Mtunzi Jimmy Luoga.
SEHEMU:2
ILIPOISHIA:
"Nilipoingia bwenini nilianza kuvua nguo moja baada ya nyingine, nilishtuka nikigusa kitu kama karatasi katika mfuko wa sweta, niliingiza mkono mfukoni na kutoa barua....Je barua hiyo aliiandika nani? Ungana nami katika sehemu hii ya pili.
SASA ENDELEA....
Niliifungua barua hiyo huku mikono yangu ikitetemeka, barua hiyo ilianza hivi; Kwako mpendwa Rose, salaamu nyingi zikufikie hapo ulipo. Naamini hu mzima wa afya. Lengo la kuandika barua hii ni kutaka kuomba urafiki baina yako nami.Japo rafiki yako alitukana matusi makubwa ambayo hayapimiki lakini naamini wewe ni msichana mwerevu na mwenye upeo nafikiri utaweza kutambua kuwa hatukuwa na makosa.Namaliza kwa kuomba unipe jibu la barua yangu kupitia anuani ya shule yetu.Nakutakia masomo mema. Wako katika maisha John Zakayo. Nilijikuta nikiishiwa nguvu za miguu baada ya kuliona jina hilo, kwani nilikuwa na furaha muda wote nikiamini barua hiyo iliandikwa na Emmanuel. Nilikuta furaha yangu ikibadilika na kuanza kuwa huzuni huku nikijiuliza maswali kadha wa kadha, huku swali la kuhusu mtu aliyeniingiza barua hiyo kwenye mfuko wa sweta langu likizidi kuniumiza kichwa."Ina maana Emmanuel alitumwa na rafiki yake John aniletee barua hiyo?..." nilijiuliza moyoni swali hilo huku maswali kadha wa kadha yakiendelea kuuza kichwa changu "Lakini mbona sikumbuki kama Emmanuel nilisogeleana naye jirani?.." niliendelea kujihoji mimi mwenyewe. Kwa kweli usiku huo ulikuwa mrefu sana kwangu, nilipata usingizi kwa Shida kwani mawazo na akili yangu yote ilihamia kwa Emmanuel mvulana ambaye nilihisi nafsi yangu ikimhitaji zaidi.Nilishtuka rafiki yangu Alice akiniamsha twende tukasome, ilikuwa majira ya saa kumi usiku kwani ilikuwa ni desturi yetu kuamka muda huo kwaajili ya kujisomea. Kwakuwa nilichelewa kulala siku hiyo nilimdanganya Alice kuwa nilikuwa sijisikii vizuri hivyo aliniacha mimi nikiendelea kuuchapa usingizi yeye akaelekea darasani.Siku iliyofuata ilikuwa jumamosi, hivyo baada ya kunywa uji mimi na rafiki yangu tulichukua nguo chafu na kwenda kuzifua."We mlokole mwenzio ulimuacha wapi ulipofika kule ukumbi wa muziki?...." Ni wasichana wasumbufu pale shuleni mmoja wao ndiye aliyeuliza swali hilo huku wakisindikiza maneno ya kebehi na vicheko, nilihisi kuumbuka mbele ya Alice ambaye alikuwa hajui chochote juu ya usiku uliopita "Wee komaaa! labda kama umenifananisha, nani aliyekuja ukumbini?" nilikuja juu kama vile sio mimi Rose niliyekwenda katika ukumbi ule wa muziki.Alice hakuwakawiza akanisaidia kuwapa makavu mpaka wakahama eneo hilo, Namshukuru mwenyezi Mungu rafiki yangu huyo alikuwa hasikilizi maneno ya mtu yeyote zaidi yangu.Siku zilizidi kukatika huku nikiendelea kumkumbuka Emmanuel mvulana aliyeiteka nafsi yangu.Siku moja tukiwa mstarini nilisikia jina langu likiitwa na kiranja aliyekuwa anagawa barua, mapigo ya moyo wangu yalinienda mbio kwani sikutambua barua hiyo ilitokea wapi, nilipoichukua niliangalia mhuri ambao ulizidi kunifanya nipate hamu ya kuifungua kwani haikutoka nje ya Morogoro, niliamini aliyeandika barua hiyo hatakuwa mwingine zaidi ya Emmanuel kwani mwandiko huo ulikuwa