Saturday, 14 January 2017

NILIMUOA DADA YANGU

Mtunzi ni Jimmy Luoga

Namba +255 755 714 395

EPISODE:2

Ilipoishia tuliona mtoto Daniel aliyebadili jina lake na kujiita Erick akikimbia kwa Mpemba mara baada ya kutaka kumuingilia kinyume na maumbile, moja kwa moja anakimbilia Bandarini ambapo anapata wazo la kuzamia Meli na kwenda jiji la Dar es salaam, Je Erick atafanikiwa kuzamia Meli? Ungana na mtunzi wako Jimmy Luoga kujua nini hatma ya Erick?

SASA ENDELEA..............
Nilisimama kandokando ya bahari takribani nusu saa huku nikitafakari nitumie njia gani ili niweze kutoka katika Mkoa wa Mtwara na kwenda kuanza maisha mapya jijini Dar es salaam ambao habari na sifa za uzuri wa jiji hilo nilizisikia na hata kusoma kwenye vitabu mbalimbali pale shuleni kwetu KIUMA, baada ya kukaa kwa muda mrefu nikipata wazo ambalo lilinifanya nijivute mpaka pale bandarini ambapo niliwakuta baadhi ya abiria wakiwa wamelala pale kituoni kwa ajili ya kuwahi Meli za alfajiri.Nami pia niliamua kutafuta sehemu ambayo ilinivutia kisha nikajilaza bila ya kutandika wala kujifunika chochote hivyo mwili wangu ulikuwa chakula cha mbu usiku huo.Ilikuwa kama majira ya saa saba usiku kwa mbali giza lilianza kutawala katika macho yangu na kupelekea usingizi mzito ulioambatana na ndoto iliyorejelea tukio la siku ambayo nilimpiga Baba na ule mtwangio, lakini nilipokuwa nanyanyua juu ule mtwangio na kutaka kumpiga nao Baba kichwani nilishtuka na kuona abiria wakiwa wamepanga foleni wakielekea ilikotia nanga Meli, moja kwa moja nami nikafuata foleni hiyo japo sikuwa hata na risiti ya kusafiria, yule aliyekuwa anakagua risiti pale getini hakuniuliza chochote kwakuwa mbele yangu kulikuwa na mama mmoja aliyevalia baibui akiwa mtoto mmoja kambeba na mwingine akiwa kamshika mkono, hivyo kwakuwa na mimi nilikuwa nyuma ya yule mtoto aliyemshika mkono mkaguzi wa risiti akajua na mimi huenda nilikuwa mtoto wa yule mama.Mara baada ya kuingia ndani ya Meli hiyo kubwa ya abiria ambayo hata jina lake sikulitambua niliendelea kumfuata yule mama mpaka mahali ambapo aliketi "shikamoh mama!" nilimsalimia yule mama kwa heshima naye akaitikia kisha nikamuomba aniruhusu nimpakate mwanae yule aliyemshika mkono kwani kwa haraka nilikadiria alikuwa na umri kama wa miaka mitano, yule mama aliniuliza wazazi wangu walipo nami sikufanya ajizi nikamuonyesha mzee mmoja wa makamo akiyekuwa siti ya mbele yetu.Yule mama alikubali kwani dhahiri alionekana zaidi kuwa mcha mungu na pia alilelewa vema katika maadili ya dini ya kiislamu, Nilifurahi yule mama alipokubali ombi langu kwani yeye alichukua siti mbili ambapo niliamini iwapo mhudumu anayekagua risiti mule ndani angepita hasingeweza kunishtukia.Mungu si Athman mambo yalienda kama nilivyopanga kwani hata yule mkaguzi alivyopita hakuweza kuniulizia risiti bali yule mama alitoa risiti mbili kisha akaendelea kukagua sehemu nyingine.Njiani yule mama alitupatia chakula ambacho alitoa kwenye vitunza vyakula, nilimshukuru yule mama kwa wema wake kwani alinilea mule ndani kama mwanae mpaka Meli ulipotia nanga katika bandari ya Salama, lakini kabla sijateremka nilimshukuru tena yule mama kisha nikaomba anitajie jina lake na mtaa aliokuwa anaishi bila kujua dhamira yangu ilikuwa ni nini, aliniambia kuwa anaitwa Mama Asha na alikuwa anaishi Magomeni Mwembechai.Mara baada ya utambulisho huo tuliagana, nilitoka pale bandarini nikiwa sijui hata kwa kuelekea kwani kwa haraka niligundua ilikuwa kama majira ya saa kumi jioni, nilijitazama toka chini mpaka juu niliishia kuguna, kwani miguuni nilikuwa chama cha kuku yani peku pia nilivaa suruali na shati lililokatika vifungo baadhi, joto la jiji hilo lilizidi kunichosha na kuanza kujikuta nikijilaumu kwanini nisingebaki pale Mtwara ambako niliamini ningeweza kupata