Monday, 23 January 2017
PATA ELIMU JUU YA UVIVU NA UWEZE KUEPUKANA NAO
Uvivu ni tabia ya kutokufanya kazi au kutokupenda kufanya kazi.Kutokupenda kujishughulisha au kutokujishughulisha na kazi yeyote ile iwe ya kukuendeleza wewe mwenyewe na wale wanaokuzunguka.
Mtu mvivu hupenda kulala na huthamini usingizi kuliko kujituma. Mvivu anaependa usingizi, njaa kwake haikosi maana hutumia muda mwingi kulala kuliko kutafuta chakula kwa ajili yake na watu wake.
Mithali 19:15 ‘’Uvivu humtia mtu katika usingizi mzito; Na nafsi yake mvivu itaona njaa.
Mithali 20:13 Usipende usingizi usije ukawa masikini; Fumbua macho yako nawe utashiba chakula.
Mithali 26:14 Mvivu hujigeuzageuza kitandani kama ilivyo kwa bawaba za mlango; ufungwapo na kufunguliwa.
Mtu mvivu ni mzembe wa kutupwa; hata kwa vitu au kazi isiyohitaji nguvu na maarifa yeye humshinda.
Mvivu hata ukimsogezea fursa mlangoni kwake umefanya kazi bure. Hata kama fursa zipo kila mahali, mvivu hawezi kuthubutu katika kujisumbua kufanya jambo lolote, maana yeye kila jambo kwake ni kero na usumbufu. Mtu mvivu ni sawa na mtu asiyeweza kufunga goli katika mpira wa miguu, hata kama mlinda mlango (goal keeper) akiondoka, yeye hawezi akafunga.
Mithali 19:24 Mtu mvivu hutia mkono wake sahanini; Ila hataki hata kuupeleka hata kinywani pake.
Mtu mvivu hujiona sahihi kwa hali aliyonayo, hata kama akishauriwa hachukui hatua.Mvivu hawezi akashaurika kwa jambo lolote la mafanikio yake, hujiona sahihi jinsi alivyo, hata ufanye vipi hawezi akabadiliika daima.Mvivu anapotumwa kufanya kazi huwa mkali au hulalamika sana apewapo majukumu ya kufanya.
Mithali 10:26 kama siki menoni, na moshi machoni, ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao.
Mithali 10:26 kama siki menoni, na moshi machoni, ndivyo alivyo mtu mvivu kwao wamtumao.
Mvivu hutawaliwa, hufanywa mtumwa na wale wenyebidii na waliofanikiwa.
Mvivu haheshimiki, hugandamizwa na kunyonywa na wale waliofanya bidii katika maisha yao na kufanikiwa. Kwa kuwa uvivu huleta umasikini, basi mvivu ni mtumwa kwa wale waliofanikiwa au kujibidisha katika kazi.
Mithali 12:24 “Mkono wa mwenye bidii utatawala; Bali mvivu atalipiswa kodi”
Mtu mvivu ni ombaomba; hali na kutumia vya jasho lake mwenyewe
Mvivu hawezi kujibidisha ili apate pesa, vitu, au mali itokanayo na nguvu zake; bali yeye haishi kuomba kila kukicha. Kwa kukosa fikra yakinifu za kujitambua pamoja na kujituma katika kutafuta na kufanya kazi.
Mithali 12:27 Mtu mvivu hapiki mawindo yake; Bali mwenye bidii anamali za thamani.
Neno la Mungu pia linawaonya watu wavivu wanaokula, kutumia na kuishi kwa kutegemea jasho la watu wengine.
2Wathesalonike 3:10, 12 10Kwa kuwa hata ule wakati tupokuwapo kwenu tuliwaagiza neno hili, kwamba ikiwa mtu hataki kufanya kazi, basi, asile chakula .Basi twawagiza hao, na kuwaonya katika Bwana Yesu Kristo, watende kazi kwa utulivi na kula chakula chao wenyewe.
Mtu mvivu hupenda maisha rahisi, hapendi kujitesa katika bidii ya kutafuta. Mvivu hapendi kujisumbua, kujibidisha katika kazi, wala kuteseka ili hapo baadae afanikiwe na kufaidi matunda yake; bali yeye (mvivu) hupenda maisha rahisi yenye mteremko ili aserereke hadi mwisho. Maisha ya kupanda mlima kwa mvivu ni machungu mno.
Mithali 20:4 Mtu mvivu kataki kulima wakati wa baridi; Hivyo wakati wa mavuno ataomba, hana kitu.
Mtu mvivu huharibu, hatunzi, hutumia kwa pupa na kwa uharibifu vitu au mali zilizotafutwa na wengine.
Kutokana na kutojua uchungu, mateso, usumbufu, gharama na jasho lililotoka katika kuvipata vitu au mali zilizotafutwa na watu wengine; mtu mvivu azikutapo mali hizo au vitu hivyo yeye hutapanya, hufuja, huharibu, hutumia kwa pupa na fujo vitu au mali hizo. Mithali 18:9 Yeye naye aliye mvivu katika kazi yake ni ndugu yake aliye mharabu.
2017 Roho ya uvivu ikuondoke,upende kufanya kazi kwa bidii,acha kuwalalamikia watu.Mvivu ana wivu na maendeleo ya wengine.Mtu mvivu ni mzigo, habebeki ni mleta ugomvi ni mgombanishi hajui kutumia akili yake.
Nunua nyumba, mashamba,endesha magari,vaa vizuri,kula unavyotaka, nenda saloon asubuhi na jioni kwa pesa ya kujitafutia mwenyewe ili upate heshima kwa Mungu na wanadamu.Mungu akubariki
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment