Walifika kituoni saa mbili usiku na kuamua kwenda moja kwa moja kwa Siwema ambapo walipofika palikuwa kimya sana huku taa zikiwa zinawaka tu ikabidi wagonge mlango ili wamuombe ifadhi ya muda hadi kesho watakapoenda kuonana na yule bibi, waligonga kama mara tatu hivi ndipo Siwema alipotoka ndani ila alipofungua mlango tu alishangaa sana na kumuuliza Sophia,
“Huyo wa nyuma mmekuja nae wa nini?”
Sophia akageuka nyuma na kushtuka sana kwani alimuona Neema.
Alijikuta akitetemeka tu na kushindwa hata cha kuongea, ila mama Sophia na Tausi inaonyesha hawakuona chochote kwahiyo walikuwa wakishangaa tu. Siwema akamuuliza tena Sophia,
“Umekuja nae wa nini huyo?”
“Dada, hata mimi sijui”
Sophia akajisogeza zaidi kwa Siwema kwani hofu ilimshika sana, ila Siwema aliendelea kuongea,
“Kama mpo pamoja na huyo mtu kwakweli siwezi kuwapokea”
“Hapana hatupo nae, hata mimi nashangaa amefata nini hapa”
Mama Sophia ikabidi aulize,
“Kwani huyo mnayemuongelea ni nani na yuko wapi?”
Siwema akauliza,
“Kwani nyie hamumuoni au? Si huyo hapo anawachekea”
Wakati mama Sophia na Tausi wakijaribu kupepesa macho ili waweze kumuona mtu huyo, naye alitoweka kabisa kwani hata Siwema na Sophia hawakumuona tena, wakatazamana kisha Siwema akawakaribisha ndani nao wakaingia. Muda kidogo Siwema akawaomba wamruhusu awaandalie chakula kwanza.
“Mnajua mmekuja bila taarifa ila ngoja niwaandalie kidogo nilichonacho”
Wakatulia pale wakisubiria Siwema aandae, ambapo alikuwa na viazi na kuamua kuvichemsha ili waweze kula na kunywa chai.
Muda kidogo Siwema alimaliza na kuwaandalia kisha kuanza mazungumzo ya hapa na pale kuwa nini kimewasibu mpaka kufika usiku ule,
“Dada, ni makubwa sana yaliyotusibu”
“Kwanza nisamehe bure mdogo wangu, yani siku ile niliambiwa ole wangu niende kueleza yaliyotokea mule ndani kwenu itakuwa ni mwisho wangu basi nikaogopa sana kumuelezea mtu yeyote ila laity kama ningepata ujasiri wa kueleza basi huenda mngepata msaada”
“Usijali dada, kwanza hapa penyewe bado hakuna usalama kabisa. Hivi huwa unalala kwa amani kweli?”
“Siku hizi kabla ya kulala huwa nawasha ubani ili nisifatwe na viumbe wabaya na inanisaidia sana tu”
Mama Sophia akashangaa sana na kumuuliza Siwema kwa mshangao,
“Ubani?”
“Ndio ubani, kwani vipi?”
“Ubani si huwa unaita majini?”
“Unajua hivi vitu mama huwa vinaenda kwa imani, kwa mimi naamini kuwa kuna majini ila pia wapo wazuri na wabaya. Hata hivyo sina imani kama ubani unaita majini kwani ingekuwa ni kweli basi majini wangejaa sana maana ni watu wengi wanaowasha ubani. Kila mtu huwa anawasha kwa maana yake. Mbona ubani unachomwa Makanisani na Miskitini, kwanini mimimnisiweze kuchoma ndani mwangu?”
“Kwahiyo huwa ukichoma unafanyaje?”
“Nanuwia watu wabaya wasinifate wala nisitokewe na chochote kibaya”
“Mmmh leo umenipa mapya kabisa, mi huwa sina imani na ubani na siku zote huwa nahisi kazi yake ni kuita majini. Yani nikisikia mtu ananunua ubani jibu ninalopata ni kuwa mtu huyo ana majini”
“Si vizuri kumdhania mtu vibaya, kila mtu analindwa na imani yake.”
