Upo tayari kuingia katika mkataba wa maisha na rafiki yako wa jinsia nyingine? Kabla ya kufaulu kuingia kwenye ndoa, wewe na mwenzio mnapaswa kuwa na sifa za ukomavu zinazoweza kuwahakikishia ndoa imara. Wachumba waliotayari kwa urafiki wa milele huwa na sifa nyingi za kupevuka, lakini kuu kati ya hizo ningependa kushiriki nawe.
1. Kila mmoja anajua anachohitaji na atakachochangia katika ndoa
Ni dalili ya utu uzima kung’amua kuwa “si vema” ubakie mwenyewe. Unaonesha umekomaa unapohisi uhitaji wa mwingine maishani mwako ili uwe kamili (Mwanzo 2:18). Unapotambua mahitaji yako ya kihisia, kiroho, kijamii, na hata kimwili unakuwa tayari kumkaribia mwenzako ili ukamilike. Ukiwa na utambuzi huo huoni sababu ya kuficha hisia zako. Huna aibu kufungua moyo wako mbele ya macho ya mwenzako. Unamtaka mwenzio ajue umeanza safari ya kumkaribia ambayo kilele chake ni “mwili mmoja”— ngozi kwa ngozi, moyo kwa moyo (Mwa 2:24-25) .
Mkaribie mwenzako na moyo mkunjufu tayari kukamilishwa na mtazamie mwenzako kukutana nawe akiwa na moyo ulio wazi tayari kujazwa na wewe. Kama mikono miwili inapoingiliana inaposhikamana ndivyo wewe na yeye mtakavyokamilishana mnakapokutana. Ulipokuwa mtoto hukujua hilo. Ulidhani wazazi na ndugu zako wapo ili kukukamilisha, kukidhi mahitaji yako tu. Upeo wa kujua mahitaji ya wengine huja na miaka inaposonga. Kama kila mmoja wenu anajua kutoa na kupokea, kupokea na kutoa basi mmeiva katika ushirikiano. Maana ndoa ni ushirikiano,“nakupa unipe”.
2. Kila mmoja humpenda mwenzake kama anavyojipenda binafsi
Wapenzi walioiva kwa ndoa wanajua fika upendo wa ushirikiano baina yao umewezekana kwa kuwa kila mmoja ameshiriki nafsi yake na mwingine. Kama kila mmoja angedharau nafsi yake angewezaje kushiriki zawadi aliyoidharau na rafiki ampendaye? Wapendanao wanajua Bwana hakukosea aliposema “mpende jirani yako kama nafsi yako.” (Walawi 19:18; Mark 12:31).
Kila mmoja wenu asipojipenda mwenyewe; yaani, asipojisikia vizuri, salama, na jasiri kama alivyo, ni vigumu kupendana ninyi kwa ninyi. Usipojikubali ulivyo hutamuamini mwenzako akikuambia amekukubali ulivyo. Tambua unapopanda mashaka nafsini utavuna hofu katika uhusiano. Hofu ya kukataliwa itatia ganzi miguu yako hata ushindwe kumkaribia mwenzako ipasavyo. Kumbuka palipo na hofu hakuna ukaribu wala upendo (1Yoh 4:18).
3. Wote hufurahi wanapokutana na vile vile wakitengana
Kama ilivyo kwa uhusiano wowote chini ya jua, ndoa inahitaji ukaribu na umbali; Sulemani anauita, “Wakati wa kukumbatia, na wakati wa kutokumbatia” (Mhu 3:5). Uhusiano unaoleta watu karibu pasipo kuwaachia nafasi ya kila mmoja kuwa kama alivyo una hatari zake. Mojawapo ni kumfanya mshirika wa uhusiano huo kuwa sehemu ya nafsi ya mwingine. Matokeo yake ni kutawaliwa na kukinaiwa.
