Mtunzi Jimmy Luoga
EPISODE:6
Ilipoishia tuliona Erick akipata nafasi aliyokuwa akiitafuta muda mrefu ya kuonana pia kuzungumza na Liz msichana aliyetokea kuiteka nafsi yake kimapenzi, Je Liz atakubali kujibu maswali ambayo Erick alihitaji kumuuliza?
SASA ENDELEA....................
Mara baada ya msichana huyo aliyejitambulisha kwa jina la Liz kukubali kujibu maswali yangu nilianza kutambua Mkoa aliotokea, alinijibu kuwa yeye alikuwa mwenyeji Shinyanga Wilaya ya Kahama, lakini kuna kitu kimoja kilinishtua juu ya lafudhi yake na kupelekea kumuuliza swali kiutani "hivi Liz hujawahi kuishi Tunduru maana lafudhi yako inafanana sana na watu wa huko?" Liz alishtuka kwani macho yangu yaliweza kugundua hilo lakini yeye alikataa katakata kuwa hakufahamu huko Tunduru, niliamua kubadili mada na kumuuliza kama alikuwa na mchumba pale chuoni au ndani ya Jiji la Dar es salaam, lakini jibu alilonipatia lilizidi kunipa matumaini kuwa msichana huyo ningemmiliki muda si mrefu kwakuwa alinieleza kuwa hakuwa na mchumba wala hakuitaji mchumba.Nilimtazama usoni msichana huyo aliyeonyesha kuwa amelewa kupitia macho yake aliyokuwa akiyarembua na kufanya niweze kufaidi uzuri wake, nilitamani Allen na mpenzi wake wasitoke mapema ili mimi na Liz tuendelee kuzungumza, baada ya Liz kumaliza kinywaji nilimuongezea tena na tena huku tukisindikiza na nyama choma, masaa yalikatika huku mimi na Liz tukiendelea kunywa na kula, giza lilishaanza kuingia kwani nilipojaribu kutazama saa yangu ya mkononi ilionyesha kuwa ilikaribia saa mbili usiku.Ghafla Allen alitoka ndani akiwa peke yake huku akiwa amevalia pensi na kawoshi yake, akijongea mpaka pale tulipokuwa mimi na Liz kisha akaniita pembeni kwa faragha "vipi Erick mmefikia wapi na huyo mtoto?" Allen alipenda sana utani hivyo hata wakati ananiuliza hivyo aliingiza na utani ndani yake, nilimjibu kuwa nilipofikia naye hapakuwa pabaya sana japo nilimueleza kuwa kuna baadhi ya mambo kama alinificha "Erick mdogo wangu hili ndio Jiji la Dar es salaam kwani wewe ni Erick si ni Daniel?, wewe unachotakiwa kufanya ni kumtia mikononi huyo mlimbwende basi" maneno ya Allen yalinibadilisha na kunitoa wasiwasi, "sasa sikiliza Letisia leo harudi na hapa kanituma nije nimueleze rafiki yake hiyo habari, sasa kazi kwako utachagua mwenyewe kumrudisha hostel au kumdanganya alale hapa?" Allen alimalizia kisha tukarudi mpaka pale alipokuwa Liz.Mara baada ya kufika tu pale Allen alimueleza Liz kama alivyoagizwa na rafiki yake Letisia kisha akatuaga na kuingia ndani, "samahani Erick nilikuwa naomba nirudishe hostel kama itawezekana" yalikuwa maneno ya msichana huyo ambaye aliongea kilevilevi, nilijaribu kumuomba alale pale lakini alionyesha msimamo kuwa hakuwa tayari kulala nje ya hostel, alinyanyuka kisha akayumba kidogo na kunifanya moja kwa moja nitambue kuwa msichana huyo alikuwa kalewa kupita kiasi, nilijaribu kumsisitiza abaki pale nyumbani tena chumba cha wageni lakini bado haikumuingia akilini.Nilivyoona msimamo wa msichana huyo nikawa sina namna zaidi ya kutekeleza matakwa yake, wote kwa pamoja tuliingia kwenye gari na kuanza safari ya kuitafuta Mabibo hostel mahali ambapo Liz na Letisia walikuwa wanaishi, tukiwa