Thursday, 19 January 2017

NILIMUOA DADA YANGU

Mtunzi Jimmy Luoga

EPISODE:8

Ilipoishia tuliona Erick akizama kwenye dimbwi zito la mapenzi na msichana Liz, lakini alfajiri ya siku ya pili yake anapigiwaa simu ya Allen na sauti ya mtu ambaye hamfahamu na kumueleza kuwa anahitajika kituo cha Polis.Je Erick anaitiwa nini kituo cha Polis na Je nini hatma ya mapenzi yake ambayo ndio kwanza yanaanza na msichana Liz? Ungana nami katika sehemu hii ya nane ya simulizi hii.

SASA ENDELEA.................
Niliendelea kujiuliza maswali kadha wa kadha kuwa kwanini simu nilipigiwa na mtu mwingine tofauti na Allen lakini nilikosa jibu kabisa, niligeuka nikamtazama Liz ambaye alikuwa bado kauchapa usingizi mzito kisha nikatabasamu, nilijaribu pia kukumbuka ndoto niliyoota usiku lakini jibu lilibaki kuwa huenda ilikuwa ndoto ya kawaida huku nikiwaza huenda Mama alichukizwa na mimi kutokomea moja kwa moja bila hata ya kumueleza nilikuwa wapi.Nilijikuta nikianza kumkumbuka Mama na dada yangu Lilian ambao niliamini kuwa huenda waliishi maisha ya tabu sana, nikiwa najimwagia maji maliwatoni picha ya Mama na dada yangu Lilian ilizidi kuyatawala mawazo yangu mpaka nikashangaa kwani haikuwahi kunitokea hali kama hiyo, nilipomaliza kuoga nilirudi moja kwa moja chumbani na kumkuta Liz akiwa ameamka huku akiwa kajilaza na kunitazama kwa aibu, wakati huo bado alikuwa amejilaza pale kitandani.Tulisalimiana kisha aliniuliza kwanini niliamka mapema kiasi kile, nilimueleza kuhusu simu niliyopigiwa kisha nikamsisitiza kuwa siku hiyo hasingeondoka ili tushinde sote nikirudi toka kituo cha Polis naye hakupinga, nilivaa suti yangu nyeusi iliyonikaa sawia kisha nikamuaga Liz na kuondoka.Nilipiga hatua za haraka mpaka mahali lilipokuwa gari langu kisha nikaingia na safari ya kituo cha Polis Oestabay ilianza, haikunichukua muda niliwasili pale kituoni kisha moja kwa moja niliingia ndani na kuishia pale mapokezi, nilipoulizia kulikoni niliitiwa pale askari mmoja alinielekeza ofisi ya Mkuu Wa Kituo ambako ndiko ilionekana ningelipewa maelezo ya kina juu ya ule wito wangu.Moja kwa moja nilielekea mpaka ofisi ya Mkuu Wa Kituo kisha nikagonga hodi na kukaribishwa na sauti nzito toka pale ndani, haraka niliweza kugundua sauti hiyo ndio ile ambayo ilizungumza nami kupitia simu ya Allen, nilipoingia nilipokelewa na mzee wa makamo ambaye alionyesha ukarimu wa hali ya juu kwangu "kama sikosei wewe ni ndugu wa Allen Andrew?" yule mzee aliyevalia gwanda la kipolis lenye nyota kadhaa mabegani mwake aliniuliza huku akitabasamu, nilimjibu kuwa hakukosea hata kidogo "tumekuita hapa kwakuwa kuna jambo muhimu tunataka kukueleza" nilitulia kimya kisha nikaitikia kwa kichwa kuonyesha kuwa nilikuwa namsikiliza mzee huyo, "tunamshikiria Allen kwa kosa la mauaji" almanusura nizimie kwani niliona kama ndoto, "unasemaje mzee sijakuelewa?" alirudia tena mara ya pili na tatu, ndipo nilipoamua kumuuliza mauaji ya nani? "mauaji ya Andrew Reuben" nilipigwa na butwaa kwani sikuweza kuamini kama Allen angeliweza kufanya tukio kama hilo, nilizidi kujiuliza maswali kuwa ni wakati gan Allen aliweza kufanya tukio hilo?, yule askari alinieleza kuwa baada ya kufanya vipimo wameweza kugundua kuwa marehemu Andrew aliuliwa kwa kukabwa shingo yake na kuvunjwa.Nilijaribu kuvuta kumbukumbu ni wakati gani Allen aliweza kufanya hivyo ndipo taratibu niliweza kukumbuka kuwa mara Baba yetu mlezi kumkuta akiwa amezidiwa tulimuingiza kwenye gari na mimi nikawa naendesha, Allen ndiye aliyemshikilia mgonjwa siti ya katikati hivyo nilihisi huenda wakati huo ndio akiutumia kumuua Andrew, "vipi mbona upo kimya muda mrefu au kuna lolote unafahamu juu ya hilo?" Mkuu wa kituo aliniuliza akiwa kanikazia macho, nilimjibu kuwa mimi sifahamu lolote juu ya hilo, "unaweza kutueleza kwanini