Friday, 7 April 2017

NYUMBA YA MAAJABU: 43

Ibra akaingia wodini na kumfata mkewe alipolala kisha akamshtua kuwa waondoke,
“Siendi popote Ibra”
“Kwanini? Tatizo ni nini tena?”
“Akili yangu imefunguka”
“Unaongelea nini Sophy?”
“Umekula tena chakula Ibra”
Ibra akashangaa na kumuuliza mkewe,
“Umejuaje?”
Sophia akafunua mkono wake na kumfanya Ibra ashangae kuona alichokishika Sophia.
Ibra akamuuliza Sophia,
“Umekipata wapi hiko?”
“Nilikitunza, siku zile sikukikata chote kukitafuna na hiki nilichoacha ni kwa matumizi mengine”
“Kwahiyo umekitafuna?”
“Ndio na nikakuona uliyokuwa unayafanya nyumbani”
Ibra alikiangalia kwa makini kile kijiti kwani kilikuwa ni kile ambacho mkewe alipewa na Yule bibi, kisha Ibra akamuuliza tena mkewe
“Eeeh kimekusaidia nini sasa?”
“Sikia Ibra, siku ile kuna masharti kidogo tulikosea ingawa vingi tuliviona. Tulisahau kusema asante Mungu”
“Kwani asante Mungu inamsaada gani na hiko kijiti?”
“Yule bibi aliniambia ni vyema kumshukuru Mungu kabla ya mambo yote huku ukiamini kuwa atatenda”
“Kheee umekuwa mlokole?”
“Hapana ila akili zangu zimefunguka”
Ibra akatulia kimya kwa muda kisha akamwambia mkewe,
“Unajua Sophy sikuelewi!”
“na huwezi kunielewa maana akili zako zimevurugika, hivi Ibra unawezaje kula chakula ambacho humjui hata muandaaji?”
“Kwani tunapokula hotelini huwa tunamjua muandaaji?”
“Je pale nyumbani ni hotelini? Yani ndani uko peke yako, unakuta chakula kimeandaliwa unakula je ni nani ameandaa?”
“Huwezi ukanielewa ila nadhani na wewe ungetafuna kidogo hiki kijiti ila kabla ya kutafuna useme asante Mungu”
Ibra alichukua kipande kidogo alichopewa na mkewe na kusema asante Mungu kisha akatafuna kile kijiti na muda ule ule alihisi kizunguzungu na kuangukia kwenye kitanda alicholazwa mkewe ambapo Sophia alijisogeza kidogo na kumuacha pembeni.

Muda kidogo Lazaro nae aliingia kwenye wodi aliyolazwa Sophia na kumkuta pale mwenzie akiwa ameanguka pembeni,
“Vipi tena na huyu shemeji?”
“Mwache akili zake zikae sawa”
“Duh! Cha kushukuru hapa wodi zao hazina wagonjwa wengi maana sijui ingekuwaje”
Lazaro akajitahidi kumuhamisha Ibra kwenye kitanda cha jirani maana wodi ile ilikuwa ni ya kulala wagonjwa wawili.
“Ila shemeji kuna tatizo”
“Tatizo gani tena?”
“Ni Yule kiumbe ambaye mumeo ameongozana nae kama dereva, si binadamu wa kawaida Yule”
“Nimetambua hilo shemeji na ndiomana nimemgomea kuondoka. Kwanza nashukuru sana kwa ujio wako kwani ulinifumbua macho sana”
“Unajua nilivyoambiwa tu kuwa umelazwa nikashtuka sana na kuamua kuja halafu kitendo cha kumuona Ibra kama kachanganyikiwa kilinishtua ukizingatia nilivyomuona nje hapo nilimuita lakini hakuniitikia. Ndiomana nilipoingia tu nilikwambia moja kwa moja kuwa mumeo hayupo sawa”
“Na kitendo cha wewe kuniambia vile kimenifungua sana ndiomana alipokuja ili tuondoke nikamgomea. Hebu angalia mida ni usiku tayari halafu tungeenda wapi? Kwakweli bora ulikuja shemeji”
“Sawa, basi mi naenda. Nitakuja kukucheki tena kesho”
Lazaro akaaga pale na kuondoka zake, Sophia nae alitulia kwa muda ila nesi alipokuja na kumshangaa Ibra pale Sophia alimuomba nesi asimuamshe mumewe amuache kwanza apumzike ila kwavile wote waliishuhudia akili ya Ibra ikabidi wasikilize anachokisema mkewe.