“Sawa nimekuelewa”
“Sawa mama, eeh Sophia niambie kwanza ulipomtoa mama na imekuwaje kuja usiku huu?”
Sophia aliamua kumueleza kwa kifupiu uhitaji wake wa kuonana na yule bibi ila kama kawaiada ya Siwema kuhusu yule bibi aliwaka sana muda huu na kudai tena kuwa yule bibi hafai na hatakiwi kabisa kuwa karibu naye,
“Hivi Sophia kwanini bado unaendelea kumng’ang’ania yule bibi?”
“Dada, hujui tu. Yule bibi amefungua akili yangu sana na pia naamini anaweza kunisaidia juu ya jambo hili tafadhali usinizuie kuonana nae”
“Mimi simuamini yule bibi yani simuamini kabisa, kuna stori mbaya sana kumuhusu hapa mtaani kwakweli hafai”
Ikabidi Sophia amueleze Siwema kuhusu kufa kwake hadi pale nduguze walipotaka kumzika na jinsi alivyorudishwa nyumbani nay ale mambo yaliyotokea kwenye kaburi alilotaka kuzikwa. Hii stori ilimsisimua sana Siwema na kumpa uoga wa hali ya juu hata akashangaa Sophia anaendelea wapi kupata ujasiri kwa mambo kama yale yaliyomtokea.
“Ujasiri huu ni kwasababu ya ile dawa niliyotafuna. Imenifungua akili sana na kunifanya nihitaji kufahamu kwa undani zaidi namna ya mimi kuepukana na hili tatizo”
“Pole sana mdogo wangu, kesho nitajitahidi ili tuweze kumpata”
Walizungumza sana kisha ukafika muda wa kulala, ambapo Siwema aliamua kutandika godoro pale sebleni kwao ili kupata nafasi kubwa zaidi ya kuweza kulala.
Wakati wamelala wakasikia mtu akigonga mlango, wa kwanza kushtuka alikuwa Tausi ambaye alimshtua dada yake kwa uoga,
“Dada, dada eti kuna mtu anagonga”
Muda huo huo Siwema nae akaamka na kusikia mlango ukigongwa, akataka kwenda kuinuka kufungua mlango ule, Sophia akamzuia Siwema
“Tafadhali usiende kufungua nakuomba”
“Kwanini wakati mtu anagonga”
“Je unamjua ni nani?”
“Atakuwa ni Tuma tu huyo, ndio zake kuchelewa kurudi sasa kwao wasipomfungulia ndio huja kwangu”
“Je huyo Tuma huwa anakuja muda huu?”
“Kwani saa ngapi saizi?”
“Saizi ni saa nane”
“Kheeee ishafika saa nane kumbe! Mara nyingi Tuma huwa anarudi saa sita, labda leo kachelewa tu”
“Hapana si yeye, tafadhali usiende kufungua”
Siwema aliweza kuona hofu kubwa aliyokuwa nayo Sophia na kumfanya asite kwenda kufungua, mama Sophia nae akashtuka na kusikia ile kugonga, huyu mama alijikuta akiinua mikono juu na kushika kichwa huku akisema
“Mungu wangu, hadi huku!”
Huyu mama machozi yalikuwa yalimlenga lenga, Siwema aliweza kuwaelewa sasa kwani akakumbuka hata vile alivyosimuliwa na Sophia muda mfupi kabla ya kulala.
Wakati ile hodi ikiendelea huku kila mmoja akiwa na hofu, Siwema akajikuta akibanwa na mkojo wa hali ya juu,
“Jamani mkojo umenibana sana, sina jinsi lazima nitoke nje nikakojoe jamani”
Sophia aliendelea kumsihi huku akimuomba akojolee hata ndoo ila asitoke nje,
“Kheee nikojolee ndoo yangu?”
“Kakojolee tu, kwani tatizo ni nini si kesho asubuhi itasafishwa”
Basi Siwema akaafikiana nao na kuchukua ndoo yake ya chooni kisha kwenda nayo chumbani kukojoa.