Awali wanandoa walipokuwa hawana hatia kila mmoja alisimama pembeni ya mwingine kwa umbali wa uhuru na ukaribu wa kutegemeana. Adamu na Hawa walifurahia uhuru wa kila mmoja kama nafsi na utegemezi wa kila mmoja kama washirika wa “mwili mmoja” (Mwa 2:28) Mambo yaliharibika dhambi ilipovamia uhusiano huo na tamaa ya mwanamke ikawa kwa mumewe na
mumewe akamtawala (Mwa 3:16 ). Tangia dhambi iingie duniani tamaa iliyokuwa mnyoro wa kuwaleta wapendanao pamoja imegeuka kuwa mnyororo wa utumwa.--sasa anayependa anapoteza umbali wa kuwa huru kama alivyo na anafanywa zezeta wa kutumikia matakwa ya bwana/bibi ake.
Ikiwa kama ndoa yenu itaeupukana na “udikteta wa upendo” mtajifunza kupeana nafasi ya kuwa nafsi katika uhusiano wenu wa sasa. Kila mmoja awe huru pasipo wivu kufurahia maburudisho ambayo mwenzake hana hamu nayo, au kuwa na marafiki wengine bila kuwa na hofu ya kuvunja uchumba. Kila mmoja awe huru kutumia talanta na vipaji alivyopewa bila ya kuwa na wasiwasi kuwa kwa kufanya hivyo anahatarisha mahusiano. Furahieni upweke wa kuwa mwenyewe na ushirika wa kuwa pamoja. Aganeni kisha rudianeni. Tenganeni kisha ambataneni. Ni kwa kutengana ndipo kila mmoja wenu ataona uthamani wa mwingine; na ni kwa kuwa pamoja ndipo kila huyo ataona haja ya kuwa na mwenyewe. Wapenzi waliozama kwenye penzi la kweli wanajua hilo na kulikubali kama uhalisia wa maisha chini ya jua.
4. Wachumba wako huru na wazi wao kwa wao kuhusiana na kila mmoja alivyo
Uhusiano wa karibu kama wa wanandoa unawataka wahusika wajianike nafsi kila mmoja kwa mwenzake pasipo kuona haya au hofu. Ndivyo wanandoa wa kwanza walivyokuwa. “Nao walikuwa uchi wote wawili, Adamu na mkewe, wala hawakuona haya” (Mwa 2:28). Hawakuwa na sababu ya kujisikia haya kwa kuwa hawakuwa na kibaya cha kuficha. Unaposhindwa kufikia kuwa huru kwa mwenzako ni kwa sababu unahofu una mabaya yanayopaswa kutojulikana. Hivyo unaishia kujilinda na kujihami ili makosa na kasoro zako zisifahamike. Lakini kwa kuwa utupu unaoulinda upo mbele ya macho yako daima, utaishia kuuona uchi wako kwa mwenzako; makosa yako utamsukumia yeye, kasoro zako utamlaumu yeye. Ni vigumu kujenga mahusiano ya wazi na mtu msiri.
Mruhusu mwenzako ajue ulikotoka, familia yako, uzoefu wako wa utotoni mpaka ujanani. Mfahamishe vidonda na makovu uliyoyapata ili akuelewe. Mueleze uliyojifunza kupitia uchumba au urafiki uliokuwa nao. Mwachie atazame kurasa za historia ya maisha yako, ukurasa mmoja baada ya mwingine. Mruhusu akusome ili akuelewe. Uhuru na uwazi wa aina hiyo utawaleta pamoja; maana, hata hivyo, hakuna ukuta kati yenu.
5. Kila mmoja wao anaweza kujieleza anataka nini kwa uwazi na upole
Hata kama wachumba wamesomana na kufahamiana kwa kitambo bado wanao umuhimu wa kila mmoja kujua namna ya kujieleza. Ni Mungu pekee anayejua yaliyomo ndani ya moyo wa mtu. Pasipo uwezo wa kujieleza mwenzako hatafahamu unataka nini; yeye si Mungu. Wachumba wanaojitambua kuwa kila mmoja ni kiungo kwa mwingine wanachukua kwa uzito ushauri wa Paulo aliposema, “uvueni uongo, mkaseme kweli kila mtu na jirani yake” (Waef 4:25).