njiani Liz alionekana akiongea sana jambo lililonivutia zaidi."Erick unakumbuka siku ya kwanza tulipogongana?" lilikuwa swali ambalo sikutegemea kuulizwa na Liz akiwa katika hali ile, wakati huo tulikuwa tukipita Mwenge na kunyoosha kama tunaelekea BAMAGA kisha nikakatisha kilipo chuo cha Ustawi wa Jamii kuelekea Sinza, nilimjibu Liz kuwa niliikumbuka sana siku hiyo, "sasa nikuambie kitu Erick?" Liz aliuliza kwa sauti ya kilevi jambo lilinifanya nipunguze sauti ya redio na kutaka kumsikiliza Liz kwa makini zaidi "Erick siku zote umeutesa moyo wangu huwezi amini" nilijikuta nikishangilia kimoyomoyo mara baada ya msichana huyo kunitamkia maneno hayo kwani siku zote nilijua mimi peke yangu niliumia kumbe wote tulikuwa tunataabika juu ya mapenzi, "Etick wewe ni mwanaume wa kwanza kuuteka moyo wangu, samahani kama nitakuwa nimekukwaza kwani kwa muda mrefu nilitamani nikuone lakini sikupata nafasi hiyo" Liz alimaliza kisha akaegemeza kichwa chake katika siti, lakini haraka niligundua kuwa alishauchapa usingizi mzito, nilijikuta nikifurahi kupita kiasi kwani siku zote sikujua kama Liz naye alinipenda kama mimi nilivyompenda.Lakini jambo moja liliniumiza kichwa kuwa amenieleza hivyo kwakuwa amelewa au amenitega?, tayari nilikuwa naiacha Sinza kupitia barabara ya Shekilango na kuingia barabara ya Manzese ambayo inatokea Ubungo, niliendesha gari haraka huku nikitazama uzuri wa Liz ambaye alikuwa kauchapa usingizi mzito, muda wote niliyarejea maneno yake kuwa alinipenda toka aliponiona mara ya kwanza.Baada ya dakika kadhaa nilikuwa nikimuamsha Liz kuwa tayari tulikuwa tumeshawasili hostel kwao, aliteremka toka ndani ya gari kisha akanishukuru kwa kunikumbatia kama vile alikuwa mpenzi wangu wa muda mrefu, tulipeana namba za simu kisha tukaagana.
**********************
Zilipita kama siku mbili bila kuwasiliana na Liz, nikiwa kwenye gari naelekea chuoni kwangu Muhimbili mara simu yangu iliita, nilipoitazama vizuri nilifurahi kuona jina la Liz likiwa juu ya kioo cha simu yangu, upesi nilipokea simu ambayo nilishushiwa lawama za kutomtaka khali tokea siku niliyomrudisha pale hostel, nilimuomba msamaha Liz kwa madai kuwa nilikuwa na kazi nyingi siku ya pili yake.Liz alinisikiliza, mwisho tulikubaliana tungekutana siku ya ijumaa mahali ambapo tungekubaliana.Siku niliona zimeganda kwani siku hiyo ilikuwa jumanne hivyo niliamua kujiweka bize na masomo na hata pale nilipokuwa huru nilizungukia kampuni nilizoachiwa na marehemu Baba yangu mlezi Andrew Reuben ambazo zilizidi kuhimalika siku hadi siku na sifa zake kuenea ndani na nje ya nchi.
Ilikuwa ijumaa tulivu katika Jiji la Dar es salaam majira ya saa moja usiku katika ufukwe wa Koko nikiwa napigiwa upepo mwanana kutoka bahari ya Hindi, ndipo nilipomuona mhudumu akija mahali nilipoketi na kunieleza kuwa nilikuwa na mgeni wangu upande wa Bar, nilishatambua kuwa huyo hakuwa mwingine zaidi ya Liz ambaye tulikubaliana tukutane hapo.Ni kweli mawazo yangu yalikuwa sawia, nilimkuta Liz akiwa ananisubiri katka meza ya peke yake, siku hiyo alipendeza maradufu ya ile ya kwanza, nilijikuta napata hamu ya kumrarua siku hiyo........
Itaendelea toleo lijalo
No comments:
Post a Comment