Saturday, 29 April 2017

NYUMBA YA MAAJABU: 52


Sophia akainuka na kutoka nje, akainama na kuchukua viatu vyake ila wakati anataka kuinua kichwa sasa ili aingie ndani akaona miguu ya mtu amesimama mbele yake, na alipomtazama alikuwa ni Neema, kwakweli Sophia alipiga kelele sana. Kitendo hiko kiliwafanya washtuke wote mule ndani, hata Sophia naye pale nje hakuweza kusogea wala kufanya chochote zaidi zaidi alianguka pale pale.
Bibi ndani alielewa moja kwa moja kilichomkumba Sophia na kufanya atoke nje ambapo Sophia alikuwa ameanguka chini huku akitetemeka tu, bibi alimuangalia Sophia kisha akamuangalia aliyesimama mbele yake, bibi hakuongea chochote zaidi ya kumsaidia Sophia kuinuka na kumuingiza ndani kisha akabeba vile viatu vya Sophia na kuviingiza halafu akafunga mlango wake huku akiwa kimya kabisa.
Hakuna aliyeweza kuhoji wala kusema lolote ukizingatia uoga ulikuwa umewajaa kupitiliza ila bibi nae alikuwa kimya kabisa, mara mlango wa bibi ukaanza kugongwa na kuwafanya mule ndani wazidi kuogopa kasoro bibi mwenyewe ambaye hakuonyesha uoga wa aina yoyote ile na wala hakusema kitu chochote, alionekana akitengeneza dawa tu za aina mbali mbali kisha akainuka na kumpaka Sophia halafu akaenda kumpaka Ibra huku ile hali ya kugongwa mlango ikiendelea na mwishowe ikawa kimya kabisa.
Kisha sasa huyu bibi akaanza kuimba imba nyimbo ambazo hawa wwngine hawakuzielewa, aliimba zile nyimbo kwa muda kama wa masaa mawili hivi kisha akanyamaza na kuanza kuwaangalia mule ndani kisha akawasalimia tena, walishangaa imekuwaje anawasalimia! Waliitikia ila hawakujua kwanini wamesalimiwa, huyu bibi alianza kuongea
“Mizimu yangu nawaomba, angalieni hawa vijana wameteseka sana. Inatosha kwasasa. Mateso waliyoyapata yanatosha. Nawaomba jambo moja tu, huyu anayewasumbua mchukueni, najua hiyo sio kazi ngumu kwenu. Mchukueni ili aache kuwasumbua hawa watu, mateso yale yanawatosha”
Huyu bibi akawa kimya sasa na kimya hiki alikaa kwa muda kidogo kisha akanyanyuka na kuelekea chumbani kwake.

Pale sebleni hakuna aliyeweza kuzungumza chochote na walikuwa kimya kabisa, ikapita kama nusu saa ndipo huyu bibi alipokuja na kuanza kuzungumza nao tena, kisha aliwauliza
“Mnajua kuhusu mizimu?”
Wote wakatikisa vichwa kuwa hawajui ila ni mama Sophia tu aliyejaribu kujibu,
“Mi huwa nasikia kuwa mizimu ni watu waliokufa zamani sana”
“Ni kweli ila vile vile mizimu ni malaika wanaotulinda huwa tu wanavaa ngozi za watu waliokufa, lengo lao kubwa ni kutulinda ili tusiteketee ila muda huo huo tunapowakosea wanauwezo mkubwa wa kutuangamiza”
Sophia akauliza,
“Kwa maana hiyo Neema ni mzimu? Kwahiyo ni malaika?”
“Neema ni mzimu ndio ila si malaika ni jini, nyie humuona kama binadamu ila Neema si binadamu wa kawaida. Na nilishawaeleza kwa kifupi histroria ya Neema, ningewaambia kwa kirefu ila sipendi kupoteza muda juu ya jambo moja. Neema alikuwa na roho mbaya sana tofauti na jina lake, na katika maisha yake alikuwa ni mtu wa visasi sana, hakuna mtu aliyewahi kugombana nae bila ya kumfanyia visasi na hata alipokuwa anakufa alikufa na kinyongo moyoni ndiomana mwisho wa siku ametumiwa na jinni mbaya akiyaendeleza yale matendo yake. Kwa maana hiyo Neema hana amani na hawezi kuwa na amani kwani anatumika vibaya huku duniani kutokana na roho aliyokuwa nayo tangia alipokuwa binadamu wa kawaida”
Bibi akatulia kwa muda na kuendelea,
“Muda niliokuwa nikiimba nilikuwa nikiita mizimu yangu ili inisaidie kuniondolea Neema na kwasasa wameshamshikilia na wamenielekeza cha kufanya”
“Ni kitu gani hiko?”
“Tunatakiwa tukafanye kafara kwenye kaburi la Neema, na kafara hiyo ni kuchinja mbuzi ila huyo mbuzi atatakiwa achinjwe na Ibra”
Hakuna aliyebisha wala aliyepinga kwa wakati huo, kisha huyu bibi akajitolea mbuzi wake kwaajili ya kwenda kufanya hiyo kafara kisha wakaianza safari.