Kulipokucha Ibra alishtuka na kujishangaa sana kujiona pale hospitali, kisha akainuka na kwenda pembeni ya mkewe na kumshtua ambapo mkewe aliamka na kumsalimia,
“Sophy imekuwaje nimelala hospitali? Wameweza kuniruhusu kweli?”
“Hospitali hii wana roho nzuri sana mume wangu, walikuona tokea mwanzo kuwa una matatizo ndiomana wakaruhusu tu ulale. Eeeh niambie”
“Nimeona mambo ya ajabu sana kwenye ndoto”
“Kama yapi?”
“Kwanza kabisa ni kuhusu Yule dereva bhana kumbe hakuwa dereva wa kawaida na mpango wake ulikuwa ni kututeketeza”
“Duh! Akili imekufunguka sasa mume wangu. Asante Mungu, eeeh baada ya kuona hayo?”
“Ila je unajua huyo dereva alikuwa ni nani?”
“Mmmh kama ni Yule mtu usimtaje tafadhari, nionee huruma nina matatizo ya miguu sitaweza kukimbia mimi”
“Pole mke wangu simtaji”
Kisha Ibra akamuomba mkewe ruhusa ya kwenda kutafuta chai,
“Nakuruhusu ila tafadhari usifanye ujinga kama wa jana”
“Siwezi kurudia tena makosa mke wangu”
Ibra alipotoka Lazaro naye aliwasili akiwa ameambatana na mkewe huku amebeba chakula cha asubuhi kwaajili ya mgonjwa na rafiki yake Ibra ila walimkuta Sophia akiwa mwenyewe, wakamsalimia pale na kumuuliza kuhusu Ibra,
“Ametoka, kasema anaenda kutafuta chai”
“Dah angejua angetusubiria sie tu, hivi shemeji ngoja nikuulize”
“Uliza tu”
“Hivi ndugu zenu wanajua kama upo hospitali?”
“Mmmh sidhani, ila labda Ibra kawataarifu”
“Kwani wewe huna namba zao hapo tuwataarifu?”
“Mimi sikumbuki namba kichwani ila nilipopata ajali simu nayo ilipotelea huko huko sababu sikuwa na fahamu yoyote ile”
“Pole sana”
Mke wa Lazaro alimsaidia Sophia pale kunywa chai kisha na yeye akaanza kuzungumza naye.
“Ila hivi unajua kwamba kuna roho inawafatilia?”
“Roho kivipi?”
“Kuna roho chafu sana inawafatilia na sijui ni kwanini ila nadhani ni kwavile hamjasimama kwenye imani”
“Mmmh sasa mnataka tusimameje jamani?”
“Inatakiwa nikufundishe kwa urefu zaidi, ukiwa sawa nitakufundisha ila kwasasa ngoja tukuache upumzike kwanza kwani hata madaktari hawataweza kuturuhusu zaidi”
Kisha Lazaro na mkewe wakaondoka huku Sophia akiwa amejawa na mawazo juu ya hiyo roho inayowafatilia.

