenisababishia matatizo yote haya, yani mimi sitaweza kuzaa tena kwasababu yako na ufirauni wako”
“Sophy, wewe ni mke wangu, habari za hivyo si nzuri zitaharibu ndoa yetu”
“Ziharibu mara ngapi? Ibra, nirudishe nyumbani tu akili yangu ikawe sawa kwanza”
Kwavile Ibra alishamuona mkewe kapaniki akaamua kutafuta usafiri ili waweze kuondoka kwenye eneo hilo kwani alihisi ndio kunakomfanya mkewe apaniki zaidi huku akijiuliza kuwa ni nani kampa habari zisizoeleweka mke wake.
Ibra akasimama ili aangalie usafiri, mara akaiona gari ya kukodi na kuisimamisha kisha akamuomba mke wake waweze kwenda kupanda gari lile,
“Hapana Ibra siwezi kupanda hilo gari sina imani nalo”
“Sophy, Sophy tafadhari usinichanganye. Umeniletea mada za ajabu hapa halafu natafuta usafiri tupande unaleta mada zingine, sitaki ujinga”
Ibra akamuinua mkewe kwa nguvu na kumpakia kwenye lile gari, ila baada ya kupanda tu wote wakashangaa kwani yule dereva wa mwanzo alikuwa mwanaume na mara hiyo hiyo akawa mwanamke. Wakati wakishangaa mara lile gari liligeuka na kuwa jeneza.
Itaendelea kama kawaida……!!!!!!
Toa maoni yako mdau.
No comments:
Post a Comment