Mtunzi Jimmy Luoga
+255 755 714 395
SEHEMU:1
Nilizaliwa Mkoa wa Ruvuma katika Wilaya ya Mbinga Mjini mtaa wa Misheni. Rose Kapinga ndilo jina nililobatizwa katika kanisa la Mtakatifu Alois Gonzaga liliopo hapa hapa Mbinga mkabala kabisa na mtaa wetu, kwani jina la Misheni limetoholewa kutoka lugha ya kiingereza missionary ambao walikuja Wilaya ya Mbinga kipindi cha ukoloni na kulijenga kanisa hilo.Mara baada ya kuhitimu elimu yangu ya msingi katika shule ya msingi Mazoezi ambayo Kwasasa inajulikana shule ya msingi Mbinga mwaka 1998 nilichaguliwa kujiunga na shule ya Wasichana Songea ambako nilifanya vizuri kidato cha nne na kunifanya niendelee na masomo ya kidato cha tano na sita katika shule ya sekondari Wasichana Kilakala iliyopo Morogoro.Wazazi wangu walifurahia sana maendeleo yangu kwani nakumbuka siku moja Mzee mmoja niliyemkumbuka Kwa jina la pili la Mzee Komba alimwambia Baba mbele yangu kuwa kamwe hawezi kusomesha Mtoto wa kike kwasababu wengi wao huishia kubeba mimba tu.Niliumia sana kwani katika maisha yangu mpaka nahitimu kidato cha sita nilikuwa Sijawahi kutembea na mwanaume japo nilikutana na majaribu mbalimbali, nakumbuka Nikiwa kidato cha tano shuleni kwetu kulikuwa na mahafali ya kuwaaga kidato cha sita.Mimi nilikuwa na rafiki yangu aliyejulikana sana pale shuleni Kwa jina la utani la utani la Aleluyah japo Hakuwa mlokole ila matendo yake ya kutojichanganya yalimpelekea kuitwa hivyo.Jina halisi la msichana huyo lilikuwa ni Alice, ambaye kwao halisi ilikuwa jiji la Dar es salaam ambako Wazazi wake walikuwa kikazi.Kama ilivyokuwa kawaida katika sherehe za mahafali katika kipindi hicho ilikuwa lazima shule jirani ialikwe, Kwa historia ya Kilakala ilikuwa ikiialika shule ya sekondari wavulana Mzumbe ambayo haipo mbali sana na shule yetu kwaajili ya kushiriki muziki.Majira ya saa kumi jioni lilikuja gari aina ya Bedford ambalo liliwabeba wanafunzi kutoka shule ya Sekondari wavulana Mzumbe ambao walikuwa wakishangilia Kwa nyimbo mbalimbali.Mimi na Alice tulikuwa bwenini tulitoka nje kushangaa kwani hatukuwahi kushuhudia tukio kama hilo na kama ujuavyo katika shule yetu tulikuwa Wasichana tupu.Mara baada ya kuteremka kwenye gari kuna baadhi ya Wasichana wa shule yetu walikumbatiana Kwa furaha na wavulana baadhi jambo ambalo lilizidi kutushangaza mimi na mwenzangu na zaudi nilijiuliza maswali mengi mojawapo likiwa la Wasichana hao waliwafahamu vipi hao wavulana na wakati muda mwingi tulilindwa kama wafungwa?. Baada ya kushangaa mimi na rafiki yangu Alice tuliingia chumbani kwaajili ya kujiandaa na masomo ya usiku kwani tulishapanga kuwa tusingehudhuria disco hilo ambalo lilishaanza kurindima kuanzia saa kumi jioni.Mara baada ya kujimwagia maji na kula chakula cha jioni tuliingia bwenini kisha tukachukua daftari zetu na kuelekea darasani "wakina dada samahani tunaomba mtusubiri mara moja!" ilikuwa sauti ya mvulana mmoja aliyekuwa na mwenzake, Mimi na Alice tulitazamana tukaona haikuwa na haja ya kuendelea kutembea hivyo tukalisikiliza ombi lao "Mimi naitwa Emanuel na Mwenzangu anaitwa John sijui wenzetu majina yenu.." alimaliza yule Kijana aliyeitwa Emmanuel "Mimi naitwa Rose Kapinga na Mwenzangu anaitwa Alice Mkuya" nilijibu huku nikitabasamu, "samahani tulikuwa na ombi moja.." Emmanuel aliyeonekana kuwa muongeaji sana kuliko mwenzake alisisitiza "Hakuna tatizo tunawasikiliza.." Alice alijibu "tulikuwa tunaomba company yenu disco baadae kama itawezekana.." Emmanueli