Ibra alipomaliza kunywa chai, akabeba vitafunwa kwenye mfuko ili akampelekee mke wake nae apate kifungua kinywa ila alipokuwa pale nje ya hospitali gafla akamuona mtu mwenye muonekano kama dereva aliyeenda nae jana kwa lengo la kumchukua mkewe, Ibra alimsogelea mtu huyo na kumshika bega ambapo mtu Yule aligeuka na alikuwa ni Yule Yule dereva,
“Hivi unajua kama nimeshakutambua?”
“Kunitambua kivipi?”
“Unadhani ukijiweka kwenye maumbo tofauti sitakujua?”
Huyu dereva alikuwa akimshangaa tu ibra na kwavile Ibra hakupata ushirikiano kutoka kwa huyu dereva aliamua kumkaba mpaka watu walipokuja kuingilia kati,
“Kaka vipi mbona unamkaba mtu bila makosa?”
“huyo sio mtu ni shetani”
Watu wakawa wanamshangaa Ibra,
“Shetani kivipi kwani kakufanyia nini tena jamani?”
“Nawaambia huyo sio mtu, kama hamniamini ngijeni muone kitakachotokea”
“Hebu acha masikhara bhana, huyu tupo nae kila siku hapa, haya sasa huo ushetani kauanza lini?”
Gafla Yule mkaka aliyekuwa amekabwa na Ibra mwanzo akaanza kutapika damu tena zilimtoka mfululizo na kufanya wenzie wamuingize pale hospitali na kumkimbizia kwa daktari, Ibra alikuwa akishangaa tu yale matukio na kujiuliza,
“inamaana shetani nae huwa anaumwa jamani?”
Ila akawasikia wale vijana wa pale kijiweni wakimwambia,
“Gharama zote za kumuhudumia huyu mtu utazitoa wewe maana ndio umemsababishia matatizo yote hadi kutapika damu sababu ya kumkaba kwako”
Ibra hakutaka kubishana nao sana, kisha akaingia hospitali nay eye akiwa hana hata vitafunwa kwani alishaviangusha wakati wa kumkaba Yule kijana.

Ibra alienda moja kwa moja alipolazwa mkewe huku akimuomba msamaha kwakutomletea vitafunwa,
“Usijali lakini nimeshakunywa chai”
“Umepata wapi?”
“Lazaro na mkewe walikuja kuniona na ndio walioniletea”
“Dah afadhali ila mimi nimepatwa na majanga bhana”
“Majanga gani tena?”
Ibra akamsimulia mkewe alivyomuona Yule mtu na jinsi alivyomkaba na yaloiyoendelea,
“Mmh mume wangu hivi una uhakika kuwa huyo mtu ndio Yule Yule dereva wa jana?”
“Nina uhakika ndio ni yeye, nilimuona vizuri na nilikariri sura yake”
“Sasa na hao wanosema huwa yupo hapo siku zote wana maana gani?”
“Hata nimeshindwa kuwaelewa”
Muda kidogo wakaletewa mgonjwa mwingine mule wodini ambaye alikuwa ni Yule kijana kwakweli ibra lishtuka sana na kujiuliza kwanini wamempeleka wodi hiyo hiyo, inamaana wodi zingimne zimejaa? Akashindwa kujizuia na kumuuliza nesi,
“Hivi kwani wodi zingine zimejaa? Kwanini huyu mmemleta humu?”
“Kaka samahani sana hayo matatizo yako ya akili sijui wanayajua hao wengine. Mimi siyajui na wala sitaki kuyajua, huwezi kutupangia cha kufanya. Hii sio hospitali yako”
Nesi akaweka sawa pale kitandani na kumsaidia Yule mgonjwa kupanda pale kitandani, Sophia akamuuliza mumewe kama mtu mwenyewe ndio Yule,
“Ndio ni huyo huyo”
“Mmmh mbona naanza kupatwa na mashaka Ibra?”
Yule nesi alipomaliza kumlaza Yule mgonjwa katoka kidogo kisha akarudi tena ndani na kumuangalia Ibra halafu akamwambia,
“Muda wa kuangalia wagonjwa umeisha kwahiyo naomba uende kaka. Nadhani umenisikia”
Kisha Yule nesi akatoka tena na kusonya, hata Sophia alimshangaa sana nesi huyu,
“Kwani vipi huyu nesi anamatatizo gani jamani au anakutaka mume wangu?”
“Hata mimi nimeshindwa kumuelewa kabisa”
“Kama anakutaka aseme ila sio kukusakama hivyo”
Muda kidogo Yule nesi akarudi akiwa ameambatana na askari,
“Nitolee huyo hapo maana muda wa kuangalia wagonjwa umeisha ila yeye anang’ang’ania kutoka hataki”
Yule askari akamuomba Ibra kwa ustaarabu kabisa kuwa atoke kabla hajafanya shurti lolote ikabidi Ibra aamue kutoka tu kwani heri nusu shari kuliko shari kamili.

