Mdogo wa Sophia aitwaye Tausi akaamua kufunua pazia la dirishani ili achungulie ni nani, ila alipofunua tu alipiga kelele za uogo na kuanguka chini.
Mule ndani wakazidi kupatwa uoga huku kaka wa Sophia akisisitiza kuwa atoke nje na kujua ni nini kinaendelea,“Kaka tafadhali, naomba unisikilize dada yako. Jamani familia yangu mimi nimepitia mengi sana nawaombe msadiki ninayoongea sasa, kwanza kabisa msitoke nje subirini pakuche nina maana yangu kabisa”
“Maana yako ni ipi Sophy?”
“Ingekuwa ni enzi zile ambazo sikuwa na ufahamu basi ningekuwa wa kwanza kushauri kuwa tutoke ila baada ya kula kijiti cha yule bibi zaidi ya mara mbili akili yangu iko vizuri sana, nawaomba tusitoke niliyopitia yanatosha na sitaweza kuwaeleza kwasasa kwasababu maalum ila nitawaeleza tu sema si kwa muda huu ambapo kuna mauza uza nje”
“Haya sasa na huyu mdogo wako tutafanya nae nini?”
“Msijali atazinduka tu ila nje tusitoke”
Wakatulia kimya kwanza kwa muda kwani hakuna aliyeweza kumuelewa Sophia kwa haraka, ule ukimya wao ukafanya wasikie kwa zaidi masufuria yakisuguliwa nje, mmoja akauliza muda kwanza
“Hivi kwani ni saa ngapi saa hizi?”
“Saa nane usiku”
“Mmmh makubwa haya, saa nane mtu tusiyemjua asugue sufuria nje kwetu kweli!”
Wakati wakitafakari hayo wakasikia mtu akigonga mlango wao na kufanya waogope zaidi, mama Sophia alishindwa hata kujisogeza kwa uoga ila Sophia alizidi kuwapa ujasiri ndugu zake kuwa wasiogope na wala wasijishughulishe kufungua mlango,
“Yani msiogope chochote ndugu zangu, na kwavile zilianza mbwembwe za kusugua sufuria na sasa ni mtu anagonga mlango hata msiwe na uoga kwanza. Tutulie tu na wala tusiende kufungua kwani hakuna miadi na mtu yeyote kuwa atakuja usiku huu.”
Ikabidi wamsikilize Sophia tu na kutulia pale pale sebleni huku muda ukizidi kwenda na yule mtu akizidi kugonga, ila ilipofika saa kumi alfajiri yule aliyekuwa akigonga aliacha kugonga na kukawa kimya kabisa, muda kidogo yule mdogo wa Sophia naye aliweza kuzinduka na kukaa huku akiangalia huku na kule.
Mama yake aliyekuwa karibu naye aliendelea kumsogelea mwanae na kumtuliza, kisha wakamuuliza alichokiona dirishani wakati amefungua pazia,
“Mmmh mama eti niliona mbuzi ndio anasugua sufuria, nimeogopa sana sijui ni uchawi loh!”
“Pole sana mwanangu, ndiomana dada yako alitukataza kuangalia nje ila usijali kila kitu kitakuwa sawa”
Walitulia kimya pale huku kila mmoja akijaribu kufikiria kuwa huyo mbuzi alikuwa anasuguaje hizo sufuria.
Kulipokucha waliweza sasa kutoka nje na kuendelea na shughuli zingine kama kawaida huku wakipanga kwenda kwa wale wazee wa mtaa huo kuwaeleza kile ambacho wamekikuta makaburini na vile ilivyokuwa usiku kwenye nyumba yao.
Kaka wa Sophia walitoka pale na kwenda kwa wazee, kisha wanawake waliendelea na shughuli za hapa na pale huku wengine wakienda kulala ukizingatia usiku hawakuweza hata kusinzia.
Muda kidogo kaka wa Sophia walirudi na wazee watatu wa mtaa ambao walifika hapo ili kuelewa zaidi kutoka kwa Sophia, walikaa na Sophia na kuzungumza nae sasa
“Kwanza kabisa ningependa tujue kabla ya sisi kuletewa taarifa ya msiba wako huku ulikuwa wapi? Na vipi uliweza kufika hapa siku yako ya mazishi?”