marehemu hakuweza kumuandika Allen kama mrithi wa mali zake na ukawa wewe?" kwa kuwa nilimpenda sana Allen kama kaka yangu wa Baba na Mama mmoja nilijibu kwa kifupi sikufahamu kwanini, mwisho aliitwa askari mpelelezi akachukua maelezo yangu kisha niliruhusiwa kuonana na Allen ambaye alikuwa kafungiwa selo.Allen alitoka na mara baada ya kuniona mimi alianza kububujikwa na mchozi, nilijikuta nikimhurumia Allen kwani tayari maji yalishamfika shingoni, nilimuuliza Allen kwanini alifanya kitendo hicho naye alinijibu kuwa tamaa ndio zilimponza, nilijikuta nikikasirishwa na majibu ya Allen kwa kukiri kuwa ni kweli yeye alihusika na mauaji ya Andrew ambaye alijitolea kutulea tangu tulipokuwa wadogo mpaka utu uzima, wakati huo Allen alibakiza kama miezi kadhaa ahitimu shahada yake ya kwanza.Niliondoka kwa jazba huku nikimuacha Allen akilia kwa sauti, niliweza kusikia kwa mbali kuwa aliomba nimsaidie aweze kutoka pale kituo cha Polis, jambo ambalo lilikuwa gumu kwa tuhuma za mauaji hapa nchini.Niliwasili nyumbani kama majira ya saa tano kasoro na kumkuta Liz akiwa kaketi sofani akitazama luninga, alinipokea kwa tabasamu kisha alisimama na kuja kunikumbatia, nilijisikia furaha lakini kwa jambo ambalo nililisikia kule kituo cha Polis juu ya tuhuma za Allen mpenzi wangu Liz aliweza kugundua na kuniuliza, nilitulia kwa dakika kadhaa kisha nikaanza kumsimulia, Liz alisikitika sana lakini haraka niliweza kuhisi jambo, kwani Liz pia alionekana kuwa na macho yaliyojaa hofu kama vile alijua jambo fulani, tayari chai ilikuwa imetengwa mezani lakini kila nilipomtazama Liz alionekana akihangaika huku na kule, kwa upande wangu nilijua huenda Liz aliumia sana juu ya tuhuma za Allen, nikiwa najimiminia chai tayari nimeinua kikombe kuelekeza kinywani nilishtuka mkono ukivumishwa na kukipiga kile kikombe, kile kikombe kilinipokonyoka na kuangukia upande wa pili.Alikuwa sio mwingine bali ni Liz ambaye alifanya hivyo na kisha akakimbilia chumbani, harufu kali ya sumu ya panya iliweza kupenyeza katika pua zangu, sikuyaamini macho yangu kwa kile ambacho nilikiona, sikutegemea msichana mzuri kama Liz angetarajia kuniua Erick mimi, niliingia chumbani kwa jazba na kumkuta Liz akiwa ameshika kisu akiwa kakionyeshea tumboni kwake akiwa na lengo la kujiua, japo nilikuwa na hasira za kuua mtu lakini nilijikuta nikibana breki na kuanza kumuomba Liz asifanye kitendo hicho, Liz alibubujikwa na machozi kisha akaanza kujieleza kuwa yeye alitumwa na Allen amuue Erick kisha angemlipa donge kubwa la pesa,nilizidi kuumia baada ya kusikia maneno ya Liz "kiukweli Erick mwanzo sikukupenda kama ulivyofikiri, lakini usiku wa kuamkia leo umeyateka kabisa mawazo yangu" niliendelea kumsikiliza Liz huku nikiwa nabubujikwa na machozi kama mwanamke, "Erick ndugu yako ndiye aliyenitumia ujumbe mfupi jana kuwa nikutilie sumu kwenye pombe lakini nilishindwa ndio maana leo niliweka kwenye chai" wakati huo bado Liz alijigeuzia kisu tumboni kwake huku akiwa analia, "Erick sina umuhimu wa kuendelea kuishi kwani ni bora nife kuliko kukukosa wewe mpenzi" maneno ya Liz yalinifanya nipige hatua taratibu kumfuata alipo huku nikimueleza kuwa yeye hakuwa na kosa bali Allen ndiye aliyekuwa na makosa, nilizidi kumuomba Liz kuwa asijiue ili aendelee kuwa mpenzi wangu, nilimhakikishia kuwa bado nilimpenda kuliko alivyofikiri kuwa upendo wangu ungeisha baada ya tukio hilo.Liz alitupa kisu kisha tukakumbatiana kwa nguvu, tokea siku hiyo ndipo mapenzi ya ukweli nilipoanza kuyapata kwa msichana huyo.Allen alifikishwa mahakamani na hukumu ilipofika alihukumiwa kifungo cha maisha jela huku ushahidi wa alama za vidole zilizothibitishwa na daktari na yeye mwenyewe kukiri kuwa kweli alimuua Abdrew Reuben kwaajili ya tamaa ya mali.
               ******************''

