Mtunzi ni Jimmy Luoga
EPISODE:4
Ilipoishia tulimuona Erick akimtembelea Allen pale chuo kikuu Mlimani, akiwa anaongea na simu ghafla aligongana na msichana mrembo ambaye daftari zake zilianguka chini.Je ni kiliendelea? Ungana nami katika sehemu hii ya nne.
SASA ENDELEA........
Yule msichana alinitazama kwa macho yake makubwa mpaka niliogopa kwani hakuongea kitu zaidi alisimama vilevile, kwa woga wa yale macho makubwa mazuri mithili ya mtu aliyekula kungu nilijikuta nikichuchumaa na kuanza kuziokota zile daftari, yule msichana alisimama vilevile huku akionekana kukasirishwa na lile tukio.Baada ya sekunde kadhaa niliinuka nikiwa na zile daftari mkononi, nilinyoosha mkono wangu kumpatia yule msichana daftari zake lakini yeye alibaki kunitolea macho tu, "hivi kakangu hivyo visimu vya kichina vinawachanganya sana eh?" nilishtuka kutokana na swali la msichana huyo, nilijaribu kujishusha kisha nikamuomba anisamehe kwani sikufanya makusudi, "sawa nimekusamehe ila siku nyingine jaribu kuwa mstaarabu unapoongea na simu kuangalia sisi watoto wa masikini tunaoshindwa kumiliki hata hiyo michina" nilijikuta nikiishiwa pozi mara baada ya huyo msichana aliyevalia sketi fupi nyeusi iliyomkaa sawia na blauzi nyeupe aliyoichomekea vema na kumfanya apendeze zaidi.Ghafla yule msichana alizivuta zile daftari zangu toka mikononi mwangu kwa nguvu kisha akaanza kupiga hatua kuondoka mahala pale, nilijikuta nikigeuka na kumtazama vema yule msichana ambaye nilimuona kuwa amejaa dharau toka sura yake macho midomo na hata mwendo wake, nilijikuta nikianza kuvutiwa msichana huyo aliyekuwa mlimbwende haswa.Niliendelea kumthaminisha kuanzia miguu yake aliyoiacha wazi kwa ile sketi yake fupi na kiuno chake kama cha nyigu, alizidi kuniacha hoi na umbo lake la kibantu na kunifanya nijikute nikijilaumu kwa kutomuuliza jina lake wala kutoomba namba yake ya simu, lakini kwa ukali na hasira alizokuwanazo ningejaribu kuomba namba ya simu au kuulizia jina lake huenda angenitukana "vipi mdogo wangu mbona umesimama hapa kama vile kuna kitu unatazama" ilikuwa sauti ya Allen ambaye alishazoea kuniita hivyo tokea tulipomdanganya Andrew kuwa sisi tulikuwa mtu na mdogo, wakati huo tayari nilikuwa nimefikisha umri wa miaka ishirini na tatu na Allen ishirini na tano, nilishtuka kwani bado nilikuwa nikitazama njia ile aliyopotelea yule msichana, nilimdanganya kuwa kuna kijana nilimfananisha hivyo nikatumia muda mrefu kumtazama.Allen alinijibu kuwa duniani wawili wawili huenda nimemfananisha, mara baada ya mazungumzo ya hapa na pale Allen aliniomba nimfuate akanitambulishe kwa rafiki zake, nilishangaa akiniongoza njia ileile aliyoelekea yule msichana badala ya kule alikotokea, sikujali wala sikujiuliza maswali mengi zaidi nilimfuata nyuma mwenyeji wangu.Baada ya kutembea kwa dakika kama mbili tulianza kupita kwenye vimbweta (viti vilivyojengelewa) vilivyokaliwa na wanachuo mbalimbali wakisoma kwa kujadiliana katika makundi, safari yetu iliishia kwenye kundi moja lililokuwa na mchanganyiko wa wa wavulana na wasichana, "habari za saa hizi jamani!" Allen alianza kwa salamu na kuwafanya wale wote waliokuwa pale wakijadiliana kutugeukia sisi na kwa pamoja waliitikia "nzuri", "siku zote nilipowaambia kuwa na mdogo wangu anasoma Chuo kikuu cha Tiba Muhimbili hamkuniamini huyu ndio yule mdogo wangu mwenyewe" , almanusura nizimie nilipogongana macho kwa macho na yule msichana niliyemgonga dakika chache zilizopita baada ya kunitazama vizuri, kwa mara ya kwanza niliweza kuona tabasamu la msichana huyo ambaye alikuwa na mvuto wa