Sophia aliamua kuwaeleza toka mahali pale ambapo yeye na mumewe walikutwa kisha yeye kusaidiwa na watu na aliyoyakuta kwa watu hao,
“Mmmh inamaana hawakuwa watu wa kawaida?”
“Kwa mujibu wa yule mwenzao ndio hivyo hawakuwa watu wa kawaida”
“Mmmh habari yako kidogo inanichanganya akili kutokana na hayo mambo halafu na kile mlichoenda kukikuta makaburini jana na jinsi mlivyotueleza yaliyotokea hapa kwenu usiku. Sasa najaribu kutafakari kwanza, ngoja nikuulize, kwanini jana ulihisi kuwa huenda ni kitu kibaya na kuwakataza wenzako kutoka nje?”
Sophia aliwaeleza kwanza kuhusu bibi aliyewahi kukutana nae na kupewa dawa ambayo aliambiwa kuwa itamsaidia kurudisha akili yake na imemuwezesha kugundua kwa urahisi kabisa kitu kizuri na kibaya kikitaka kutokea.
“Je unamfahamu huyo bibi?”
“Nikimuona namfahamu ila sijui anapoishi kwani mara nyingi huwa ananikuta nyumbani kwa rafiki yangu ila nahisi rafiki yangu anajua anapoishi huyo bibi”
“Itakuwa ni vyema kwenda kuonana na huyo bibi, nadhani anaweza kutusaidia juu ya hili pia. Hivyobasi jipangeni mpate siku nzuri ya kuonana na huyo bibi”
Kwavile mama Sophia naye alikuwepo hapo akawaomba sana kuwa inawezekana kwahiyo hata kesho waweze kwenda huko kuonana na huyo bibi.
“Basi itakuwa vizuri sana, ngoja na sisi tukajaribu kupita huko makaburini na kuona kitu kilichoendelea”
Hawa wazee wakaaga kisha wakaondoka na kaka zake Sophia kuelekea huko makaburini ili kuona kama walichoelezwa kina ukweli wowote au ni nini.
Walianza kufika karibia na eneo la makaburi na kusikia kuna harufu ya mapishi inaendelea, ikafanya wajiulize
“Ni harufu gani ya mapishi itoke huko kwenye nyumba za watu mpaka huku kwenye eneo la makaburi?”
Hakuna aliyekuwa na jibu ila walipofika makaburini walishangaa sana, wakaona lile kaburi walilopanga kumzika Sophia likiwa limeota nyasi kwa juu kisha yule mbuzi waliyemzika pembeni alikuwa juu ya kaburi hilo akila zile nyasi, kisha yule mbuzi akawaangalia na kutabasamu hapo ndipo amani ya moyo ilipowatoweka kabisa na kujikuta kila mmoja akikimbia kwa nija yake na sehemu ya kwanza kufika ilikuwa ni kwakina Sophia tena mahali hapo hata wale wazee hawakukaa tena wakaondoka na kuwaacha tu wakaka wa Sophia huku pale nyumbani wakishangaa kuwa wamekumbwa na kitu gani, kaka wa Sophia alieleza kwa kifupi tu
“Ni bora tuliyokutana nayo jana kuliko leo”
“Kivipi jamani, hebu tuambie”
“Ushawahi kuona mbuzi anatabasamu?”
“Mbuzi anatabasamu? Kivipi mbona ni habari ya ajabu sana!”
“Ndio hivyo mama yani mimi hadi nashangaa na ninaanza kuwa na mashaka na uwepo wa Sophia jamani sijui kama na yeye ni mtu”
Sophia alijisikia vibaya kwa hilo kwani hakutegemea kama ndugu zake wanaweza kuwa wanamfikiria vibaya kiasi kile cha kusema kuwa hata yeye wana mashaka nae, alitamani kesho yake ifike tu ili aweze kwenda kwa yule bibi na kuzungumza nae kwa undani zaidi akihisi kuwa huenda anaweza akapata amani ya moyo pamoja na familia yake. Hakutaka kupoteza muda kwa kubishana na watu wa familia yake kwahiyo muda huo aliamua kwenda kupumzika ukizingatia hakupumzika kabisa.
