Saturday, 14 January 2017

NILIMUOA DADA YANGU

Mtunzi Jimmy luoga

Simu +255 755 714 395
EPISODE:3

Ilipoishia tulimuona Daniel ambaye kwa sasa alijiita Erick akifanikiwa kuingia Jiji la Dar es salaam na kukutana na Allen ambaye naye anadai kuwa ni mwenyeji wa Mbinga mkoani Ruvuma, wanajikuta wakikubaliana kuwa marafiki wa damu.Kutokana na Allen kuwa mwenyeji katika Jiji hilo anaamua kumueleza majukumu ambayo yanamfanya yeye aweze kujipatia ridhiki yake ya kila siku, Je ni majukumu gani hayo? Ungana nami sehemu hii ya tatu ili tuweze kujua hatma ya simulizi hii.

SASA ENDELEA..............
Nilijikuta natamani kumuuliza Allen ni majukumu gani ambayo yangeweza kunipatia fedha ambazo zingeniwezesha kuishi katika Jiji hilo la Dar es salaam, Allen alikaa kimya kwa dakika kadhaa kisha akakohoa kidogo kuweka koo lake sawia kisha akaanza kunieleza majukumu hayo, katika majukumu yote aliyonielekeza sikuona zuri hata moja kwani alipofikia jukumu la tatu mapigo ya moyo wangu yalienda kasi na kumueleza Allen sikuwa tayari kwa majukumu yote hayo labda kidogo lilinivutia jukumu la kwanza ambalo lilikuwa ni la hatari pia ila niliona lilikuwa na uafadhali.Majukumu aliyonieleza Allen yalikuwa kama ifuatavyo; moja ni la kuosha magari barabarani japo alisema kuwa kuna baadhi ya madereva wa magari hawakuwalipa pia ilihitaji wepesi wa hali ya juu hasa kwenye msongamano mkubwa wa magari yanaposimama ndipo kazi hiyo ingefanyika, jukumu la pili sikuvutiwa nalo ambalo niliona mwisho wangu ingelikuwa kifo au kuishia gerezani, hilo lilijihusisha na vitendo vya wizi wa vioo vya magari (site mirror) na jukumu la mwisho alidai kuwa hilo ndio lilikuwa na malipo ya pesa nyingi kila walipofanikiwa wakiongozwa na mkubwa wao ambaye alinitajia jina moja la Mnene. Jukumu hilo lilikuwa ni la kutisha na kuhudhunisha, Allen alisema kwamba wao walikuwa wakitumiwa na huyo Mnene kuchunguza misiba inayotokea Jijini zaidi ya watu maarufu kisha walichunguza pia aina ya majeneza waliyozikia yalikuwa na gharama kiasi gani kisha baada ya mazishi kikosi chao kikiongozwa na Mnene walikwenda kufukua kaburi kisha kuchukua jeneza na maiti kuizika bila jeneza.Allen aliendelea kunihadithia kuwa majeneza hayo yaliuzwa kwa bei ghali na kuwafanya wao waweze kuishi maisha mazuri japo mpaka wakati huo Allen tulikuwa tumeamka wote pale uchochoroni.Mara baada ya kumsikiliza kwa makini kama dakika arobaini na tano ndipo nilipomjibu Allen kuwa kati ya kazi hizo zote niliona yenye unafuu ni ile ya kuosha magari ingenifaa japo nayo sikuipenda toka moyoni, Allen alinitazama kisha akaniambia kazi hiyo ilihitaji niwe ngangari kweli kwani baadhi ya watoto wa mitaani walikuwa wakiwanyang'anya pesa wale ambao walionekana kuwa wapole sana.Nilimjibu Allen kuwa nitapambana nao vivyo hivyo, majira ya saa tano asubuhi tayari mimi na rafiki yangu Allen tulikuwa na maji yetu kwenye ndoo ndogo huku mikononi tukiwa na sado kila mmoja kitambaa na sabuni ya unga, moja kwa moja kazi ilianzia pale Kariakoo round about, nilijifunza kupitia mwenyeji wangu Allen ambaye alionekana kuwa mwepesi zaidi kila magari yaliposimama aliingia katikati na kuanza kuosha gari haraka tena kuna baadhi ya madereva walimtukana na hata wengine kutaka kumsukuma na gari.Nilijikuta nikimwonea huruma rafiki yangu kwani kuna baadhi ya madereva japo walisafishiwa magari yao hawakumpa hata shilingi, baada ya kupigiwa jua kama lisaa limoja Allen alifika mpaka pale nilipokuwa nimesimama mimi "Erick umeona kazi ilivyo ngumu?, mpaka sasa nimeambulia shilingi mia tano tu" maneno hayo ya Allen yaliuchoma moyo wangu kwani sikutegemea kuona baadhi ya Watanzania wakiwa na roho ngumu kiasi hicho, nilimwambia Allen apumzike na mimi nikajaribu bahati yangu, jambo moja ambalo Allen alinisisitiza kuwa makini pale barabarani.Nilichukua kopo moja la maji yaliyochanganywa sabuni ya unga na kitambaa changu mkononi kisha