Walipofika makaburini, bibi alisimama kwanza na kumuangalia Sophia kisha akamwambia,
“Mimi sijui kaburi la Neema lilipo ila nimeambiwa kuwa wewe unajua kaburi lake lilipo”
Sophia akamkumbuka yule bonge wa hospitali na akakumbuka jinsi alivyoonyeshwa kaburi la Neema na jinsi alivyopewa maelekezo na yule bonge kwahiyo moja kwa moja aliongoza mpaka kwenye kaburi la Neema ambapo bibi aliwapaka dawa kisha Ibra akatakiwa kumchinja mbuzi juu ya kaburi hilo, kisha naye akafanya hivyo na muda huo huo Ibra akajikuta akiweza kuongea kama zamani. Kwakweli alifurahi sana kwani hakufikiria kama ataweza tena kuongea kama zamani kwahiyo kwake hili lilikuwa ni jambo la kushukuru sana. Alijikuta akimsogelea yule bibi na kuanza kumshukuru bila kikomo, ila huyu bibi alitabasamu tu na kuwaomba waondoke eneo hilo na kurudi nyumbani kwani giza nalo lilishaanza kuingia.
Walipofika tu, kabla hawajaingia ndani bibi akasikia sauti ya mbuzi ikitoka ndani kwake ilihali mbuzi wake wote wapo kwenye banda nje, kwahiyo bibi akawaomba wasiingie ndani kwanza mpaka pale atakapofanya dawa zake. Kwahiyo aliwataka wote kutulia pale nje kisha akaongea ongea maneno na kuingia ndani kwake ambapo alitoka na dawa na kuinyunyiza nyumba nzima kisha akarudi ndani na kuanza kuwaita mmoja mmoja kwa majina tena aliwataka waitike ndio waingie ndani, nao wakafanya hivyo kwahiyo alipowamaliza wote akafunga mlango. Giza nalo lilikuwa limeshaingia tayari, hivyo karibia wote mule ndani walikuwa wamejikunyata
“Jamani, usiku ndio unakuwa na mambo mengi sana, hivyo tunatakiwa kuwa makini sana na huu usiku wa leo kwani yule Neema ndio atamalizia hasira zake leo na kama tukiwa wadhaifu basi atatushinda kwa mara nyingine. Kwa tulichokifanya tumemshind tayari, sasa hatutakiwi kutetereka na chochote. Mkisikia anagonga mlango wala msishtuke, mkisikia anaongea wala msishtuke tuwe kimya kabisa na kama tumelala muda huo basi tulala vizuri kabisa yani hofu na mashaka vyote viondoeni. Huu ni usiku wa mwisho kwake”
Walikubaliana na bibi kisha kuendelea na mambo mengine.