kazi mahali pengine ukiacha kwa Mpemba aliyetaka kunifanyia uhaini mkubwa.Nilijikuta natembea bila kutambua hatma ya safari yangu ilikuwa ni wapi, nilivuka barabara kwa shida kwani tayari nilishafikisha umri wa miaka kumi na moja, baada ya dakika kadhaa kiu ilinishika na kujikuta koo likikaukiwa hasa, bahati nzuri mbele yangu nilimuona kijana kasimama huku akiwa ameshika deli kama la barafu nilizokuwa nauza mimi kwa yule Mpemba, nikamsogelea japo niombe msaada wa barafu moja nikate kiu, nilipomuuliza kabeba nini alinijibu kwa furaha kuwa alibeba maji ya pakiti hivyo nilitumia kauli ya kuomba msaada japo pakiti moja naye alinipatia haraka, jambo la kushangaza nilipotaka kuondoka alidai fedha, nilijaribu kumuelekeza kuwa niliomba msaada lakini hakunielewa hivyo kwa hasira alinivua shati na kuniacha tumbo wazi, nilijikuta nikilia mpaka msamalia mwema mmoja aliponiona na kuniuliza kulikoni, nilipomueleza alinipatia shilingi elfu moja hivyo nikamlipa muuza maji shilingi mia yake na kunipatia chenji na shati langu.Tayari giza lilianza kuchukua nafasi bila kutambua nilikuwa wapi muda huo, "Gongo la mboto Gongo la mboto!" ni sauti ya konda iliyokuwa ikiitilia na kuona watu wakigombania kuingia garini, nilijikuta nikiachia tabasamu kwani kule kwetu Tunduru mambo hayo sikuwahi kuona, nilizidi kupiga hatua kwenda mbele nikaona sanamu moja katikati ya barabara likiwa limeshika bunduki huku magari yakilizunguka, nilijikuta nikicheka peke yangu.Nilitembea kwenda mbele zaidi kwani tayari taa za majumba marefu kama yaliyokuwa yakianguka ziliangaza, nilipepesa macho mpaka jengo moja refu lilinijulisha kuwa hapo palikuwa Mnazi mmoja, niliendelea kutembea bila kujua nilikokuwa naenda lakini mwisho nilitokea mahali ambapo kidogo palinivutia, hapo watu wslikuea kwenye shamrashamra za kupanda magari na wrngine waliuza nguo na viatu vilivyotandazwa chini "samahani kaka sijui hapa ni wapi?" yule kijana alinijibu huku anatembea kuwa pale ni Kariakoo, hivyo nikakumbuka simulizi mbalimbali kutoka kwa watu wa pale kijijini kwetu juu ya mtaa huo uliosifika kuwa na soko kubwa nchini.Tayari ilikuea kama majira ya saa tatu kasoro usiku na njaa tayari ilishaanza kuniuma na wakati huo mfukoni nilikuwa na ile shilingi mia tisa niliyobaki nayo, nilsogea mpaka kwenye kibanda kimoja walichokuwa wanachoma chips ambapo baada ya kuuliza bei ya chips zao niligundua kuwa iwapo ningeagiza kavu ningebakiwa na shilingi mia nne ya chai asubuhi.Mara baada ya kuagiza na kula nilianza safari ya kutafuta mahali pakulala, nikakamata barabara kama naelekea Msimbazi kisha nikakata kulia ambako kulikuwa na uchochoro, nilpoanza kupiga hatua nilianza kuona watu wakiwa wametandika maboksi na kulala, sikushangaa namimi pia nilitafuta maboksi kisha nikayatandika vema nakuuchapa usingizi mzito.Alfajili ya siku ya pili niliamka kama wenzangu na kujiuliza wapi ningeanzia "dogo umetokea mkoa gani?" ni swali ambalo niliulizwa na mtoto mwenzangu ambaye alionekana kunizidi kama miaka mitatu hivi, sikutaka kuwa mtata nilimjibu kuwa nilitokea Mkoa wa Ruvuma Wilaye ya Tunduru, yule mtoto alifurahi akanieleza yeye pia ni mwenyeji Mbinga mkoa huohuo pia akanitajia jina lake la Allen Komba.Wote wawili tulijawa na furaha na kuhaidiana kuwa marafiki wa kudumu.Allen alinisimulia mkasa mzima uliompeleka Dar kuwa ni ukatili aliokuwa akifanyiwa na mama yake wa kambo mara tu baada ya mama yake mzazi kufariki na baba yake kuoa mke mwingine, nilimpa pole kisha nami nikamsimulia mkasa mzima.Kwakuwa Allen alikuwa mwenyeji alinielekeza majukumu ambayo yeye yalimuwezesha kukidhi mahitaji yake ya kila siku.....

Je ni majukumu gani hayo? ungana naming toleo lijalo uweze kujua nini hatma ya Daniel jijini Dar es salaam na huyo rafiki yake Allen.

No comments:

Post a Comment