Wakati akitoa haja ndogo hiyo akasikia kama mtu akigonga dirisha lake kumbe Sophia naye alisikia na kumfanya ainuke na kukimbilia chumbani kwa Siwema ili kumzuia kuwa asifungue hata dirisha,
“Kheee Sophia mdogo wangu umeanza kuchanganyikiwa eeeh!”
“Kwa yaliyonipata nina haki ya kuchanganyikiwa dada yangu, nakuomba hata hilo dirisha usifungue”
Siwema alimsikiliza Sophia kwahiyo alimaliza na kurudi sebleni ambapo ile hodi ilidumu kwa muda wa nusu saa na kuwa kimya kabisa, mama Sophia akakumbuka kitu na kumwambia Siwema.
“Ila leo hujawasha ule ubani wako”
“Aaah bora umenikumbusha”
Siwema alinyanyuka na kusogelea jiko lake la mkaa huku akiangalia kama kuna moto ulibaki, akaona vimoto akachukua na kuwasha ubani wake kisha akarudi na kuwaambia,
“Tulale sasa”
Wote waliweza kuendelea kulala kasoro Sophia hakuweza kabisa kuendelea kulala hadi panakucha.
Asubuhi na mapema Sophia alifungua malango wa Siwema na kutoka nje, macho yake yaliangalia ule mpera wa Siwema moja kwa moja huku akijiambia,
“Laiti kama ningekuwa na ufahamu ile siku ya kwanza kabisa basi sasa hivi ningekuwa na mtoto wangu”
Akainamisha macho chini kisha akainua tena na kwenda kuufata ule mpera, alipofika alikaa chini yake huku akiendelea kutafakari na kukumbuka siku ya kwanza alipokuwa akitafuta pera kwenye mti huo wakati mimba yake ikiwa change kabisa. Sophia akaangalia tumbo lake na kujishika huku akisikitika na kusema tena,
“Laiti ningejua, ningekuwa na mtoto wangu sasa. Hivi kwanini sikumsikiliza yule bibi? Kwanini niliyapuuzia maneno yake? Kweli usilolijua sawa na usiku wa giza”
Sophia alikuwa akihisi kuwa huenda yule bibi atatokea tena kama kawaida yake ila huyu bibi hakutokea wala nini.
Wakina Siwema nao walivyoamka walishangaa kutokumuona Sophia, ikabidi Siwema atoke nje na kumuona Sophia akiwa chini ya mpera ametulia tu, Siwema alimsikitikia sana Sophia kisha akamuita ambapo Sophia aliinuka pale na kwenda alipo Siwema.
“Sophia mdogo wangu usifanye mawazo yakutawale kiasi hiko, jiandaeni na ndugu zake nioweze kuwapeleka kwa yule bibi kwani nina hakika tukiulizia tutafika nyumbani kwake tu”
Sophia alikubali na kwenda kujiandaa yeye pamoja na ndugu zake kwa lengo la kwenda kuonana na yule bibi. Mama Sophia alimuuliza mwanae kwa uhakika wa mwisho,
“Unaamini kuwa huyo bibi anaweza kukusaidia?”
“Naamini hilo mama kwani yule bibi anaonekana kujua vitu vingi sana vya kwenye nyumba niliyokuwa nikiishi kwahiyo naamini anaweza kunisaidia”
“Sawa mwanangu, unajua kama ningezoea kwenda kwa waganga wa kienyeji basi ningekupeleka mapema sana ila mimi huwa sina imani na waganga wa kienyeji. Na kwa maelezo yako nahisi kama huyo bibi ana uganga uganga flani hivi”
“Mfano kama ni mganga itakuwaje?”
“Ni juu yako ila mimi sina imani na waganga mwanangu, ni afadhali wale wazee wa jadi. Ila kwavile ni wao waliosema twende tukaonane na huyo bibi basi hakuna tatizo”
Walimaliza kujiandaa kisha kutoka pale nyumbani kwa Siwema na kuanza msako wa kumtafuta yule bibi huku wakisaidiwa na Siwema.