Usiku ulifika huku Sophia na wote kwenye familia yao walikuwa wamelala, muda huu Sophia akajiwa na ndoto na kwenye ndoto hii alijiona yupo kwenye ile nyumba yake na mumewe, muda kidogo akamuona Neema aliyekuwa akimuangalia na kumuuliza,
“Hivi kwanini nakuja kwenu na kukonga mlango hunifungulii? Kwa madai yako unaogopa makosa mliyofanya ya kuniokota?”
Sophia alikuwa kimya tu akimtazama huyu Neema, kisha huyu Neema akamwambia tena Sophia,
“Wewe ulitakiwa uwe kwenye hali niliyokuwa nayo mimi kwasasa ila nakushangaa sana, hebu niruhusu tuondoke pamoja ili uweze kuepukana na haya yanayokupata pia ukapate pumziko la moyo”
Hapa sasa Sophia akapata ujasiri wa kumjibu,
“Sina haja ya kwenda na wewe Neema”
“Sasa unafikiri unafaida gani kwenye maisha ikiwa huna kizazi? Unadhani mumeo atakupenda tena bila kizazi? Na kwanini hujawaambia kwenu kuhusu mumeo na maovu yake yanavyokutesa?”
“Sitakuwa binadamu wa kwanza kukosa kizazi, kwahiyo bado nina nafasi kubwa ya kuendelea kuishi kwanza kunitoa kizazi wala sio kikwazo kwangu”
“Basi tuachane na hayo Sophia, kwa usalama wako na usalama wa familia yako nifungulie mlango niingie ndani kwenu”
Sophia akashtuka kutoka kwenye ule usingizi, na gafla akasikia mlango wao ukigongwa tena kama jana usiku huku ndugu wote wa Sophia wakiwa wameamka na kujiuliza kama wafungue ule mlango au la. Sophia alisogea kwa haraka sana na kuwaomba ndugu zake,
“Tafadhali msifungue”
Mara gafla akasikia sauti kutoka nje,
“Sophia acha roho mbaya hebu nifungulie bhana”
Wote walishtuka mule ndani kwani ile sauti ilikuwa ni ngeni masikioni mwao ila ilikuwa ni sauti iliyozoeleka kwenye masikio ya Sophia, ingawa Sophia alikuwa akitetemeka ila alipata ujasiri wa kuongea kwa nguvu,
“Sikufungulii, ondoka kwetu shetani wewe”
Kikasikika kicheko kikubwa sana, kisha sauti ikasema,
“Unajua kabisa kuondoka ni maamuzi yangu Sophia, naomba unifungulie kwa amani tu kabla sijafanya chochote kibaya. Nifungulie Sophia”
“Nimesema Sifungui”
“Unajua wazi kitu ambacho naweza kufanya, unajua wazi nilivyo na roho mbaya. Sasa kwa amani yako fungua Sophia”
Ndugu wa Sophia walikuwa wakitetemeka sana huku wakimuangalia ndugu yao na kungoja atakachosema huku wengine wakijaribu kumshawishi Sophia akubali kufungua ila Sophia alitulia na wazo lake lile lile la kuto kufungua, ile sauti ya nje sasa iliongea kwa ukali zaidi,
“Nakupa sekunde kumi Sophia usipofungua kijiji kizima kitasimulia nitakachokifanya”
Sophia alikaa kimya kwa muda huku akitetemeka kwani hakujua cha kufanya kisha akajikuta akikunja mikono yake huku akisema,
“Asante Mungu, asante Mungu”
Alikuwa akirudia hayo maneno huku mule ndani kwao wote wakimshangaa Sophia kwani hakuna aliyewahi kumuona Sophia akiwa vile hata mara moja, Sophia alikazana kumshukuru Mungu kwani bado alikuwa na maneno ya yule bibi kuwa amshukuru mungu hata kwa jambo ambalo halijafanyika huku akiamini kuwa Mungu anaenda kufanya jambo hilo.