Wakati wamelala yani usiku wa manane wakaanza kusikia mtu akigonga mlango na wa kwanza kusikia mlango ukigongwa alikuwa ni Sophia, uoga ulimjaa ila akashika maneno ya yule bibi kuwa wasiwe na uoga wa aina yoyote ile. Kadri muda ulivyozidi kwenda ndipo ile gonga ya mlango nayo iliongezeka na kuna muda mlango uligongwa kanakwamba anayegonga anataka kuuvunja kabisa. Uoga ulianza kuwajaa ila wakajipa moyo, Sophia alimuangalia yule bibi ambaye alikuwa amelala hoi kabisa na kufanya Sophia azidi kupatwa na wasiwasi ikiwa kama yule mgongaji akitaka kuwafanyia kitu kibaya ikabidi Sophia amuamshe yule bibi kwa kumtingisha ila huyu bibi alipoamka alimpa ishara Sophia kuwa alale tu, kitendo cha Sophia kuambiwa kwa ishara kuwa alale tu kilionwa pia na Tausi na mama yao ambao walikuwa wameshtuka pia hivyo wakarudi tena kuendelea na usingizi ambao kiukweli ulikuwa ni usingizi wa uoga kwani walilala bila amani.
Ulipita muda mrefu kidogo ndipo zile harakati za kugongwa kwa mlango zilipoacha na waliendelea kuwa vile vile hadi kunapokucha, na kulipokucha tu wote waliamka na kukaa huku wakimsikilizia huyu bibi kama wataendelea kuongea.
Huyu bibi alipoamka cha kwanza kabisa alicheka sana na kuwauliza,
“Mbona mpo kimya?”
“Ulisema tusiongee chochote”
Huyu bibi alicheka zaidi na kuwaambia,
“Nilisema msiongee ule usiku kwamaana ya kumkaribisha yule mgongaji ila sio kumekucha hivi na ameshaondoka”
Kisha huyu bibi akachukua dawa nyingine na kuwapaka,
“Hii dawa ni ya mwisho na kuanzia sasa mpo huru kabisa, ila cha msingi na muhimu msirudi tena kwenye ile nyumba”
Sophia akauliza,
“Na vitu vyetu je?”
“Hakuna mlivyoacha zaidi ya zile nguo zenu, kwanza kabisa mnachotakiwa kufahamu ni kuwa ile nyumba imejengwa chini ya majini, ile nyumba inalindwa na majini. Mwenye nyumba alikuwa na majini mengi sana. Jiulizeni kwanini ile nyumba unaweza ukajisahau ikawa wazi ila ukirudi hakuna kilichoibiwa! Kwenye ile nyumba vitu vyote mmevikuta mule ndani, hakuna cha kwenu mule zaidi ya nguo, je naongea uongo?”
Sophia akamtazama mume wake ili apate mrejesho wa majibu kwani yeye hakujua kama mumewe alikuta kila kitu ndani, Ibra akajibu
“Ni kweli bibi, aliyeniuzia ile nyumba aliniambia nichukue na vitu vyote vya mule ndani eti yeye havihitaji tena”
Sophia alijikuta akimuuliza Ibra kwa hamaki,
‘Kheeee, hadi Tv, makochi, Friji, vitanda na magodoro?”
“Sasa mke wangu unafikiri mimi nilikuwa na pesa gani kiasi cha kununua nyumba na kununua fenicha zote zile niweke ndani? Huwezo huo sikuwa nao kabisa, hata hivyo ile nyumba niliinunua kwa bei ndogo sana unaweza sema ni nyumba ya tope ila nikapewa na kila kitu kilichopo mule ndani ambacho gharama yake ilizidi hata bei ya nyumba. Ndiomana wakati tunahama kule tulipokuwa tunakaa mwanzo nikakwambia tusichukue chochote tubebe nguo zetu tu”
Sophia na wote mule ndani waliishia kusikitika tu kwani hata Sophia mwenyewe hakufikiria kama mule ndani walikuwa wakiishi kwenye misingi hiyo.