Bila kupiga chenga onesha uhitaji wako wa msaada wa mwenzako: huruma yake, usikivu wake, faraja yake, au uwepo wake. Tumia maneno, “nilikuwa naonelea kwamba…’, “honey ningefurahi..”, au “Mpenzi nilisikitika…” Mwalike mwenzako achungulie moyo wako ulivyomhitaji badala ya kumnyoshea kidole moyoni mwake na kumtoa makosa. Hakika, “Jawabu la upole hugeuza hasira; Bali neno liumizalo huchochea ghadhabu.” (Mith 15:1).
Hivyo, acha kujifanya mshitaki, vua joho la uhakimu, vua uongo, bakia na uso wa rafiki wa kusaidiwa (maana ndiyo uso wako halisi) uone kama mwenzako hataguswa na akusaidie. Jifunze kujieleza pasipo kumshambulia mwenzako. Usiruhusu namna unavyopeleka ujumbe uharibu ujumbe wenyewe. Kumbuka maneno yanaweza yasivunje mfupa lakini yakavunja moyo. Jitahidi kujieleza kwa uwazi uliochanganyikana na upole ili ufaidi msaada unaoutazamia.

6. Kila mmoja anatafuta kutimiza mahitaji ya mwenzake
Wapenzi walioachana na utoto hawaendekezi “umimi” katika mahusiano yao. Hawajifikirii wao tu. Hawana mashindano tena ya “mwamba ngoma”; isipokuwa, wamejifunza kila mmoja kumhesabu “mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake” na badala ya kila mtu kuangalia mambo yake mwenyewe kila mtu huangalia mambo ya mwenzake (Wafil 2:3,4). Alichosema Paulo ndicho kinachothibitishwa na wanandoa wengi leo: unapojali mahitaji ya mwenzako, mwenzako anavutwa kujali mambo yako.
Utajua upo tayari kwa ndoa kama uko tayari kumtimizia mahitaji mwenzako. Hakika utafaidi ndoa wewe mtoaji kuliko hata mpokeaji. Maana ni ukweli mtupu kwamba, "ni heri kutoa kuliko kupokea" (Matendo 20:35)
7. Kila mmoja ana uwezo wa kujitegemea kiuchumi
Uwezo wa kutegemeza familia kiuchumi ni muhimu kwa kila mchumba kuwa nao. Una afya, talanta, ajira, na ujuzi wa kukusaidia kujitegemeza kifedha? Kama ndiyo basi upo tayari kwa ndoa. Uchumi unapokuwa mzuri wa kutosha kuwahakikishia ndani chakula mezani, mavazi ya kuwasitiri, na pango la kuwahifadhi, basi ninyi wapendanao mna hakika ya kuwa na muda kuendeleza pendo lenu.
Mahitaji ya msingi kama chakula, mavazi na malazi yasipotafutiwa ufumbuzi ndoa haibakii salama. Na kama mahitaji ya msingi sio shida ila wachumba wanauchu wa utajiri bado mahusiano yao yatakuwa hatarini. Badala ya kuwa na muda wa mahusiano, kila mmoja atakuwa barabarani “kujitafutia”.
Maisha ya ukristo na hasa ya ndoa ya kikristo yanapaswa yawe ya kuridhika na vilivyo vya muhimu maishani. Paulo alikazia wazo hilo aliposema, “Kwa maana hatukuja na kitu duniani, tena hatuwezi kutoka na kitu; ila tukiwa na chakula na nguo tutaridhika na vitu hivyo. Lakini hao watakao kuwa na mali huanguka katika majaribu na tanzi, na tamaa nyingi zisizo na maana, zenye kudhuru, ziwatosazo wanadamu katika upotevu na uharibifu.” (1Tim 6:7-9; Mith 30:8). Ndoa si mali na mali si ndoa.
Wachumba ambao hawajalewa na mvinyo wa mahaba hawatakimbilia ndoa pasipo maandalizi ya kujitegemea kiuchumi. Na wapenzi ambao hawajatekwa na ndoto za utajiri hawatachelewesha mipango ya ndoa kwa kisingizio “hatuko tayari”.

No comments:
Post a Comment