Mtunzi Jimmy Luoga
SEHEMU:4
Ilipoishia tuliona msichana Rose akiifungua barua iliyotoka kwa Emmanuel, akiwa na shauku kubwa anaenda mahali ambapo pametulia na kuanza kuisoma.Je barua hiyo itampatia majibu na matarajio yake ya kuwa wapenzi na Emmanuel?
SASA ENDELEA......................
Barua hiyo iliandikwa hivi, "Kwako mpendwa Rose, pokea salamu nyingi hapo ulipo.Mimi ni mzima wa afya njema hofu na mashaka ni kwako wewe uliyembali nami.Lengo la kukuandikia barua hii ni kutaka kukujibu kuwa barua yako nimeisoma na kuielewa, kwa kifupi nimekubali ombi lako lakini kwa sherti moja la kutokutana kimwili mpaka tutakapomaliza masomo.Nadhani utakuwa umenielewa hivyo kwa kipindi hiki chote kilichobaki tutaendelea kuwa marafiki wa kawaida.Asante, wako akupendaye Emmanuel Ngui. Nilijikuta nikiachia kicheko cha furaha peke yangu pale mahali nilipokuwa nasoma ile barua, nilikuwa na furaha isiyo na kifani kwani suala la kukutana kimwili hata mimi binafsi sikulihitaji haraka kwakuwa toka nizaliwe nilijiwekea nadhiri ya kutolewa bikra hiyo na mume wangu atakayenioa.Siku zilikatika huku tarehe za kufanya mtihani wa kuhitimu kidato cha sita zikisogea kwa kasi, mawasiliano ya barua kati yangu na Emmanuel yalizidi kwani ilikuwa kila juma lazima nipokee na nitume barua kwa Emmanuel mvulana niliyetokea kumpenda kuliko mtu yeyote Duniani.Nakumbuka kama kesho yake tunaingia kwenye mtihani wa kumalizia kidato cha sita alinitakia mtihani mwema kisha akaniekeza mahali ambapo tungekutana kwaajili ya kuagana mara baada ya kumaliza mitihani, aliandika kwa herufi kubwa MOROGORO HOTEL.Nilifurahi zaidi kwani niliamini siku hiyo tungezungumza mambo mengi sana.Siku iliyofuata tulianza mitihani huku nikiona siku haziendi kutokana na hamu ya kukutana na Emmanuel pale hotel.Mara tu baada ya kumaliza kufanya mitihani wanafunzi walianza kuagana na kuondoka mmoja baada ya mwingine, "Rose kuna mgeni wako anakuhitaji kule ofisi ya Mkuu wa shule.." alikuwa rafiki yangu Alice aliyeingia pale ndani na kunipa taarifa hiyo.Upesi wazo la Emmanuel lilinijia akilini kuwa huenda kaamua kunifuata pale shule, nilitoka nje kwa haraka bila hata ya kumuuliza Alice huyo mgeni kama alimuona.Mara tu baada ya kuingia ofisini nilijikuta nikipoteza furaha yangu kwani nilimuona Baba yangu mzazi Mzee Kapinga akiwa anaongea na mkuu wa shule, "Nimekuja kumchukua binti yangu, naondoka naye sasa havi.." hayo yalikuwa maneno niliyoyasikia kabla hata sijawasalimia.Mwili wangu wote nihisi ukikosa nguvu na furaha yote kupote ghafla, niliwasalimia kwa unyonge Baba na Mkuu wa shule jambo lililopelekea kuulizwa swali na Mkuu kama nilikuwa na tatizo likiwemo suala la ugonjwa lakini nilitikisa kichwa kukataa."Rose bwana! Babako anakuja kukuchukua badala ya kufurahia wewe unanyongea kiasi hicho?.." Mkuu aliongezea maneno hayo na kumruhusu Baba kunichukua, "Binti yangu nilikuwa natokea Dar es salaam kununua gari, hivyo nimeona ni heri nikupitie turudi nyumbani.." Baba aliongea kwa upole jambo lililopelekea niitikie kwa kichwa kuwa nilikuwa tayari kuongozana naye.Aliniomba niende bwenini nikachukue vifaa vyangu tayari kwa safari ya kurudi kwetu Mbinga.Nilienda bwenini lakini moyoni nikikosa amani ni kwa mtindo upi ningeweza kumtaarifu Emmanuel kuwa ningeshindwa kwenda pale Morogoro Hotel kuzungumza nae, nilifungasha virago vyangu nikisaidiwa na rafiki yangu kipenzi Alice ambaye alikuwa akilia kwa kutoniona tena mpaka mwenyezi mungu atakavyotukutanisha, sote kwa pamoja tuliungana kwenye kilio hicho huku mimi nikiongezea na machungu ya kutomuona Emmanuel kwakuwa hata anuani ya kwao pia sikufahamu wapi ningeipata.Ikumbukwe kuwa miaka ya tisini simu zilikuwa za mezani tu hivyo ilikuwa ngumu kwa mimi kufanya mawasiliano na kijana huyo.Alice alinisindikiza mpaka kwenye gari ambalo Baba alitoka kulinunua, nakumbuka vizuri sana gari hilo lilikuwa Land Lover 110, Baba alituangalia kwa uchungu jinsi tulivyokuwa tunaagana na Alice ambaye alitiririkwa na mchozi