aina yake, wote kwa pamoja walinichangamkia na kunikaribisha.Muda wote akili yangu ilimuwaza yule msichana ambaye nilimwangalia kwa kumvizia bila hata yeye kujua, "nilikuwa naomba nimtembeze na kumuonyesha mandhari ya hapa chuoni kwetu" wale wenzake hawakupinga, lakini niliona kama Allen aliniwahisha kuondoka katika eneo lile kwani tayari nilishapagawa na urembo wa yule msichana, niliondoka kwa shingo upande na hata kabla sijapotea toka eneo lile niligeuka nyuma na kujikuta tukigonganisha macho yetu kwa mara nyingine."Allen kakangu chuo chenu kizuri sana ila kuna jambo moja ulisahau kunieleza" Allen alinitazama kisha akaniuliza jambo gani, nikamwambia kuwa alisahau kunitambulisha wale wanakundi wenzake, alicheka kisha akanijibu kwa mkato kuwa isingenisaidia kitu kwani ningesahau baada ya dakika kadhaa, laiti kama angejua kuwa lengo langu lilikuwa nini asingeongea vile.Safari yetu iliishia nilipoegesha gari kisha wote tukaingia kurudi nyumbani.Mara baada ya kufika nyumbani tulimkuta Andrew ambaye ndiye tulimuona kama baba yetu wa kutuzaa akiwa amejilaza kwenye kochi akiwa anatetemeka japo jua kali lilikuwa likiwaka nje, moja kwa moja tulitoka mbio mpaka pale kwenye kochi kisha tukaanza kumuuliza kulikoni lakini hakujibu kitu, haraka tulimbeba Baba yetu mpaka kwenye gari na kisha mimi niliendesha kwa kasi ya ajabu mpaka Muhimbili, kwa kuwa baadhi ya madaktari walinifahamu walijaribu kumshughulikia Baba yetu mlezi kwa hali na mali lakini baada ya lisaa limoja kupita daktari mmoja ambaye nilimfahamu kwa jina la Makenzi alituita ofisini kwake.Alipoanza kuzungumza tu nilitambua ni kitu gani alitaka kutueleza "tumejaribu kutumia utaalamu na juhudi za hali ya juu lakini tumeshindwa kuokoa maisha ya Mr Andrew" sote kwa pamoja tulishindwa kujizuia machozi yaliyokuwa yakitutoka bila kutarajia.Daktari alituomba tuwe wavumilivu kwani yote ilikuwa ni mipango ya Mungu, tulirudi nyumbani huku mwili wa Baba yetu mlezi tukiacha ukipelekwa mochwari tayari kwa kusubiri taratibu za mazishi zifanyike.Mara baada ya kurudi nyumbani nilimpigia simu meneja wa kampuni yake ya kusafirisha wanyama pori nje ya nchi, alipokuja tulipanga nae taratibu za mazishi kwa Baba yetu mlezi siku zote alitusisitiza kuwa iwapo angefariki tungemzika hapa hapa nchini.Mara baada ya mazishi siku ya tatu kikao kilikaliwa kikiongozwa na Mwanasheria wake aliyemuachia wosia atusomee, Mwanasheria alianza kwa salamu kisha sote tukaitikia, kikao hicho kilihudhiliwa na mameneja wanne katika kampuni zake zote mimi na Allen pia, baada ya salamu Mwanasheria huyo alianza kwa kutaja mali za marehemu zote kisha akahitimisha kwa kumtaja mrithi wa mali hizo, Mwanasheria alisoma hivi "Mimi Andrew Reuben ambaye hapa Tanzania sina ndugu namrithisha mali zangu zote na hati pamoja na akaunti za fedha zangu mwanangu Erick Andrew kutokana na kumsoma tabia yake toka nilipowachukua na kuanza kuishi nao.Ghafla Allen alisimama kwa ghadhabu na kutoka nje bila hata ya kuaga, nilimuomba Mwanasheria asimamishe kikao kidogo kisha nikatoka nje alikoelekea Allen, nilipomkuta Allen alikataa nisimsogelee, nilijaribu kumsihi Allen kuwa nisingemtupa lakini bado hakutaka nimsogelee.Baada ya kuona imeshindikana nilirudi ndani kisha tukahitimisha kikao kwa mimi kusaini mbele ya mwanasheria na wale mameneja kunitambua kuwa kuanzia wakati huo mimi ndio nilikuwa Mkurugenzi wao mpya...
Je, Allen alilidhika na mrithi wa mali za Baba yao mlezi na nini hatma ya Erick na yule msichana?. Ungana nami toleo lijalo.
Usisahau kutoa maoni yako
No comments:
Post a Comment