Sasa wodini alibaki Sophia na Yule mgonjwa ambapo Sophia aliamua kumuuliza maswali Yule mgonjwa ili kujiridhisha,
“Kaka samahani, unaitwa nani kwani?”
“Nimezoeleka kwa jina la bonge”
“Bonge!! Ila mbona wewe ni kimbaumbau na sio bonge?”
“Ndio, huwa wananiita hivyo sababu ya wembamba wangu”
“Sawa, jina lako halisi je?”
“Naitwa Samson”
“Aaah, eeh imekuwaje?”
“si huyo jamaa sijui ndio mumeo kaja kanikaba balaa yani kama ningemchukulia hatua basi angekuwa polisi kutoa maelezo saizi. Halafu cha kushangaza nikaanza kutapika damu”
“Dah! Pole sana, na je ni kweli jana alikukodi wewe?”
“Anikodi mie saa ngapi? Kwanza jana sikuwa maeneo haya kabisa, kuna jirani yetu alifiwa na jana tulikuwa kuzika hata sikuja huku siku nzima yani nimeshangaa kweli kuja kunishutumu mimi”
“Pole mwaya, msamehe bure yule ni mume wnagu ila kuna matatizo Fulani yanamkabili ndiomana”
“Asante, ila alichonifanyia sio sawa kabisa ukizingatia hakuna nilichomkosea”
“Ila wewe jana mlivyoenda kuzika kuna kaburi ulikaa eeeh”
Bonge akashtuka sana na kumuuliza Sophia,
“Umejuaje? Maana kuna kaburi nilikaa kweli tena nilikaa peke yangu baada ya kuchoka kuchimba, wewe umejuaje?”
“Nikipona nitaomba unipeleke kwenye hilo kaburi”
“Niambie umejuaje dada? Mbona umeanza kunitisha?”
“Kuna kitu nimeona, na nimejua kwanini mume wangu amejua ni wewe na nimeelewa kwanini ulikuwa ni wewe”
“Nilikuwa ni mimi kivipi?”
“Hukuwa wewe kiuhalisia ila mwili wako na sura yako ndio vilivyotumika”
“Kwenye nini mbona sikuelewi”
Sophia akakaa kimya na kumuomba huyu mgonjwa apumzike kwanza kwani kuna mengi alikuwa akiyaona, kwakweli Sophia hata yeye mwenyewe alianza kujishangaa kwani vitu vingi sana vilibadilika kwake na alikuwa akiona mambo mengi sana ingawa mengine alikuwa akimficha mumewe na kuogopa kumueleza waziwazi. Akafikiria mengi sana huku akimuangalia huyu bonge ambaye hakuna alilokuwa akilijua zaidi ya kujua vile alivyokabwa na Ibra kiasi cha kuzindua tatizo linguine kwenye mwili wake.

Ibra alikaa pale nje akisubiri muda wa kuona tena wagonjwa ufike huku akiwa amekerwa sana na yule nesi aliyemtoa mule wodini, muda wa kuona wagonjwa ulipofika Ibra akaenda tena kumuona mkewe kwani hakuwa na imani kabisa na mtu aliyelazwa pamoja na mkewe.
Akiwa mule wodini mara akaja tena rafiki yake Lazaro akiwa ameambatana na baba John, baada ya salamu na pole baba John akamwambia Ibra,
“Kuna habari mbaya ndugu yangu”
“Habari gani tena hiyo?”
Lazaro akawa anamzuia baba John kusema hiyo habari mule wodini ila baba John hakutaka kusikia na kumwambia Ibra kilichojiri.
Kwakweli ilikuwa ni habari mbaya sana kwa Ibra na kumfanya aanguke chini na kuzimia.

Itaendelea kama kwaida……..!!!!!!
Toa maoni yako mdau.

No comments:

Post a Comment