Bibi aliendelea kuwaambia,
“Kwahiyo kama mtataka nguo zenu labda niwape dawa za kwenda kuchukua hizo nguo na kuachana na ile nyumba kabisa, aliyeachiwa tu ile nyumba ni ana mizimu hatari nay eye kama angeamua kuishi mule angalau angeweza kupambana na hayo majini ila nyumba ilimshinda pia. Je mtaweza nyie watu wa kawaida? Pale ukiwa ni mtu wa dini hakikisha umeshika dini kufa na kupona yani usitetereke hata kidogo maana kitendo cha wewe kutetereka basi ushawapa nafasi wale majini na hapo utajuta kuwafahamu. Ile nyumba kuna kipindi unaweza kwenda eneo lile ukatafuta na kutafuta usiione, kwahiyo jamani ile nyumba sio nyumba ya kawaida na ndiomana siku ya kwanza kabisa nakuona Sophia nilikwambia kuwa ile nyumba ni nyumba ya maajabu”
Wakakaa kimya kwa muda kwanza kwani hakuna hata mmoja aliyekuwa na hamu ya kurudi kwenye nyumba hiyo. Kisha mama Sophia akauliza kitu kingine,
“Je kitendo cha hawa kwenda kuchukua nguo zao kwenye nyumba ile hizo nguo hazitawadhuru kweli?”
“Tena umenikumbusha kitu, kuna jambo nililiona kwenye ndoto usiku kwahiyo cha kuwashauri kwasasa ni bora hizo nguo mkasamehe tu na mkaanze maisha upya kabisa. Achaneni na hizo nguo msije mkahama na majini bure”
“Huyo aliyejenga alikuwa na maana gani kujenga na majini?”
“Ni historia ndefu sana ila aliyejenga nyumba ile alitafuta utajiri kwa waganga ambapo alipewa jinni lililoita wenzie zaidi na zaidi halafu kulitoa jinni lile alishindwa kwani mganga aliyempa alikuwa ameshakufa kwahiyo majini yakawa ndio rafiki zake na akawa anawasaidia hadi kupata damu ya watu na kunywa. Kwahiyo mambo yake mengi sana aliyafanya kwa kutumia majini”
“Sasa itakuwaje ile nyumba kama akienda kukaa mtu mwingine?”
“Ile nyumba kwasasa ni picha tu na kama hamuamini mnaweza kwenda msiione, ila atakayejitia kiburi pale basi atakwenda na maji. Hakuna mwenye uwezo wa kuiteketeza ile nyumba zaidi ya yule aliyeachiwa ambaye hayupo nchini ila siku akirudi kwa hakika mizimu yake itamuonyesha mateso yenu na kumfanya akaiteketeze ile nyumba kwahiyo msiwe na mashaka yoyote”
“Kwahiyo tukirudi majumbani kwetu tunaweza kuishi kwa amani?”
“Ndio mtaishi kwa amani kabisa ila kwa ushauri nawaomba kila mmoja aende kwa kiongozi wake wa dini akapate ushauri wa kiroho, mfanyiwe sala na maombi kisha muwe na imani kwa Mungu ili muweze kuendelea mbele. Mfano kama wewe Sophia na hivyo kizazi kilishatoka basi hata raha ya maisha umekosa ila mrudie Mungu na utapata amani na furaha”
“Inamaana wewe unafanya mambo ya kiganga na maombi pia?”
“Tunatakiwa tuamini juu ya uwepo wa Mungu katika maisha yetu, yani kama unatembea na humuamini Mungu basi ujue wewe una matatizo kushinda hata huyo tunayemuita shetani. Wote tumeumbwa na Mungu na tunapaswa tumuamini katika maisha yetu.”
Sophia na Ibra wakawa kimya kwa muda huku kila mmoja akijitafakari kivyake kwani wao hawakuwa watu wa maombi wala ibada na wakashangaa mtu kama huyu anayetumia madawa ya kienyeji bado anawashauri wamuamini Mungu na wamrudie Mungu.
“Nawaambia kweli, laity kama mngekuwa ni watu wa ibada basi kwa hakika kuna mambo mngeyaepuka kabisa hata kwenye ile nyumba msingekaa hata wiki mngehama wenyewe na mngejiokoa na mambo mengi ila kwavile hamkuwa watu wa ibada ndiomana akili zetu zilimalizwa kwa urahisi sana”
Wakaafikiana na huyu bibi, wakakumbuka hata vile Jane alivyokuwa akiwashauri kuwa wafanye maombi jinsi gani walivyokuwa wakimponda ila kwasasa walibaki kujutia tu. Bibi aliwaruhusu kuondoka na kurudi makwao.

Safari ya kutoka pale kwa bibi ikawadia na sehemu ya kwanza ilikuwa kumuacha Siwema nyumbani kwake kisha na wao kurudi makwao, Ibra alirudi kwao na Sophia pia alirudi kwao na familia yake ambapo kama walivyoshauriwa na yule bibi waliamua kumtafuta mtu wa maombi aweze kusaidiana nao katika kuiombea familia yao ambapo alifika na kuwasaidia kwa maombi huku akiwasisitiza kuwa wasiache kufanya sala na katika maisha yao sala iwe ni kila kitu.
“Kwakweli tumejifunza vitu vingi sana, wengine hapa ilikuwa kitu kidogo tunakimbilia kwa mganga wakati kumbe tungetulia na kumshirikisha Mungu basi kila kitu kingeenda sawa ila tumejifumza sana”
Mama Sophia alikuwa akijilaumu yeye mwenyewe kwanza,
“Ila kosa ni langu la kutowafundisha wanangu maadili ya kumjua Mungu ndiomana yote haya yametokea ila tumepata fundisho sasa”
Wakaanza kujitahidi kufanya ibada kila siku na ikawasaidia kuishi na kulala kwa amani bila ya hofu wala tatizo lolote.