mashavuni nami vivyo hivyo.Gari liliiacha Kilakala na kuteremka mpaka barabara iliyoelekea Morogoro Mjini.Niliumia kila nilipokumbuka barua ya mwisho ya Emmanuel ambaye niliamini kuwa huo ndio ulikuwa mwisho wetu wa kuonana naye na ingebaki kuwa historia katika maisha yangu.Dereva aliendesha kwa kasi gari hilo mpaka Msamvu ambapo Baba aliteremka garini na aliporudi alibeba chipsi na Soda ambazo alinikabidhi, nilijaribu kupepesa macho nje huenda ningemuona Emmanuel lakini niliambulia patupu.Safari ya Songea hatimaye Mbinga ilianza huku nikiwa sina namna tena juu ya Emmanuel, nilitengeneza picha mbalimbali kichwani ni kwa jinsi gani Emmanuel angeumia kwa kutoniona pale Morogoro Hotel.Ilikuwa majira ya saa nane tulipoondoka Morogoro usingizi ulianza kunichukua taratibu na kujikuta kwenye ndoto nzito.Niliota nikiwa nimetoka pale shuleni na kwenda Morogoro Hotel mimi pamoja na Alice, lakini tulipofika pale tukamkuta John akiwa na Emmanuel, nilimuuliza Emmanuel kulikoni John alikuwepo pale? akanijibu kuwa John ndiye mpenzi wangu nayeye wake ni Alice ambaye alikumbatiana naye, nilipandwa na hasira na kuondoka eneo hilo huku nikilia, "Rose mwanangu unalia nini?.." ilikuwa sauti ya Baba ikiniuliza, kumbe alikuwa anasikia nilivyokuwa nalia, nilimwambia Baba kuwa nilimkumbuka rafiki yangu Alice, akanituliza kisha nikasinzia tena ndoto ileile ikarudia tena.Safari hii nilimkuta Emmanuel na Alice wakiwa hawana nguo chumbani pale Morogoro Hotel wakifanya mapenzi, waliponiona waliniomba msamaha kwa madai kuwa walifanya hivyo kutokana na mimi kusafiri bila kumtaarifu, hivyo kwa hasira kaamua kutembea na rafiki yangu Alice ambaye aliniangalia kwa aibu.Niliufunga mlango kwa nguvu na kutoka eneo hilo huku nikiangua tena kilio cha nguvu.Kama ilivyo ada Baba alinituliza tena, ilikuwa ni usiku wa kiza kinene dereva akiendelea kuendesha gari kwa kasi ileile, "Tutalala hapa Iringa kisha alfajiri tutaendelea na safari.." maelezo ya Baba yalinifanya nijue kumbe tulikuwa tumeshaingia Iringa.Nilipotazama saa yangu ya mshale ilikuwa imetimu saa 5 ya usiku.Tulilala Iringa, alfajiri safari ilianza huku nikijiuliza maswali mengi kwanini niliota ndoto mbili zilizofanana?.Saa nane mchana tulikuwa tumewasili Mbinga.Nilianza maisha wilayani Mbinga huku nikiwa namkumbuka sana Emmanuel mvulana ambaye niliamini kuwa ndiye lilikuwa chaguo langu.
***********************
Miezi kadhaa ilipita, siku moja nikiwa nakula chakula cha mchana nilisikia katika Redio kuwa matokeo ya kidato cha sita yakitangazwa huku nikisikia jina la mwanafunzi aliyeongoza kitaifa kuwa Emmanuel Ngui kutoka Mzumbe, nilijikuta nikirukaruka kwa furaha kama vile mimi nikiwa nimetangazwa kuwa nimefanya vizuri.Nilijikuta nikilia mchozi wa furaha niliposikia jina langu likiwa mwanafunzi wa pili kufanya vizuri ambapo Alice alikuwa wa tatu na John wa tano.Nilianza kurudisha matumaini ya kukutana kwa mara nyingine tena na watu ambao nilipotezana nao kwa muda wa miezi miwili iliyopita, nilianza kukumbuka na zile ndoto nilizokuwa nikiota nikapata picha huenda ikatokea kweli huko mbeleni.Wazazi wangu walifurahi sana na kunipatia zawadi kemkem, niliwahaidi kutowaangusha katika suala la kujisomea.Ilikuwa siku ya alhamis Afisa Elimu Wilaya alipofika pale nyumbani akiwa na barua kutoka Wizarani ambayo alitusomea kuwa kutokana na kufanya vizuri kitaifa na kuwa mshindi wa pili na wa kwanza kwa wasichana kitaifa tulihitajika kwenda Bungeni kukabidhiwa zawadi pamoja na scholarship.Nilifurahia hiyo safari kwani Afisa Elimu aliongezea kuwa mshindi wa kwanza mpaka wa kumi kitaifa watakuwepo huko, pia ghalama za usafiri wa wazazi na mimi mwenyewe zitalipwa na Serikali.Niliona tarehe za kwenda Dodoma zinachelewa kwani taswira ya Emmanuel ilitawala katika macho yangu....................
Je nini kitaendelea? Ungana na mtunzi wako Jimmy Luoga toleo lijalo hapahapa kwenye blog yetu pendwa ya Archandramu.blog.
Pia usisahau kutuandikia maoni yako
No comments:
Post a Comment