Niliendeleza gurudumu la maisha huku niliyedhani ni ndugu yangu kumbe ni adui yangu akiozea Segerea, mapenzi baina yangu na Liz yalipamba moto kwani yeye alikuwa wa kwanza kuhitimu Shahada ya uchumi na kuhamia moja kwa moja pale nyumbani kwangu, niliamua kumpa nafasi ya Ukaimu Mkurugenzi katika kampuni zangu kwakuwa mimi nilikuwa nabanwa na masomo.Siku zilizidi kwenda huku mimi na Liz tukiishi nyumba moja kama mke na mume huku tukiendelea kuvunja amri ya sita, miaka ilienda na hatimaye mimi pia nilikuwa nahitimu na kutunukiwa Shahada ya udaktari.Siku moja nilipokuwa na Liz sebuleni tulijadiliana swala la ndoa ambapo nae aliafiki kwa asilimiamoja, lakini nilipozungumzia anipeleke kwa wazazi wake alipiga danadana kuwa bado ilikuwa mapema, sikumlazimisha kwani hata yeye pia aliposema tuende kwa wazazi wangu nami nilimzungusha kwani nilijua kuwa tuhuma za mauaji ya Baba yangu mzazi zingefufuka upya, niliamua kumdanganya Liz kwa kuwaandaa wazazi wa bandia na kuwaleta pale nyumbani, waliishi pale nyumbani kama siku tatu kisha wakaondoka, sasa kazi ilikuwa kwake kumbe nayeye hakupenda kunipeleka Kahama hivyo aliwaleta wazazi wake ambao mimi binafsi nilikubaliana na Liz kuwa tuafikiane kwenye swala la ndoa.Wazazi wa Liz walikaa kwa siku kadhaa kisha wakaondoka, taratibu za kutoa mahali na harusi zilifanyika lakini kila nilipomueleza mpenzi wangu Liz juu ya kutoa mahali alikataa katakata kuwa yeye hakupenda kufunga ndoa ya kulipiwa mahali kwani haikuwa na haja.Niliamua kusikiliza matakwa ya mke wangu mtarajiwa, taratibu na mipango ya harusi ilifanyika na hatimaye siku iliyopangwa iliwadia, wafanyakazi wa kampuni zangu siku hiyo walihudhuria kanisa la mtakatifu Joseph lililopo mkabala kabisa na bahari ya Hindi, kanisa lilifurika watu wengi kushuhudia harusi yangu na Liz, mara baada ya kuwasili Bi harusi pale kanisani nilimpokea kisha misa takatifu ya sakramenti ya ndoa ilianza.Ulifikia wakati wa kufunga ndoa ambapo mimi na Liz tulijongea mpaka pale altareni ambapo Padre alianza kutufungisha ndoa, ilipofikia wakati wa kufungishwa ndoa kanisa zima lilikuwa kimya kwani mara nyingi tukio kama hilo huweza kubadilika mara moja na hali ikawa sio shwari, Padre alianza kunuliza mimi ambapo nilijibu kwa ustadi mkubwa "Erick unakubali kumuoa Lizbeth Peter? kwa tabu na raha awe mke wako wa ndoa mpaka kifo kitakapowatenganisha?" Padre alianza "ndio nakubali" nilijibu na kusababisha kanisa zima kulipuka vifijo na nderemo, wakati huo na wale wazazi wangu wa bandia walikuwepo pale kanisani pia wazazi wa Liz walikuwepo, baada ya kumaliza kwangu Padre alimgeukia Liz ambaye mchozi ulimlengalenga kisha akaanza kumuuliza kama alivyoniuliza mimi, Liz alikaa kimya kama dakika nzima, Padre alirudia tena mara ya pili, minong'ono ilianza kusikika.........

Je Liz atakubali kuolewa na Erick?, na nini hatma ya simuliz hii? ungana nami toleo lijalo

No comments:

Post a Comment