tofauti na ule wa mwanzo."Rafiki yangu fungua hiyo barua tuisome wote!" alining'ang'ania Alice jambo ambalo nililipinga kwani ilikuwa kawaida yetu kwa kila barua aliyopata mmoja wetu tuliisoma wote, "hivi umeanza lini kukataa kuifungua barua mbele yangu au tayari umepata mchumba shule ya jirani?..." swali hilo lilinifanya nitafutie kisingizio kwa kutoka nje kwa hasira huku barua yangu ikiwa mkononi, Alice alinifuata kuniomba msamaha lakini niliendelea na safari yangu mpaka kwenye ukumbi wa chakula ambao haukuwa na mtu.Nitazama huku na kule kisha nikaifungua barua hiyo, cha kwanza kabisa nilirusha macho mwishoni mwa barua hiyo ambako niliona jina la John kwa awamu nyingine, nilipandwa na ghadhabu tena hata bila ya kuisoma niliichana vipande vipande na kisha kwenda kuitupa chooni.Nilizidi kuumia katika nafsi yangu na kuhaidi kumuandukia barua Emmanuel Japo kimila na desturi za kitanzania ningeonekana najipendekeza, lakini sikujali hilo.Tuliendelea na shughuli za masomo huku nikitafuta siku ya kuandika barua ambayo nilihahidi ningeituma kwa Emmanuel mvulana ambaye nilijuta kumfahamu kwani nilihisi aliutesa zaidi moyo wangu.Siku moja kabla sijaandika barua tukiwa mstarini Mwalimu wetu wa kiingereza alitusomea barua ya mwaliko wa Mdahalo (debate) kutoka shule ya Sekondari Mzumbe ambayo ilitakiwa ifanyike siku ya ijumaa, nilifurahi sana kusikia hivyo kwani niliamini kwenda huko Mzumbe kungenifanya nimuone tena Emmanuel kwa mara nyingine, nilikuwa na asilimia miamoja ya kwenda huko kwani kwa pale shuleni nilikuwa mwenyekiti wa mdalo.Nilihisi siku haziendi kwani siku hiyo Mwalimu wetu wa kiingereza alipotangaza ilikuwa jumanne.Tulianza mazoezi kwa kishindo, siku ya Alhamis nilipata wazo jingine la kuandika barua ambayo ningemkabidhi Emmanuel laiti kama ningeonana naye ana kwa ana.Usiku wa kuamkia ijumaa niliuona unachelewa kukucha, nilipata usingizi wa mang'amung'amu lakini niliposhtuka tayari kulishapambazuka.Mwalimu wa kiingereza aliniita na kuniomba niwaandae wale wanafunzi ambao wangekwenda Mzumbe kwaajili ya mdahalo, sikupata shida kuwaandaa Kwakuwa wote waliohitaji kwenda huko walishiriki katika mazoezi ya maandalizi.Mara baada ya chakula cha mchana ambacho siku hiyo tuliwahishiwa tulianza safari na Lori la shule.Tuliingia Mzumbe Sekondari majira ya saa saba na nusu mchana ambapo tuliwakuta wanafunzi wakitusubiri kwa hamu, nilizidi kufarijika kwani niliamini ningeweza kumtia machoni Emmanuel mvulana ambaye nilihisi huenda ndio mwenyezi Mungu alishanipangia kuwa chaguo sahihi la moyo wangu.Kama ilivyo ada wanafunzi wa Mzumbe Sekondari walitupokea kwa furaha huku tukipeana mikono, furaha yangu haikutimia kwani kila nilipopepesa macho yangu sikuweza kumuona Emmanuel, "Oh! Emmanuel upo wapi?, jitokeze Japo niione sura yako...." nilikuwa nikiongea kimoyomoyo maneno hayo, "Karibu sana Rose jisikie upo nyumbani.." ilikuwa sauti ya upole iliyopenyeza katika ngoma ya masikio yangu, niligeuka na kukutana uso kwa uso na.............
Je, ni nani aliyekutana na Rose? usichoke wala usikose kuungana nami toleo lijayo.Siku njema!!!!
Usisahau kutoa maoni yako pia
No comments:
Post a Comment