Kila walipopita na kuulizia walipewa majibu ambayo hayakuwaridhisha na pia majibu yalikuwa yakiwakatisha tamaa na kuona kwamba inawezekana wasiweze kuonana na yule bibi,
“Kwakweli yule bibi huwa namuona tu na hata sijui anapoishi, wengi huwa wanasema anaishi mtaa wa pili huko ila kila unayemuuliza naye atakwambia kuwa ameambiwa”
Siwema akamuuliza tena huyu mtu,
“Vipi kuhusu swala la uchawi la yule bibi?”
“Kama ilivyo kuishi kwake ndivyo ilivyo swala la uchawi, wengi utawasikia kuwa yule bibi ni mchawi sana ni mtu mbaya hafai kabisa ila ukimuuliza kuhusu uchawi wa yule bibi atakwambia kuwa ameambiwa na watu. Kwahiyo hakuna mtu yeyote mwenye uhakika na maisha ya yule bibi”
Siwema akapumua kidogo kisha kumshukuru huyu mtu na kuendelea na safari hadi walipoingia mtaa huo wa pili ambapo anahisiwa kuishi huyo bibi, wakati wanatembea na kuulizia huku kila mmoja akidai kutokufahamu anapoishi yule bibi huku wengine wakidai anaishi mtaa waliotoka wao wakajikuta wamesimama kwa muda kwanza na kukosa uelekeo, wakati wamesimama hapo Sophia akahisi kang’atwa na kitu na kushtuka sana, akafanya wote wageuke na kuangalia kuwa ni nini wakaona nyoka akikimbia,
“Mungu wangu ni nyoka!”
“Tutafanyaje sasa?”
Siwema akachukua kitambaa na kumfunga Sophia mguuni huku akisema watafute usafiri wamuwahishe hospitali, na kwa bahati nzuri kuna gari ilikuwa inapita pale mtaani wakaamua kusimamisha gari hiyo ila kabla hawajapanda wakamuona yule bibi kwa mbali akiwaangalia. Sophia akasita kupanda na kuwaomba wakazungumze na yule bibi kwanza,
“Sophia, sumu ya nyoka ni kali sana, tafadhali tuwahi hospitali kwanza halafu tutarudi kuzungumza na huyo bibi”
“Hapana jamani, najua vizuri kama nyoka ana sumu kali ila nina uhakika yule bibi ana dawa ya kuweza kuniondoa hii sumu ya nyoka”
Ikabidi wamwambie yule dereva aondoke kisha wao wakaanza kumfata yule bibi huku wakimsaidia Sophia kutembea kwani alikuwa akichechemea.
Walipofika tu karibia na yule bibi, kuna majani alichuma na kuyafikicha kisha akampaka Sophia machoni na muda huo huo yale maumivu ya kung’atwa yakapotea na Sophia akaanza kutembea kawida kisha yule bibi akamwambia Sophia,
“Si nyoka aliyekung’ata”
“Ni kitu gani bibi?”
“Ni mauzauza tu, hawakutaka uonane na mimi. Hujiulizi kuwa lile gari la haraka haraka vile limetokea wapi? Wanataka kuwarudisha nyuma ila kwasasa ni kusonga mbele tu.”
Huyu bibi alimuangalia mama Sophia na kumuangalia Siwema kisha akawaambia,
“Mimi si mchawi wala si mganga wa kienyeji kama mnavyofikiria ila mtaelewa mimi ni nani na kwanini wengi hunichukulia kama mchawi”
Kisha wakaendelea kusonga mbele kuelekea nyumbani kwa yule bibi, huyu bibi akamuuliza Sophia,
“Yuko wapi mumeo?”
“Hata sijui alipo bibi”
“Je, unahisi kuwa bado yupo kwenye nyumba yenu?”
“Sijui bibi, yani mimi na yeye tumeachana kwenye mazingira ya kutatanisha sana”
“Pole sana ila angalia nyuma kwanza”
Sophia akageuka nyuma na kumuona Ibra, kwakweli alishtuka sana.
Itaendelea kama kawaida……..!!!!!!
Toa maoni yako mdau.
No comments:
Post a Comment