alizungumza Kwa ushujaa, hapo ndipo nilipoamini kwanini rafiki yangu aliitwa Aleluyah, aliwaporomoshea matusi wale wakaka mpaka walipoondoka walishindwa hata kuaga, nilimtuliza Alice kisha tukaelekea darasani.Kadiri giza lilivyozidi ndipo kelele za muziki zilivyozidi hivyo hatukuwa na budi kuhahirisha masomo usiku huo na kwenda kulala.Majira kama ya saa tatu sauti ya muzuki na kelele za wanafunzi zilianza kuniingiza majaribuni huku roho yangu ikihadaika kuwa niende japo nikashangae tu na sio kucheza, niliteremka toka kitandani kwangu moja Kwa moja mpaka chini kisha nikamtazama Alice ambaye alikuwa anakoroma wakati huo, nilijiweka sawa kisha nilinyatia na kuondoka pale chumbani.Nilijongea moja Kwa moja mpaka ukumbi wa shule ambao uliwekwa muziki, nilipoingia ndani nilikuta muziki umechanganya huku wanafunzi wakicheza wawili wawili na baadhi yao wakicheza peke yao. Nilijivuta taratibu mpaka kwenye kiti kilichokuwa wazi kisha nikaketi nikiwaangalia waliokuwa katikati wakilisakata rhumba, baadhi ya wanafunzi wenzangu walinishangaa sana kuniona humo ndani kwani dhahiri kabisa waliamini nisingeweza kutia mguu wangu eneo hilo, kila wimbo mzuri ulipoanza wanafunzi walipiga kelele za kushangilia.Nilijikuta nikitabasamu peke yangu nikiwa nimeketi kitini, baada ya muda kidogo niliweza kusikia mtangazaji akisema kuwa kuna mwanafunzi kutoka Mzumbe alitaka kufanya show ya muziki wa Michael Jackson "Thriller" hivyo waliomba ukumbi uachwe wazi Kwa muda, wanafunzi walishangilia Kwa nguvu Mara baada ya mvulana huyo kuingia katikati ya ukumbi huo.Kiukweli mavazi ya kumeremeta aliyovaa Kijana huyo yalimvutia kila mmoja.Nilijipenyeza katika kundi la watu waliokuwa wakiniziba, nilipofika mbele niliweza kumuona mtu ambaye sura yake nilihisi niliona mchana huo.Hakuwa mwingine bali ni Emmanuel ambaye alionekana kupendeza zaidi na namna alivyokuwa akicheza vizuri nilijikuta nikiingia katikati na kumtuza noti ya shilingi mia mbili kisha nikampangusa jasho na kitambaa changu, umati mzima uliripuka Kwa shangwe na nderemo kwani hakuna aliyetarajia kuniona mimi naweza kufanya jambo kama hilo kutokana na upole niliokuwa nao pale shuleni.Baada ya show kumalizika nilirudi tena kitini na muziki uliendelea, nilishtuka mtu akinishika bega langu la kulia, nilipoyainua macho yangu yaligongana na Emmanuel ambaye aliniinamia kisha akaniomba nikacheze naye japo kidogo, nilijikuta nikihadaika na kumkubalia mvulana huyo ambaye alionekana kuwavutia Wasichana wengi pale ndani.Emmanuel alionekana mnyenyekevu pia mwenye kujiheshimu kwani pamoja tulikuwa tukicheza muziki hatukukalibiana wala kushikana mwilini, Nilijikuta nikianza kumpenda Kijana huyo ambaye alionekana kujari sana hisia zangu.Tukiwa katikati ya muziki mwalimu aliamuru muziki ufungwe kisha Wasichana wote tukaambiwa tubaki pale ndani na wavulana wote waliambiwa waende kwenye gari.Nilibaki nimeganda nikimtazama Emmanuel ambaye alikuwa akinitazama kwa macho ya huruma, nilijikuta nikianza kumuwaza kijana huyo ambaye sikujua ni siku gani tungeweza kukutana.Zoezi la kuondolewa wavulana lilipoisha tulifuatia wasichana kutoka huku tukisindikizwa na matroni wetu bwenini.Nilipoingia bwenini nilianza kuvua nguo moja baada ya nyingine ndipo katika mfuko wangu wa sweta nilishtuka nikishika kitu kama karatasi, nilipoangalia vizuri niliweza kuona barua.............
Je barua hiyo imeandikwa na nani? Usikose kuungana nami toleo lijalo.
No comments:
Post a Comment