Na ukapita muda mrefu huku kimya kikitawala pale nyumbani kwao, haikusikika sauti ya kugongwa kwa mlango na wala sauti ya yule mtu wan je, ila hata hivyo hakuna aliyeweza kulala pale nyumbani kwakina Sophia kwani kila mmoja bado alikuwa na uoga katika moyo wake.
Kulipokucha kila mmoja alikuwa akimwambia Sophia kwenda kwa huyo bibi ili waweze kuepukana na hayo yanayotaka kuendelea hapo nyumbani kwao, kisha Sophia aliamua kuwapa ushauri ndugu zake wa kugawanyika kutokana na usalama wao kuwa waondoke waote hapo nyumbani na nyumba ifungwe kwa muda kwani inawezekana huyo kiumbe akienda kupambana na Sophia alipo na kushindwa akarudi tena kwenye familia yake.
“Jamani mimi nawaomba ndugu zangu, nawaomba sana. Dada zangu mrudi kwa waume zenu na kaka zangu mrudi kwenu au hata muende kwa ndugu kisha mimi nitaondoka hapa na mama pamoja na Tausi ila nyumba tutaifunga mpaka pale tutakaporudi kwani inatakiwa tuepuke mabalaa haya, huyu kiumbe anaweza akaja hapa wakati hatupo na kufanya uharibifu zaidi ingawa shida yake kubwa ni mimi kwahiyo cha msingi ni kutengana wote humu ndani.”
Wakakubaliana hivyo kisha kila mmoja kuanza kujiandaa kwaajili ya kuondoka, mpaka kufikia saa kumi jioni karibia kila mmoja alikuwa ameondoka kisha wakina Sophia wakafunga milango na wao kuondoka wakiwa na funguo ili asije yeyote akarudi kabla ya muda ambao wamekubaliana.
Sophia akiwa na mama yake huku akiambatana na mdogo wake Tausi pamoja na kaka yao aliyekuwa akiwasindikiza, walifika mahali na kuweza kupanda mabasi ambayo yangewapeleka mjini ili waweze kufika mahali anapoishi Siwema. Kisha kaka yao naye akaondoka zake na kuelekea nyumbani kwake na yeye kwenye mke na watoto wake.
Wakiwa kwenye lile basi lilifika mahali na kuharibika kisha wakaanza kusubiri litengenezwe,
“Mmmh tutafika usiku”
“Sio tatizo kufika usiku, cha msingi tufike salama”
Muda kidogo ilionekana gari ya kukodi ikipita kisha ikasimama karibu yao kisha wakamsikia dereva akisema,
“Buku buku mpaka mjini”
Tausi akamtazama dada yake na kumwambia,
“Dada tungeenda kupanda hiyo tax si unaona anatangaza buku buku yani bei sawa na hili basi tulilopanda”
“Kuwa makini mdogo wangu, kwanini bei ya hiyo tax tuisikie sisi tu ilihali hapa kuna abiria wengi tu? Acha iende tu”
Tausi hakuwa na hoja ya ziada ikabidi tu akubaliane na dada yake kisha wakasubiri mpaka lile basi lilipokuwa sawa na kupanda kisha kuendelea na safari yao.
Walifika kituoni saa mbili usiku na kuamua kwenda moja kwa moja kwa Siwema ambapo walipofika palikuwa kimya sana huku taa zikiwa zinawaka tu ikabidi wagonge mlango ili wamuombe ifadhi ya muda hadi kesho watakapoenda kuonana na yule bibi, waligonga kama mara tatu hivi ndipo Siwema alipotoka ndani ila alipofungua mlango tu alishangaa sana na kumuuliza Sophia,
“Huyo wa nyuma mmekuja nae wa nini?”
Sophia akageuka nyuma na kushtuka sana kwani alimuona Neema.
Itaendelea kama kawaida……..!!!!!!
Toa maoni yako mdau.
No comments:
Post a Comment