Monday, 30 January 2017

MALKIA WA PEMBE ZA NDOVU KESI KUSIKILIZWA TENA FEBRUARI 3

Kesi ya pembe za ndovu inayomkabili mwanamke raia wa China Yang Feng Glan maarufu kama “Malkia wa Pembe” imeahirishwa tena jijini Dar es salaam, Tanzania hadi Februari tatu mwaka huu, ambapo itasikilizwa siku nzima.

Sababu za kuhairishwa kwa kesi hiyo inayosikilizwa kwenye mahakama ya hakimu mkazi kisutu jijini Dar es salaam ni upande wa serikali kushindwa kuleta mashahidi mahakamani wakidai kupewa muda zaidi ili kuwaleta mashahidi mahakamani hapo.

Hata hivyo upande wa mshtakiwa ukiongozwa na wakili Masumbuko Lamwai, umepinga hoja hizo kwa kuieleza mahakama kuwa shauri hilo limekuwa likichukua muda mrefu sababu ya upande wa mashtaka ambao ni serikali umeshindwa kuleta ushahidi mahamani.

Wakili Lamwai ameitaka mahakama kutumia nguvu ya mahakama kutupilia mbali kesi hiyo kwa kuwa serikali ilitakiwa kuleta mashahidi tangu oktoba 2016 lakini wameshindwa kufanya hivyo.

Nao upande wa jamhuri ukiongozwa na wakili mkuu wa serikali Faraja Nchimbi na wakili Elia Attanas umeomba kupewa muda zaidi ili waweze kupitia hoja zilizotolewa na upande wa mtuhumiwa, miongoni mwake ikiwa ni ombi la washtakiwa kwa mahakama kuifuta kesi hiyo.

Akizungumza na sauti ya Amerika nje ya mahakama ya hakim mkazi Kisutu, Hassan Kiango anaelezea zaidi kuhusiana na uamuzi huo wa mahakama, ambapo ameeleza kuwa hakim ametoa onyo la mwisho kwa upande wa serikali la kuwataka kuwaleta mashahidi mahakamani hapo.

Mwanamke wa China Yang Feng Glan anayetuhumiwa kuongoza genge la usafirishaji pembe za ndovu barani Afrika Akipewa jina la utani ìIvory Queenî, anadaiwa kusafirisha pembe za ndovu 706 kutoka nchini Tanzania kwenda Mashariki ya mbali. Glan, 66, anadaiwa kuwa na ukaribu na majangili wa Afrika Mashariki na walanguzi wa China.

No comments:

Post a Comment