nikaanza kupiga hatua mpaka pale barabarani, ile nakanyaga barabara tu nilisikia jina langu likiitwa kwa mbali kama vile nilikuwa naamka usingizini, tokea dakika hiyo nilijiona kama vile nilikuwa usingizini naota ndoto ambayo sikuweza kuielewa mwisho kwa mbali niliweza kusikia sauti ya mtu ikiita jina langu la Erick mfululizo, nilipofumbua macho nilimwona Allen akiwa anabubujikwa na machozi, pembeni yake alisimama mzee mmoja wa kizungu, nilipoangalia mkono wangu niliona mrija wa damu uliotokea juu ambapo niliona chupa ya damu.Allen alinikumbatia kwa nguvu huku akiwa analia kwa furaha, nilijaribu kuvuta kumbukumbu lakini ziliishia pale nilipokuwa nakanyaga barabara, yule mzungu alitutazama huku akiwa kaachia tabasamu mdomoni kwake.Nilimuuliza Allen kulikoni nilikuwa hapo hospitali naye taratibu akaanza kunihadithia ilivyokuwa na nilipomuuliza kuhusu huyo mzungu alinijibu kuwa yeye ndiye aliyenigonga na gari lake hivyo alihaidi kunisaidia mpaka ningelipona, yule mzungu alisogea mpaka pale nilipokuwa nimelala kisha akapiga magoti, alijitahidi kuzungumza kiswahili kisha akaniomba msamaha nami nikamsamehe, alisimama kisha akahaidi kutusaidia mimi na rafiki yangu Allen.Namshukuru Mungu kuwa nilivunjika mguu mmoja hivyo baada ya juma moja kupita niliruhusiwa kutoka pale hospitali ya Taifa Muhimbili, namshukuru yule mzungu ambaye alijitambulisha kwa jina la Andrew kuja kutuchukua pale hospitali na kutupeleka mpaka nyumbani kwake Tegeta.Maisha katika jumba la Andrew yalianza nikiwa natembelea magongo mpaka wakati wa kufungua lile hogo uliwadia, afya yangu iliendelea vizuri chini ya usimamizi wa rafiki yangu Allen ambaye nilimuona kama kaka yangu na Andrew kama Baba yetu, pale ndani Andrew alikuwa akiishi peke yake isipokuwa mchana walikuja wafanyakazi wa kazi za ndani kisha waliondoka jioni.Siku zilianza kwenda huku Andrew akitulea sisi kama wanae, nakumbuka siku moja tukiwa tumeketi sebuleni mzungu aliomba tumueleze yaliyotusibu mpaka tukafikia hatua ya kuosha magari pale barabarani.Mimi na Allen tukamuongopea yule mzungu kuwa sisi tulikuwa mtu na mdogo na wazazi wetu walifariki kwa ajali ya Meli ya MV BUKOBA, Andrew alituonea huruma hivyo alihaidi kutupeleka shule.Nilijisikia furaha kusikia habari hiyo kwani ndoto zangu za kuwa mtu mbele za watu niliona zikianza kurejea ghafla.Baada ya siku kadhaa tukiwa tumevalia sare za shule za gharama tuliwasili shule ya kimataifa ijulikanayo kwa jina la International Academy iliyopo Mikocheni mkabala kabisa na kiwanda cha Coka cola, niliendelea darasa la nne na Allen la tano, japo lugha ya kufundishia ilikuwa kiingereza lakini tulisoma kwa bidii mpaka tukawa tunashika nafasi nzuri darasani.Siku zilikimbia miezi na miaka pia ilikatika, nilijikuta nikisahau kabisa kijijini nilikotoroka, mimi na Allen tulimheshimu Andrew kama Baba yetu kwani kwa kudhihirisha hilo shuleni jina la pili tulitwa Andrew.Mara baada ya kuhitimu kidato cha nne pale International Academy nilienda shule aliyokuwa ametangulia kaka yangu Allen Aghakhan Sekondari ambapo nilihitimu na kufaulu vema masomo ya sayansi.Mwaka huohuo nilichaguliwa kujiunga Chuo kikuu Muhimbili kusomea shahada ya Udaktari wakati huo Allen alikuwa mwaka wa pili Chuo Kikuu Dar es salaam shahada ya Uchumi.Siku moja nilimtembelea Allen pale chuoni kwao, nikiwa nimejiziuka kuongea na simu na Allen aliyekuwa akinielekeza mahali alipokuwa ghafla niligongana uso kwa uso na msichana mrembo na kumsababishia daftari zake zianguke chini..........

Je msichana huyo ni nani? Erick na Allen sasa ni ndugu je nini hatma ya undugu wao? Ungana nami Alhmis.
Pia naomba niwaeleze wale wanaopenda kukosoa kazi za wenzao wafungue page zao wafundishe lugha wenzao vinginevyo unakuta watu tunachukizwa na hizo tabia zenu na kuacha hata kurusha stori kwa kuona shukrani za tembo mateke.Jirekebisheni kwani hatulipani hapa.

No comments:

Post a Comment