Baada ya muda kiliwekwa kikao cha familia mbili yani familia ya Ibra na familia ya Sophia ambapo Ibra alienda kumdai mkewe kuwa wakaanze maisha upya, kwa upande wa Sophia ilikuwa tofauti sana kwani alikataa katakata,
“Ibra, siwezi na sitaweza tena kwenda kuishi na wewe nisamehe tu kwa hilo ila sitaweza kabisa kabisa yaliyonikuta yanatosha”
“Kwani mimi niliyapanga hayo Sophia jamani?”
“Naweza sema uliyapanga ndio, kwanza fikiria kuwa ujinga ufanye wewe kwenye ujana wako huko halafu mateso nipate mimi yani sitaweza kuwa na mtoto sababu ya ujinga wako. Fikiria pia, kwanini hukuniambia toka mwanzo kiasi cha pesa ulichonunulia ile nyumba na kwanini hukuniambia kama kila kitu ulikikuta mule ndani labda akili yangu ingefunguka. Kwakweli Ibra sitaweza tena kuishi na wewe”
Wazee waliamua kumshauri Sophia na kumshawishi arudiane na mumewe ila Sophia alikataa katakata. Ikabidi kikao kihairishwe tu kwani hawakupata muafaka wa aina yeyote ile.
Kesho yake Ibra alienda tena nyumbani kwakina Sophia na kutimuliwa ila baada ya wiki alienda tena na kumuomba Sophia jambo moja tu.
“Jambo gani hilo?”
“Naomba twende mahali, halafu hapo ukaniache rasmi name sitalalamika tena”
Kwavile Sophia hakutaka usumbufu wa Ibra tena ikamlazimu akakubali tu kisha wakafunga safari na moja kwa moja Ibra alienda na Sophia mahali ambapo walianza wote maisha, Ibra akamwambia Sophia
“Unapakumbuka hapa?”
“Napakumbuka, si ndio tulipoanzia maisha! Ila kwangu hapana thamani tena laiti ningejua bora ningebaki hapa tu kuliko kule tulipohamia”
Kisha Ibra akaondoka pale na Sophia na kwenda nae kule walikohamia,
“Kwanini tumekuja huku tena?”
“Nilikuwa nakamilisha kuangalia mazingira yaliyofanya tuachane, pale kwa mwanzo tuliishi kwa amani sana ila huku ndio kumefanya tuachane. Na baada ya hapa sitakusumbua tena Sophia kwani najihisi nitakuwa chizi”
Ila kadri walivyosogea hawakuweza kuiona nyumba waliyokuwa wanaishi badala yake ulionekana uwanja mpana sana na ndani ya uwanja huo kulikuwa na maandishi yaliyosomeka kwa herufi kubwa ‘NYUMBA YA MAAJABU’ Sophia akashtuka sana na kuogopa kisha akamuangalia Ibra, muda huu Ibra akamwambia Sophia,
“Kwaheri Sophia maana kwa hakika sitaweza kupambana peke yangu, nilikutegemea wewe, nakupenda sana na sitaweza kuendelea kusema nina furaha wakati furaha sina. Mimi naenda kuingia pale kwenye kiwanja na nitakaa humo maisha yangu yote mpaka pale Mungu atakaponiita”
Ibra alimbusu Sophia kwenye paji la uso kisha kuanza hatua za kuelekea kwenye kiwanja kile ambapo kila aliposogea alianza kuiona nyumba waliyokuwa wakiishi ikijitokeza, Sophia hakuweza kustahimili Ibra arudi tena mule hivyo alimkimbilia na kumshika mkono kisha kusogea nae mbali kabisa, akamuangalia kwa uchungu na kumwambia,
“Nimekusamehe Ibra, nakupenda sana”
Wakakumbatiana huku wakilia kwa uchungu na kujikuta wakikumbuka yale yote waliyokuwa wakiyapitia.

---------------------------------------------MWISHO-------------------------------------------------------
Mwisho wa stori hii ya NYUMBA YA MAAJABU ndio mwanzo wa stori nyingine, nashukuru sana wadau wangu kwa moyo wenu wa upendo na uvumilivu. Kuna changamoto zilinipata hapo kati nikashindwa kuwaletea stori hii ila ni mapito tu.
Mwenye maoni, ushauri au pendekezo usisite kuniambia au kama una jambo binafsi njoo kwenye akaunti yangu binafsi ya Facebook (Atuganile Mwakalile) nitumie ujumbe na nitakujibu.
Asanteni sana, nawapenda sana.

No comments:

Post a Comment